Kumekuwapo mvutano kati ya CCM na Chadema kuhusu uamuzi wa CCM kuwaita viongozi wa taasisi mbalimbali za umma, kujieleza kwenye mikutano ya chama hicho. Chadema wanapinga uamuzi huo. Nnape Nnauye (CCM) na John Mnyika (Chadema) wameingia kwenye malumbano. Hii ni moja ya sehemu ya malumbano hayo.
HOJA YA NAPE
Nimesoma kwa mshangao sana hoja ya John Mnyika juu ya uamuzi wa CCM kusimamia Ilani yake ya Uchaguzi, ambayo licha ya kuchaguliwa kihalali na wananchi mwaka 2010, utekelezaji wake utaleta mabadiliko katika maisha ya kawaida ya wananchi.
Bila shaka ni katika mtikisiko wa kukata roho kwa chama muflisi cha Chadema, ndiyo maana viongozi wake sasa wanakurupuka kutoa matamko yasiyo na kichwa wala miguu, katika kuhangaika kukata roho kwa kujidanganya kijinga tu kwamba wanaweza kuzuia nguvu ya timu mpya ya CCM ambayo bila shaka imewatia homa sana watani. Juhudi hizi ni sawa na kuzuia mafuriko kwa vidole. (Poor Chadema, R.I.P Chadema).
Kama hata kuzisoma na kuzitafsiri sheria na kanuni za utumishi zimewashinda watani wangu hawa, mnawezaje kuongoza nchi? Katika mazingira haya ni bora kukaa kimya badala ya kufumbua kinywa na kuonesha jinsi usivyoelewa nchi inaongozwaje. Sasa sina hakika kama hii tafsiri anayojaribu kuijenga Mnyika (John) hapa ni msimamo wa chama kizima au ni matokeo ya kukimbia shule.
Kama ni msimamo wa chama kizima, basi ni aibu kwa chama ambacho kimeendesha siasa kwa miaka 20 sasa kuwa na mtazamo wa hovyo na wa ajabu kama huu. Kama ni msimamo wa mbunge wangu John, basi si vibaya umri bado unaruhusu kurudi darasani kujaribu kumalizia alichokikimbia shuleni.
Pengine tujaribu kutafakari maswali yafuatayo:-
1. Ilani ya uchaguzi (kama wanafahamu maana yake) inayotekelezwa ni ya nani?
2. Nani anasimamia na nani anatekeleza ilani ya uchaguzi ya chama kilichopo madarakani?
3. Ni lini mwenye ilani anakagua utekelezaji wa ilani yake? Anasubiri miaka mitano? Anamuuliza nani hatua mbalimbali za utekelezaji ukiachilia mbali kwenda na kujionea mwenyewe hatua hizo?
4. Mtiririko gani wa mawasiliano kati ya chama tawala na Serikali yake ili kupata mrejesho kwa wananchi?
Soma kisa hiki
Mtoto wa miaka mitatu anamzuia babaake kuingia chumbani baada ya kufika kutoka kazini akamkuta mamaake anavaa, hivyo mtoto anamwambia baba usiingie chumbani kwani mama anavaa nguo katoka bafuni. TATIZO HAPA NI MTOTO KUTOELEWA MAHUSIANO YALIYOPO KATI YA BABA NA MAMA.
Nape Nnauye ni Katibu wa Itikadi na Uenezi wa Chama Cha Mapinduzi (CCM).
MAJIBU YA JOHN MNYIKA
Nape, nashukuru kwa majibu yako na majibu kama haya haya yaliyotolewa na Naibu Katibu Mkuu wenu Mwigulu Nchemba, naona ni vyema nijielekeze kwenye hoja zako na niachane na vioja vingine.
Ikiwa majibu haya ni msimamo pia wa Mwenyekiti wenu Kikwete (Rais Jakaya Kikwete) na Katibu Mkuu Kinana (Abdulrahman), hakika mnadhihirisha kauli niliyotoa bungeni kwamba tumefika hapa tulipo kwa sababu ya “udhaifu wa Rais, uzembe wa Bunge na Wabunge na Upuuzi wa CCM”.
