*Wabunge wajiandaa kukwamisha tena bajeti ya Wizara ya Nishati, wahoji zabuni ya mafuta BP
*Wajiandaa kuwang’oa Waziri Profesa Muhongo, Katibu Mkuu Maswi Ijumaa ya wiki hii
*Katibu Mkuu aanika ukweli, asema Wizara yake haikufanya manunuzi waliohusika ni RITA, Zitto anena
Kuna kila dalili kuwa imeibuka vita ya wazi kati ya Wizara ya Nishati na Madini na Shirika la Umeme Tanzania (TANESCO), huku Mkurugenzi Mkuu wa Tanesco aliyesimamishwa kazi, William Mhando, akipigiwa debe la wazi na wabunge.
Taarifa zilizopatikana kwenye ofisi za Bunge zinasema kuwa Kamati ya Nishati na Madini inajipanga kukwamisha bajeti ya wizara hiyo kama Mkurugenzi Mkuu wa Tanesco aliyesimamishwa kazi, Injinia Mhando, hatarejeshwa kazini huku wizara ikisisitiza kuwa amesimamishwa kazi kupisha uchunguzi wala hajafukuzwa.
Kwa upande wake, Mwenyekiti wa Kamati ya Bunge ya Hesabu za Mashirika ya Umma, Zitto Kabwe, naye ana msimamo kuwa Mhando ameonewa na wizara inaweza kujiokoa kwa kumrejesha ofisini kisha ufanywe uchunguzi maalumu utakaoendeshwa na Ofisi ya Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Serikali (CAG).
“Unajua kilichopo ni mvutano baina ya Kamati (ya Bunge) na Katibu Mkuu (Maswi). Yeye anasema alikiuka Sheria ya Ununuzi wa Umma kwa sababu ya uzalendo. Anasema mimi Munde na Sara Msafiri tunafanya biashara ya matairi na Tanesco, ndiyo maana tunaipigia debe Tanesco.
Aliwaambia waandishi wa habari kuwa tangu alipoteuliwa aliwaambia wazi watumishi wa wizara hiyo kuwa anataka kurejesha heshima ya Serikali ndani ya Wizara ya Nishati na Madini, anataka kuondoa ubadhirifu na la mwisho ni kuwa na uwazi katika kazi
zinazofanywa na wizara.
“Nimewaambia wazi kuwa asiyeyaweza hayo afunge mizigo aondoke,” alisema Maswi.
Mhando adaiwa kuomba msaada wa Simbachawene
Awali, Katibu Mkuu aliiambia JAMHURI kuwa Mhando alikuwa amepita kwa Naibu Waziri Simbachawene akimtaka amsaidie kumlinda, kwa maelezo kuwa Katibu Mkuu hampendi yeye (Mhando).
“Mhando alikwenda kwa Naibu Waziri Simbachawene akamwambia anaomba amlinde kwani mimi simpendi. Simbachawene akamwambia Waziri Muhongo, Waziri akamwambia Simbachawene mwambie Katibu Mkuu, akaniambia.
“Mimi nikamwita. Nikamwambia unasema sikupendi kivipi? Nikamwambia mimi Kama Maswi na wewe kama Mhando tunaweza kuwa marafiki lakini urafiki wetu si wa MD au Katibu Mkuu. Hivi ni vitu viwili tofauti. Nilimwita nikamuuliza mimi nikupende wewe unataka uwe mchumba wangu?
“Tangu mwanzo niliwaambia wakurugenzi wote msijipendekeze kwangu. Mtu anayetaka kuja kwangu afanye kazi. Mhando akawa hafanyi kazi, anazunguka anatafuta jinsi ya sisi kukubaliana naye tumsaidie. Anatuma watu nimsaidie kufanya kazi, nimsaidie nini? Kufanya kazi ipi?
“Siku moja nikamwita nikamwambia nikusaidie nini? Mimi nafikiri hunielewi. Nikamwambia wewe ni rafiki yangu kama Mhando na Maswi, lakini kama MD na Katibu Mkuu ni vitu viwili tofauti,” alisema Maswi.
Mhando atuhumiwa kumpa kazi mkewe
Tuhuma nyingine anazochunguzwa nazo Mhado kwa sasa ni kwamba alimpatia mke wake zabuni ya kuuza stationery kupitia kampuni ya Santa Clara. Kampuni hii imepewa mkataba wa Sh milioni 800 kuiuzia Tanesco.
Mke wa Mhando sasa anafahamika kama Eva Stephen William wakati zamani alifahamika kama Eva Stephen Mhando.
