DAR ES SALAAM

Na Abbas Mwalimu

Urusi inatekeleza kile alichokiita Rais wake, Vladimir Putin, ‘Operesheni Maalumu’ nchini Ukraine aliyoitangaza Februari 24, mwaka huu.

Wakati huu Urusi ikielekea Kyiv ambao ni Mji Mkuu wa Ukraine, Rais wake, Volodymyr Zelensky, ameuomba Muungano wa Umoja wa Kujihami Kaskazini mwa Bahari ya Atlantiki (NATO) umsaidie, lakini hakuna nchi hata moja iliyojibu ombi hilo.

Makala hii inaangazia sababu za Urusi kuingia Ukraine na uhalisia wa NATO kuisaidia Ukraine isikutane na athari zaidi, ikiwamo kutwaliwa kwa Kyiv na athari za vikwazo ilivyowekewa Urusi kutoka Marekani na Umoja wa Ulaya (EU).

Chanzo cha vita

Chanzo cha vita/mgogoro na uvamizi huu wa sasa wa Urusi kinatokana na tishio la kiusalama linaloletwa na NATO dhidi ya Urusi.

Tishio hilo lilianza kushika hatamu baada ya Februari, 2014 Rais wa zamani wa Ukraine, Viktor Yanukovych, kuondolewa madarakani.

Yanukovych aliondolewa madarakani kwa mapinduzi yaliyoungwa mkono na kusaidiwa na nchi za Magharibi baada ya kukataa kusaini mkataba wa ushirikiano wa soko huria na EU, badala yake kujielekeza zaidi Urusi kwa kupatiwa msaada wa fedha na nchi hiyo (Rejea Congressional Research Service Report ya Oktoba 5, 2021 kubaini hili).

Hali hiyo ilisababisha kutokea kwa maandamano makubwa na hatimaye mapinduzi yaliyojulikana kama Mapinduzi ya Heshima (Revolution of Dignity) Novemba, 2013 yaliyosababisha Yanukovych kukimbilia Moscow Februari, 2014.

Hapo ndipo Urusi ilipoanza vita na Ukraine kwa kulivamia na kulitwaa kwa nguvu eneo la Crimea lenye wakazi wengi wenye asili ya Urusi (Rejea tena Congressional Research Service Report ya Oktoba 5, 2021).

Kwa kulitwaa eneo la Crimea, Urusi inaamini  hatua hiyo ilipunguza ushawishi na athari za NATO, hasa Marekani katika eneo la Bahari Nyeusi na Bahari ya Caspian.

Lakini licha ya kufanya hivyo kwa miaka kadhaa sasa, Urusi imekuwa ikiendelea kuhofu namna NATO inavyojipanua kueleka eneo la mashariki mwa Ulaya kwa kupenyeza ushawishi kwa nchi za Georgia, Ukraine na Belarus kimkakati.

Kujipanua huku kwa NATO kunaelezwa na Kremlin kuwa na athari kubwa za kiusalama kwa Urusi katika eneo la mpaka wake wa mashariki mwa Ukraine, hivyo kuathiri kwa kiasi kikubwa wigo wa ushawishi eneo lote la Ulaya Mashariki na kusini mwa Caucasus.

Mkakati wa Urusi katika vita hii umejikita katika namna tatu:-

Mosi, kupunguza ukubwa wa mpaka wa Ukraine. Kwa kawaida ukubwa wa mpaka wa nchi hutoa tafsiri ya namna nchi hiyo inakavyokuwa ngumu kuivamia kama alivyobainisha Sheehan (1996) katika ‘The Balance of Power: History and Theory’ kuwa mpaka wa nchi ni sehemu muhimu katika vita, hasa katika kutafsiri umbali wa kuifikia Ikulu ya nchi.

Hii ndiyo sababu Ikulu nyingi za nchi huwa katikati ya nchi ili kuondoa athari za kufikiwa kwa urahisi na maadui.

Mkakati wa pili ni kuyakamata na kuyakalia maneo ya Luhansk na Donetsk kwa kutumia serikali zinazoendeshwa nyuma ya pazia na Urusi.

Luhansk na Donetsk ni maeneo ambayo kwa miaka takriban minane sasa Urusi imekuwa ikijenga ushawishi yajitenge kutoka Ukraine. Kujitenga kwa maeneo hayo kuna athari kubwa kwa uchumi wa Ukraine.

Urusi imetekeleza mkakati huo kwa kuyatambua maeneo hayo kama nchi huru kupitia kwa makundi yaliyojitenga ya Donetsk People’s Republic kwa kifupi DPR na Luhansk People’s Republic au LPR Februari 22, mwaka huu.

Maeneo haya mawili kwa pamoja yanaunda eneo la Donbas ambalo ni muhimu kwa uchumi wa Ukraine kwa kuwa na viwanda vingi na machimbo ya makaa ya mawe.