Kinachoendelea katika suala hili ni sehemu tu ya udhaifu, uzembe na upuuzi huo. Maandishi yako yote hayajajibu hoja, nashauri kwanza soma hapa: JOHN MNYIKA: Balozi Sefue na Yambesi watoe kauli iwapo Serikali imetoa waraka wa maagizo kwa watumishi wa umma kutoa taarifa katika mikutano ya CCM kinyume cha maadili.
Jibu kwanza hoja wakati nikisubiri majibu juu ya kauli yangu hiyo na ile ya awali. Nashauri pia ujijibu mwenyewe hayo maswali uliyoyauliza ili udhihirishe uelewa wako tenge, kuhusu masuala hayo uliyohitaji majibu halafu nitakuja kukupa majibu sahihi kwa kuzingatia Katiba ya nchi, katiba za vyama vya siasa, sheria za nchi, kanuni za nchi, kanuni za vyama vya siasa, maadili ya nchi na maadili ya vyama vya siasa, waraka wa serikali na waraka wa vyama vya siasa. Kama huna majibu unaweza pia kusema, sasa hivi na nitajibu masuala yote kama ulivyohitaji.
Hata hivyo, katika hatua ya sasa ni vizuri nikaweka kwenye muktadha masuala yafuatayo: Kuna tofauti kati ya viongozi na wateule wa kisiasa na watumishi wa umma (political appointees and public leaders vs civil servants); kauli yangu imehusu watumishi wa umma (civil servants) kufuatia kauli yenu ya Mwanza ya kutaka watumishi wa umma wa TANROADS, TANESCO n.k kuja kujieleza kwenye mikutano ya CCM.
Nape na Nchemba mmejikita katika kujibu hoja juu ya wateule wa kisiasa kama mawaziri, nayasema haya kwa kurejea maandiko yenu kwenye mitandao mingine ya kijamii kuhusu kauli yangu. Ni vizuri mkasoma kwanza kauli yangu na kuielewa kabla ya kuanza kujibu.
Ieleweke pia sipingi CCM kusimamia ilani yake pale ambapo ina mamlaka ya kufanya hivyo, na Mwalimu Nyerere aliwahi kusema kwamba, “Chama legelege huzaa Serikali legelege”. Hivyo, ulegelege wa sasa wa Serikali ni matokeo ya ulegelege wa CCM. Tiba yake si kuwaita watumishi wa umma kwenye vikao vya CCM, tiba yake ni kusimamia wateule wa wachaguliwa na wateule wa kisiasa waliotokana na chama chenu wenye wajibu wa kuwawakilisha na pia kusimamia utekelezaji kwenye Serikali.
Rais Kikwete ni mjumbe wa Kamati Kuu ya chama chenu na vikao vingine vyote. Mmewahi kumwita kumhoji kuhusu utekelezaji wa ilani yenu kuhusu maisha bora kwa kila Mtanzania wakati huu ambapo gharama za maisha zinapanda kwa ari, nguvu na kasi zaidi? Waziri Mkuu ni mjumbe wa vikao vya chama chenu, Kinana anasema mawaziri watajieleza kwenye NEC, hivi kabla ya kuwaita mawaziri kujieleza; mmewahi kumwita Waziri Mkuu na kumwajibisha?
Mnaweza kuwaita viongozi wa kisiasa wateule wenu kuwahoji kwenye vikao vyenu, lakini si watumishi wa umma kama ambavyo nitaeleza kwa kirefu kwa mujibu wa Katiba, sheria, kanuni na maadili baada ya majibu yako.
Kwa upande mwingine, kitendo cha mawaziri sasa kuitwa kuhojiwa kwenye NEC ni ishara ya udhaifu wa Rais kama Mwenyekiti wa Baraza la Mawaziri katika kuwasimamia mawaziri hao na uzembe wa wabunge wa CCM katika kuwasimamia mawaziri bungeni kwa kiwango ambacho sasa kazi hiyo inataka ifanywe na watu wengine.
