Nianze makala kwa kumshukuru Mungu ambaye kwa huruma yake anatujaalia afya njema katika maisha yetu ya kila siku. Tangu tupate Uhuru Desemba 9, 1961 hadi sasa, nchi yetu imekuwa na sifa kubwa ya Watanzania kuishi kwa utulivu na amani.  

Kusema kweli, amani ni hitaji la msingi mno, maana bila kuwapo amani hata mahitaji kama chakula, mavazi na makazi inakuwa shida kuyapata. Mahali ambako hapana amani, hata fursa ya kumwabudu Mwenyezi Mungu ni tabu na vilevile kupata maendeleo kwa watu inakuwa vigumu. Hii ina maana kwamba kama amani haipo misingi muhimu kwa maisha ya binadamu inasambaratika. Hali kama hiyo hujitokeza kwa sababu kila mara watu wanakuwa katika mahangaiko na familia kusambaratika: akina mama na watoto kuathirika zaidi kutokana na mapigano na mizozo. 

Sehemu zenye mapigano ya mara kwa mara hakuna nafasi ya kutulizana na kufanya shughuli za kujiletea maendeleo. Mali na rasilimali nyingine pamoja na fursa za kiuchumi huharibiwa kutokana na vita au mapigano na matokeo yake ni watu kukimbia ili kuyanusuru maisha yao. 

Kwa mfano, sehemu ambazo amani hakuna watu hujikuta ni wakimbizi katika nchi nyingine wakitafuta amani na utulivu. Hivyo uwepo wa amani ni suala la msingi kwa binadamu kwa mambo mengi yanayohusiana na maisha yetu ya kila siku. Amani ikidorora maisha yanakuwa magumu sana. Hivyo, taifa likiwa na amani na watu wake wakaweza kuishi kwa kusikilizana – ni jambo jema sana linalostahili kudumishwa wakati wote. 

Kwa muda mrefu kumekuwapo viashiria vya mizozo kati ya wakulima na wafugaji sehemu mbalimbali nchini. Kwa mfano, katika wilaya za Mvomero na Kilosa mkoani Morogoro yamekuwapo matukio ya kuashiria kuvunjika kwa utulivu na amani kutokana na wafugaji kulishia mifugo kwenye mashamba ya wakulima. Vilevile, nimekuwa nikisikia mizozo kama hiyo sehemu nyingine nchini. Yawezekana pia wakulima wakawa wanavamia maeneo ya kuchungia mifugo. 

Katika harakati kama hizo uwezekano wa kuzuka mifarakano na mapigano ni mkubwa. Katika hali kama hiyo uwezekano wa baadhi ya watu kupoteza maisha yao pia ni mkubwa. Palipo na kutokuelewana na mifarakano kati ya wakulima na wafugaji, mali zinaharibiwa; na isitoshe mifugo huharibu mazao na kusababisha hasara kubwa. Mfano mzuri ni katika Wilaya ya Mvomero, sehemu za Turiani ambako kuna uwekezaji kwenye mashamba ya miwa kwa ajili ya kuzalisha sukari na bidhaa nyingine.

Kwa hali isiyotarajiwa, wafugaji walipeleka mifugo yao kwenye eneo la shamba la miwa (Mtibwa Sugar Estate) na kulisha. Taarifa ya habari ya saa mbili usiku Novemba 22, mwaka huu iliyorushwa na ITV ilionesha uharibifu mkubwa uliofanywa na mifugo (zaidi ya ng’ombe 500) katika shamba la miwa Mtibwa. Habari hiyo ilitolewa na vyombo vingine vya habari kama Jamboleo la Jumatano Novemba 23 (toleo namba 2633) ikiwa na kichwa cha habari “Mifugo 500 yashikiliwa kwa kuharibu miwa ya mil. 800/-”.

Habari ilieleza kuwa hekta 30 za miwa yenye thamani shilingi zaidi ya milioni 800 zimeharibiwa na mifugo. Je, hali kama hii inaashiria nini kwamba wafugaji wana nguvu nyingi kuliko wakulima hivyo wanaweza kufanya wanavyotaka? Kwa nini wafugaji hawataki kuheshimu na kufuata sheria na taratibu zilizopo: kwamba kila Mtanzania anao uhuru wa kuishi sehemu yoyote nchini lakini asivunje sheria.

