Na Deodatus Balile
Kwa muda wa wiki tatu hivi, sijapata kuandika katika safu hii. Ni kutokana na kubanwa na majukumu mengi, ambayo bila kujitoa pengine mengi yangekwama.
Nimepokea simu na ujumbe kutoka kwa wasomaji wangu kadhaa wakihoji kulikoni siandiki? Naomba mniwie radhi katika hili.
Sitanii, kwa hakika nilishindwa kuandika na sababu ya msingi ilikuwa ni maandalizi ya mikutano miwili; Mkutano Mkuu wa Mwaka wa Jukwaa la Wahariri Tanzania (TEF), ambao tumeufanyia Zanzibar, Machi 9, 2022 na maandalizi ya Mkutano wa Siku ya Uhuru wa Vyombo vya Habari Duniani (WPFD), utakaofanyika Arusha, Tanzania Mei 3, 2022.
Hakika mikutano hii imechukua muda wangu mwingi, lakini kwa kuwa yote inalenga katika kujenga taaluma imara, naamini imekuwa heri kuisimamia mikutano hii.
Sitanii, tunaelekea mwezi wa pili sasa, kuna shida kubwa. Baada ya Urusi kuishambulia Ukraine, na Marekani ikaishawishi dunia kuiwekea vikwazo Urusi, uchumi wa dunia umeyumba.
Ikumbukwe Urusi ndiyo mzalishaji namba mbili wa mafuta duniani. Urusi ilikuwa inauza asilimia 40 ya gesi kwa Bara la Ulaya… Ukraine ndiyo mzalishaji wa ngano namba moja duniani.
Nimeifuatilia hii vita inayoendelea. Kwa kususia mafuta ya Urusi, dunia imepoteza wastani wa mapipa milioni 12 kwa siku.
Marekani imetangaza kutoa mapipa milioni moja kila siku kuingiza katika uchumi wa taifa lake. Hizi zinazobaki milioni 11 ni Bara la Ulaya, Afrika na Asia. Kwao Marekani wamejiwekea kinga kwa miezi sita ijayo.
Sitanii, leo mimi sitaki kuzungumza hayo ya kimataifa. Nataka kujadili yanayotuhusu. Inawezekana ni kweli Vita ya Urusi na Ukraine imeharibu mzunguko wa biashara duniani.
Ni kweli kabisa kuwa vita hii imeongeza mafuta katika moto ambao tayari ulikuwa unawaka wa corona. Kwamba, meli ziliacha kusafirisha bidhaa na huduma kwa hofu ya corona.
Kwamba, viwanda vingi huko Ulaya na Asia vimefunga uzalishaji kwa hofu ya corona. Bidhaa na huduma hazisafirishwi tena kutoka mabara hayo kuja Afrika.
Sitanii, yapo yaliyonisikitisha. Kubwa ni kiwango cha uadilifu cha wafanyabiashara wetu. Kabla sijagusa kinachoendelea, najiuliza iko wapi Tume ya Ushindani?
Liko wapi Baraza la Walaji chini ya Tume ya Ushindani? Hivi karibuni nimekwenda kununua nondo, sikuamini.
Duka la kwanza aliniambia nondo moja ya milimita 16 ni Sh 29,000. Moyo ukapiga paa! Hapo ni Bukoba. Nikaenda duka jirani, nikauliza bei ya nondo hiyo hiyo, ni Sh 22,000.
Nikiwa Dar es Salaam, duka moja wakataka kuniuzia rangi ya nyumba ndoo Sh 54,000, nikashtuka. Kwenda duka jingine, nikauziwa ndoo moja Sh 32,000.
Bati la geji 30 lililokuwa linauzwa Sh 17,000 miezi tisa iliyopita, kwa sasa linauzwa Sh 29,000. Ndoo ndogo ya mafuta ya kula tuliyokuwa tunanunua Sh 18,000 miaka mitatu iliyopita, leo inauzwa Sh 65,000.
Mkate tuliokuwa tunaununua Sh 1,200 miezi 15 iliyopita, leo unauzwa Sh 3,000. Kreti ya soda tuliyokuwa tunainunua Sh 10,000, mwishoni mwa wiki imepanda hadi Sh 12,000.
Nilipanga kufungua duka la vifaa vya ujenzi, ambapo Januari niliulizia bidhaa za kuanzia angalau kupamba duka, wakaniambia nitafute Sh milioni 12, nikaanza kutafuta nikijua kufikia Juni nitakuwa nimepata angalau nusu nianze, lakini Jumamosi nilipoulizia kwa mwenye duka la jumla, akaniambia nikitaka kuanza niwe na Sh milioni 30 kwa sasa.
Sitanii, ingawa tunaujua ukweli kuwa vita ya Urusi na Ukraine imeleta shida, ila yatupasa kukataa uhujumu unaoendelea.
Nashawishika kuiomba serikali irejeshe Tume ya Bei. Leo nchi yetu isingekuwa na Mamlaka ya Udhibiti wa Nishati na Maji (EWURA), petroli na dizeli tungekuwa tunanunua lita moja Sh 10,000. EWURA imekuwa mkombozi, imedhibiti bei za mafuta nchini.
Sitanii, naamini baadhi ya wafanyabiashara kwao maadili ni sifuri. Kuamini kuwa watajitathmini na kupunguza bei wenyewe, tunawekeza matumaini kusikostahili.
Nashawishika Tume ya Ushindani wa Haki ibadilishwe haraka na kuwa Mamlaka ya Udhibiti wa Bei kwa Ushindani wenye Maadili.
Mhe. Rais Samia Suluhu Hassan, ufahamu bila kuchukua hatua za haraka kuwadhibiti wafanyabiashara waliojazwa Roho Mtakavitu na si Roho Mtakatifu, nchi wataipeleka kusiko.
Mimi ni muumini wa biashara huria, lakini bila Maadili na Udhibiti inageuka biashara holela. Tumechoka wafanyabiashara kusingizia Urusi na Ukraine, serikali sasa iingilie kuwanusuru wananchi. Mungu ibariki Tanzania.