Katika mazingira hayo, Watanzania wakiwamo wanachama wa CCM wana sababu ya kumlipa mshahara Rais na kuwalipa wabunge wenu huku kazi inaenda kufanywa na NEC? Je, mnataka kuwaambia Watanzania kwamba vyombo vyenu hivyo vimeshindwa kufanya kazi zake ipasavyo za kuisimamia Serikali kutekeleza ilani na chama kutoa sera na uongozi wa ujumla?
Hali hii unaweza kushuka ngazi ya chini kwenye Halmashauri na kwenye taaasisi na mashirika mengine kwenye ngazi mbalimbali. Hivi ina maana mameya na madiwani wenu katika maeneo ambayo mnatawala wana udhaifu na uzembe kwa kiwango ambacho sasa mnataka wakurugenzi wa Halmashauri na maafisa wao (watumishi wa umma) wakajieleze kwenye vikao vya CCM vya wilaya kinyume cha Katiba, sheria, kanuni na maadili?
Kwa mfano wa Nyamagana kwa kutaka TANROADS na TANESCO wakajieleze vikao vya CCM vya mkoa na wilaya, hivi maana yake mna mkuu wa mkoa na Kamati ya Ushauri ya Mkoa (RCC), mkuu wa wilaya na Kamati ya Ushauri ya Wilaya (DCC) wenye udhaifu na uzembe kwa kiwango cha sasa watumishi wa umma wa mashirika (watumishi wa umma) hayo wakajieleze ndani ya vikao vya CCM.
Katiba ya chama chenu tayari ilishaweka mfumo ambao kwa misingi ya utawala bora na demokrasia si sawa, lakini ni mfumo uliovumilika kwa miaka mingi wa wakuu wa wilaya na mikoa kuwa sehemu ya kamati za CCM za mikoa husika, hawa wateule wa kisiasa ndiyo waliopaswa kwenda kwenye vikao vya chama chenu na kutoa hizo unazoziita taarifa za utekelezaji wa ilani na wanayo fursa ya kukutana na hao watumishi wa umma.
Kwa hiyo, kama kweli mngekuwa na dhamira ya dhati ya kubadilika, si kufanya ‘danganya toto’ mngeanza kwanza kuwawajibisha hao kwa kushindwa kutimiza wajibu wao!
Mmejaribu kuigeuza nchi kuwa dola ya kipolisi ukirejea matukio kama ya Ulimboka, Mwangosi n.k baada ya kuambiwa msikimbilie polisi, mnayo hamu ya kurejesha mfumo wa chama kushika hatamu katikati ya mfumo wa vyama vingi. Afadhali wakati wa Nyerere chama kilishika hatamu kwenye mfumo wa chama kimoja na kutoa uongozi, sasa chama hakishiki tena hatamu, kinatafuta ‘utamu’, utamu wa kubaki madarakani baada ya kuzidiwa na M4C na utamu wa kufanya ufisadi kupitia ofisi za umma.
Katika hili la kuwataka watumishi wa umma wahudhurie vikao vya CCM na kutoa taarifa kwa lazima (na wala sizungumzii mawaziri kuzungumza kwenye mikutano yenu ya hadhara kwa nafasi zao za kichama) hamko sahihi. Na iwapo ni mfumo mpya wa utawala na utamaduni mpya wa kisiasa mnataka kuuanzisha fanyeni hivyo, na sisi tutawaita waje kwenye mikutano yetu na mtaona matokeo yake.
Nitaeleza zaidi ukijielekeza kwanza kujibu hoja kwa hoja kutokana na kauli yangu; JOHN MNYIKA: Balozi Sefue na Yambesi watoe kauli iwapo Serikali imetoa waraka wa maagizo kwa watumishi wa umma kutoa taarifa katika mikutano ya CCM kinyume cha maadili na pia ukajibu mwenyewe hayo maswali yako uliyouliza, iwapo huna majibu yake; nitakusaidia kujibu.
John Mnyika ni Mkurugenzi wa Habari na Uenezi wa Chadema. Pia ni Mbunge wa Ubungo na Msemaji Mkuu wa Kambi Rasmi ya Upinzani Bungeni wa Wizara ya Nishati na Madini.