Utaratibu huo ni kwa kila mtu – awe mkulima; mfugaji; mfanyakazi au mfanyabiashara wakiwamo wawekezaji. Wafugaji hawana haki ya kupeleka na kuchunga mifugo yao kwenye mashamba ya wakulima. Kwa kufanya hivyo wanavunja sheria, hivyo kustahili kushitakiwa. Sheria inatakiwa itekelezwe bila shuruti kwa faida yetu sote. Kama baadhi yetu hatutaki kutii sheria na tukafanya tunavyotaka na hatua dhidi yetu hazichukuliwi: inaonekana ni dalili za kushindikana utawala wa sheria. Nathubutu kusema hivyo kwa sababu matukio ya aina hiyo (mizozo kati ya wakulima na wafugaji) yamekuwa yakijitokeza mara kwa mara wakati mamlaka husika na vyombo vya kusimamia sheria vipo. 

Mimi kama raia wa kawaida najiuliza je, kiburi walichonacho wafugaji hadi waharibu mashamba kwa kuchungia mifugo wapendavyo wanakipata wapi? Haingii akilini unapopata habari kwamba wafugaji katika eneo fulani wameharibu mashamba ya wakulima: kisa kulisha mifugo. Wakati mwingine hata ugomvi unazuka na wanaoathirika ni wakulima kwa kupigwa hata kupoteza maisha. Sasa wakulima wameanza kuwa na hofu. Wengi wanayo hofu kubwa hasa wanapoona makundi ya mifugo yamehamishiwa katika sehemu wanazoishi. Hii ni hatari kwa maana wakulima si tu watahofia mazao yao kuharibiwa na mifugo, bali pia hata maisha yao kuwa hatarini. 

Kwa mantiki hiyo hawatalima kwa bidii wakihofu kupoteza nguvu zao. Hali kama hiyo inapojitokeza inaathiri maendeleo ya wakulima kwa kutopata chakula cha kutosha pia kwa kukosa kipato cha kutosheleza mahitaji yao mengine yanayotegemea rasilimali fedha. Isitoshe, hata sisi tuishio mijini na katika majiji kama Dar es Salaam maisha yetu yanategemea nguvu za wakulima na wafugaji. Tunahitaji chakula na kitoweo. Kunapotokea mizozo kati ya makundi haya mawili; wote tunaathirika.

Vilevile, hali hii inajenga chuki kati ya familia za wakulima na wafugaji kiasi kwamba kutodhibiti hali hiyo tunahatarisha amani yetu. Taifa letu linakaliwa na watu wa aina nne: wakulima, wafugaji, wafanyabiashara (ikiwamo wawekezaji kwenye viwanda) na wafanyakazi za kuajiriwa (salaried labour). Kipato chetu au kuweza kuyamudu maisha yetu ya kila siku kunatokana na jasho letu katika kuyatekeleza majukumi yetu katika sehemu zetu za kazi au mahali tunapoishi. Kwa msingi huo wote tunatakiwa tufanye kazi zetu kwa kutambua kuwa inatupasa kuziheshimu kazi na shughuli zinazofanywa na makundi mengine kwa nia ya kuinua uchumi wetu: mtu mmoja mmoja, familia, jamii na taifa. 

Si mwelekeo mzuri kwa mojawapo ya makundi kudharau kazi, mchango au maslahi ya makundi mengine. Shughuli zote za kiuchumi zinazofanywa na makundi yote zikiimarishwa na kuboreshwa zitakuwa zenye tija kwa maendeleao yetu na taifa letu na hivyo amani kustawi kwa faida yetu sote.