Hivyo ‘kuyakalia’ maeneo hayo ni kuuvunja nguvu uchumi wa Ukraine.

Haya yalibainishwa pia na Wasielewski na Jones (2022:2) katika andiko lao ‘Russia’s Possible Invasion of Ukraine’ kwamba kitendo cha Urusi kuyamega na kuyatwaa maeneo ya Ukraine kutaivunja nguvu za kiuchumi nchi hiyo na kuiongezea Urusi nguvu kazi, uwezo wa viwanda na maliasili zitakazoifanya kuwa nchi tishio kwa dunia.

Kwa upande mwingine kuyakalia maeneo hayo kunapunguza zaidi mpaka wa Urusi na Ukraine kuelekea Ikulu ya Ukraine mjini Kyiv kutokea upande wa mashariki, hivyo kuiweka Ukraine katika hatari zaidi.

Mkakati wa Tatu ni kuilazimisha Ukraine isijiunge NATO

Urusi inatekeleza hili kwa kukamata maeneo ya magharibi mwa Mto Dnepr, Odessa hadi Transdniestria ili kuiathiri kiulinzi na kiuchumi Ukraine kwa kuinyima uwezekano wa kutumia Bahari Nyeusi.

Sambamba na hilo, lengo ni kukamata pia maeneo ya Mariupol, Kherson na Odessa. Urusi inaamini kuwa maeneo hayo yanaweza kutumika kwa ajili ya kuwapatia maji wananchi wa Crimea huku Ukraine ikizuiwa isipate mwanya wa kutumia bahari.

Hayo yote yanalenga kuifanya Ukraine ikose njia nyingine zaidi badala yake ilazimike kukaa katika meza ya makubaliano kule Minsk, Belarus na ‘kujitia kitanzi.’

Ni ipi nafasi ya NATO?

Kikanuni NATO inakosa mamlaka ya kisheria kuingia Ukraine na kuilinda nchi hiyo.

Hili liliwekwa bayana na Rais wa Marekani, Joe Biden; Waziri Mkuu wa Uingereza, Boris Johnson na Katibu Mkuu wa NATO, Jens Stoltenberg, baada ya kufanya mkutano na viongozi wakuu wa nchi na serikali wa Umoja huo kwa njia ya video Februari 25, mwaka huu na badala yake viongozi hao wamekubaliana kupeleka vikosi na silaha nchini Poland na Latvia ambazo ni wanachama wa NATO.

Kwanini wapeleke vikosi na silaha Poland na Latvia?

Kimsingi, NATO imeanzishwa kwa mujibu wa Ibara ya 51 ya Mkataba wa Umoja wa Mataifa (UN) (tazama collective defense) wa mwaka 1945 haiwezi kwenda kuingia katika nchi ambayo si mwanachama wake kulinda usalama pasipo kuidhinishwa na Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa (UNSC).

Endapo Ukraine ingekuwa imetia saini Mkataba wa kuanzishwa kwa NATO wa Aprili 4, 1949 leo hii vita ya Urusi na Ukraine ingekuwa kubwa na huenda ingechukua muda mrefu zaidi, kwa sababu ingekuwa mwanachama, hivyo Ibara za 5 na 6 za mkataba huo zingeihusu Ukraine.

Kutokana na hilo NATO inawawia vigumu kupeleka vikosi na silaha kwa kuepuka gharama zitakazokuwa ngumu kuzithibitisha.

Ugumu mwingine wa NATO kuingia unatokana na ukweli kwamba kwa kuwa Ukraine si mwanachama, hivyo uamuzi wa nini kifanywe unatoka UN kupitia UNSC kwa kupiga kura kupitisha azimio la kuilinda nchi hiyo.

Kikanuni, UNSC hufanya kazi zake kwa kuzingatia Ibara ya 39, 40, 41, 42 na 43 za Mkataba wa UN.

Kwa mfano baada ya kupitishwa Azimio namba 1973 mwaka 2011 lililotoa wajibu wa nchi wanachama wa EU kulinda raia nchini Libya (Responsibility to Protect  -R2P) NATO iliwashiwa taa za kijani kupitia ibara ya 43 ya mkataba huo wa UN.

 Azimio la UNSC ni kikwazo cha kusuluhisha mzozo huu kwa sababu mbili. Mosi, nchi iliyo katika vita ni mhusika mkuu wa kuamua uamuzi wa Baraza la Usalama. Pili, upigaji wa kura kupitisha azimio hautoi nafasi kwa Ukraine kusaidiwa.

Ukweli upo hivi; UNSC ina wanachama 15 waliogawanyika katika makundi mawili:-

(1) Wanachama watano wa kudumu.

(2) Wanachama 10 wa kawaida wanaopatikana kwa mzunguko wa kinchi na mgawanyiko wa kikanda.