Inapotokea kundi mmoja ndani ya nchi yetu likajenga ubabe na kuwa na mtazamo potofu kwa kuzidharau shughuli za makundi mengine inakuwa ni hatari kwa uhai wa Taifa letu. Mtazamo walionao baadhi ya wafugaji kwamba kila kilicho kijani popote kwao ni halali yao kupeleka mifugo na kuchungia huko, unasababishwa na nini? Je, ni kutokujua (ignorance), mazoea ya kuona kilicho kijani ni rasilimali ya kulisha mifugo bila kujali mipaka au mahali rasilimali hiyo ilipo. Je, uhalali huo kwa wafugaji unatoka wapi?  Ni kutokana na nguvu za kisiasa au ni jeuri ya fedha kwa baadhi ya wafugaji au ni kitu gani hasa? Je, sheria, taratibu na kanuni vimeshindwa kufanya kazi kwa kudhibiti wafugaji kuvamia mashamba ya wakulima? Je, hali kama hiyo itaendelea hadi lini? Je, ni vema kuachia wafugaji waendelee hivyo hivyo bila wahusika (kwa ngazi zote kuanzia Serikali za Mitaa huko vijijini hadi kitaifa) kuchukua hatua stahiki? Maswali haya (na mengineyo) inafaa tuyatafakari kwa kina na tupate majibu kwa pamoja na kuchukua hatua za kudhibiti uharibifu wa mazao ya wakulima kutokana na mifugo kutosimamiwa ipasavyo.

Mifugo ni rasilimali muhimu inayohitajika kwa ustawi wetu na Taifa. Changamoto iliyo mbele yetu ni namna gani wafugaji wanaitumia mifugo yao kuweka rehani maendeleo ya wakulima. Kuna haja kubwa ya kutoa elimu kwa wafugaji ili waheshimu haki za wakulima, lakini pia wafanye shughuli za kuchunga mifugo kulingana na taratibu za matumizi bora ya ardhi vijijini na sehemu nyingine za hifadhi za Taifa. 

Wafugaji wajue mipaka yao, waiheshimu na wajitahidi kutumia rasilimali ardhi zilizotengwa kwa ufugaji (rangelands) kwa umakini mkubwa na kwa misingi endelevu. Ni vizuri pia kwa wafugaji kuelimishwa vya kutosha na kumilikishwa maeneo ya kufugia ili wafahamu uwezo wa eneo na waweke idadi ya mifugo kulingana na uwezo wa eneo husika. Si jambo la busara kwa wafugaji kuwa na mifugo mingi kuzidi uwezo wa maeneo ya kuchungia. Matokeo yake ni uharibifu mkubwa wa mazingira; changamoto inayosababisha wafugaji wahamehame. Kwa kufanya hivyo, wanasababisha uharibifu usiotarajiwa kwenye mashamba. 

Ushauri wangu kwa viongozi wote kuanzia vijijini hadi Taifa zikiwamo serikali za vijiji; watunga sera na wafanya uamuzi (policy & decision makers) pamoja na wanasiasa (politicians): wote kwa pamoja na kwa nia moja wahakikishe mizozo kati ya wakulima na wafugaji inadhibitiwa ipasavyo. Hii ni pamoja na kutenga maeneo maalumu ya wafugaji na kuwamilikisha. Vilevile, wafugaji wapewe elimu na utaalamu juu ya ufugaji bora ili badala ya kuwa na mifugo mingi, waweze kufuga kulingana na uwezo wa maeneo watakayomilikishwa na wayaendeleze wakisaidiwa na wataalamu wa mifugo. 

Kuwepo mipango mahsusi ya kuwezesha wafugaji kufanya shughuli zao kibiashara kwa faida yao na Taifa letu. Wakiwapo ng’ombe wachache wa maziwa na wachache wa nyama kwa kila mfugaji, lakini wenye tija kubwa itakuwa faraja kwa mfugaji mwenyewe na wakati huohuo kuweka mazingira yetu katika hali ya matumaini kuliko kuwa na mifugo mingi yenye tija kidogo na pia kusababisha uharibifu kwa mazingira  na hatimaye kuwapo hali ya kutokuelewana kati ya wafugaji na wakulima. 

Ufugaji bora wa kibiashara unawezekana; uhifadhi wa mazingira pia unawezekana: Tanzania ni moja, hivyo kwa pamoja tushirikiane kudumisha amani na upendo miongoni mwetu hasa wakulima na wafugaji.