Mfano wa wanachama wasio wa kudumu ni nchi ya Kenya inayoiwakilisha Afrika kupitia Balozi Kimani.

Kikwazo kwa Ukraine ni Kura ya Turufu (VETO)

Veto ni hadhi ya kura yenye uamuzi mzito ama ya mwisho katika maazimio mbalimbali yanayopitishwa na UNSC.

Hadhi hii ya veto imepewa kwa upendeleo mataifa matano yanayoitwa wanachama wa kudumu wa UN.

Mataifa haya yamepewa hadhi hiyo kutokana na mchango wao mkubwa uliosababisha kuundwa kwa UN.

Mataifa haya ni pamoja na Uingereza, Ufaransa, Marekani, China na Urusi iliyorithi hadhi hii kutoka kwa iliyokuwa USSR.

Upigaji wa kura katika UNSC

Upigaji wa kura za kuidhinisha azimio lolote la UN katika usuluhishi wa migogoro huhitaji angalau kura 9 kutoka miongoni mwa wajumbe 15 wa Baraza la Usalama.

Katika kura hizo tisa, kusitokee nchi mwanachama wa kudumu ikapiga kura ya ‘HAPANA’, azimio hilo haliwezi kupata utekelezaji wenye mantiki hata kama litapata kura zaidi ya 11 za kuliwezesha  kupelekwa kwenye Baraza Kuu la Umoja wa Mataifa (UNGA).

Nani anadhani Urusi itapiga kura kuidhinisha NATO waingie Ukraine?

Kwa msingi huo, hawa wanachama wa kawaida 10 ni kama hawana umuhimu wowote katika uamuzi wa UNSC. Ni kama picha tu zimekaa pale, huo ndiyo ukweli.

Kimsingi mataifa hayo matano hufanya uamuzi wa ‘NDIYO ama HAPANA’ kulingana na jinsi gani yana masilahi katika azimio lililopo mbele yao.

Ndiyo maana Rais Biden aliliona hilo mapema na kusema hatapeleka vikosi Ukraine, watu walimshangaa na walimuona kama mtu mwoga, la hasha! Alijua ugumu ulipo. Ni katika UNSC.

Ni wazi kuwa ikiwa nchi inayojadiliwa ina masilahi ya moja kwa moja na jambo husika kama ilivyo kwa Urusi, hupiga kura ya ‘HAPANA’ kuzuia azimio kupita. Urusi tayari imepiga kura ya HAPANA.

Je, kwa namna UNSC ilivyo, Ukraine itapona?

Lakini udhaifu huu wa UNSC unaleta maswali ya kisheria hasa kuzingatia kanuni za asili za haki  (Principles of Natural Justice) hasa ‘Nemo judex in causa sua’ inayoweka wazi kuwa upande hauwezi kushiriki katika kufanya uamuzi katika jambo ambalo una masilahi nalo.

Urusi imeingia vitani dhidi ya Ukraine kwa sababu ina masilahi na nchi hiyo kwa kuzingatia hofu ya nchi hiyo kujiunga NATO, hivyo kuwa katika hatari ya kupoteza biashara yake ya gesi nchini Ukraine na nchi nyingine za Ulaya ikiwamo Ujerumani. Je, UNSC si kikwazo kwa amani?

Vikwazo vilivyowekwa na Marekani na EU vitasaidia?

Jibu ni kuwa vitasaidia lakini baada ya muda mrefu. Lakini yafaa tujiulize, hadi muda huo ambao vikwazo vitaanza kuonyesha athari Ukraine itakuwa wapi?

Tafiti nyingi zinaonyesha wazi kuwa vikwazo vimekuwa havina athari tarajiwa ukilinganisha na nia au malengo ya nchi.

Hii ndiyo sababu Rais Zelenskyy ameweka bayana kuwa vikwazo pekee havitoshi, bali nchi washirika zinapaswa kufanya zaidi ya hapo.

Kwa mfano Smeets (2018) katika andiko lake  ‘Can economic sanctions be effective?’ lililotoka katika ripoti ya  Machi 15, 2018 ya Shirika la Biashara Duniani (WTO) anabainisha kwa kusema kuwa takwimu za vikwazo vya kiuchumi kuwa na athari ni dhaifu mno.

Smeets anakubaliana na Hufbauer na wenzake (1990) kwa kuweka bayana kuwa vikwazo vina kiwango kidogo cha kuwezesha kufikiwa kwa lengo la kuiathiri nchi husika, akitoa mfano wa Urusi yenyewe ilipowekewa vikwazo mwaka 2014 na Iran iliyowekewa vikwazo kadhaa tangu mwaka 1979, lakini bado zinaendelea kukua kiuchumi.

Mwandishi wa makala hii ni mchambuzi wa siasa na diplomasia. +255 719 258 484