Mikataba 23 inachunguzwa, lakini pia mitatu inayofanyiwa kazi mara moja ni ununuzi wa mita za Luku kwa bei mara mbili ya bei halisi, mkataba wa ku-supply stationery na ununuzi wa vifaa vyenye ubora usioridhisha.
Mboma adaiwa kumpigia debe Mhando
Wiki ya Juni 17, Mwenyekiti wa Bodi ya Tanesco, Jenerali mstaafu Robert Mboma, anadaiwa alikwenda Dodoma na Mhando wakiwa kwenye gari moja kufanya uzengezi kuhakikisha Mhando anarejeshwa madarakani, lakini inadaiwa aligonga mwam ba. Juhudi za kumpata Jenerali Mboma zimegonga mwamba kwani simu yake inaita bila kupokewa.
Maswi ahoji nia ya wabunge
Akizungumza na waandishi wa habari jana, Maswi alihoji inakuwaje wabunge wanamtetea kwa kiwango kikubwa Mhando aliyesimamishwa kazi kwa utaratibu sawa na ilivyotokea kwa Mkurugenzi Mkuu wa Shirika la Viwango Tanzania (TBS), Charles Ekelege, lakini hakuna anayependekeza Ekelege aendelee kuwa kazini wakati uchunguzi ukiendelea?
“Alikuja kwenye Kamati tarehe 17 Juni may be (labda) akidhani amepata kitu kinaschotaka kugawa wajumbe. Kama wajumbe, mimi nikawaambia wajumbe hawa ikithibitika nafanya biashara na Tanesco niko tayari kujiuzulu hadi ubunge. Hata hivyo, si kosa kufanya biashara isipokuwa unapaswa ku-declare interests (kutangaza mgongano wa kimasilahi).
“Zedi akamwambia ulitaja majina ya wabunge wanaofanya biashara na Tanesco yeye akasema sikutaja. Mwenyekiti akamwambia Katibu Mkuu ‘nadhani una matatizo’. Sara akasema hafanyi biashara yoyote na Tanesco na akamtaka atoe vithibitisho… Katibu Mkuu akasisitiza kuwa hajawataja hao wabunge,” alisema Tambwe.
Mbunge huyo alisema Serikali inawachanganya, kwani wakati wizara inadai Tanesco wanaiba bilioni 60 kila mwezi, CAG amelipatia shirika hilo hati safi.
“[Christopher ole] Sendeka akamwambia tatizo lako Maswi unataka ubabe na Sara [Msafiri] akamwambia Katibu ukiwa mchawi utakula watoto wa jirani unamaliza, kisha utakwenda kula wa kwako,” alisema Tambwe akiwakariri wabunge hao wakimsihi Maswi aachane na mpango wa kumsimamisha kazi Injinia Mhando.
Alisema bajeti ya mwaka jana iligomewa Serikali ikasema itawapa hela ya mpango wa dharura Sh bilioni 408, lakini hadi leo Tanesco wananunua umeme bei kubwa kisha wanauza kwa bei ndogo. “Nasema suluhisho ni kununua mitambo ikamilikiwa na Tanesco si kuendelea na utaratibu huu wa kukodisha,” alisema.
Hata hivyo, Tambwe alisema vita yote iliyopo ni kwamba wizara na Tanesco wanagombea kununua mafuta kwani huko ndiko kwenye ulaji.
Msafiri amsema Maswi
Mbunge wa Viti Maalum ,Sara Msafiri (CCM), alipoulizwa tuhuma dhidi yake alisema: “Hizo ni mbinu chafu zinazofanywa na Katibu Mkuu Maswi na Waziri wake kuwatisha, kuwaziba midomo na kuwagawa wabunge hasa wajumbe wa Kamati ya Nishati na Madini.
Kwenye kikao Katibu Mkuu wa Wizara alitakiwa kuthibitisha tuhuma hizo, walisema wanayo orodha ya majina ya wabunge wanaofanya biashara, lakini ndani ya Kamati ya Nishati na Madini hakuna yeyote anayefanya biashara na taasisi zilizo chini ya Wizara ya Nishati na Madini.
“Aidha, si dhambi kwa Mbunge kufanya biashara, anachotakiwa ni kutangaza ili kuepuka mgongano wa kimasilahi.”
Zitto aitahadharisha wizara, Waziri Mkuu
Kwa upende wake, Mbunge wa Kigoma Kaskazini, ambaye pia ni Mwenyekiti wa Kamati ya Hesabu za Mashirika ya Umma, Zitto Kabwe, anasema anachopinga ni unyanyasaji dhidi ya watumishi wa umma na si vinginevyo.
“Sijatangulizwa na mtu kumtetea Mhando, kwani ni wajibu wangu kama Mwenyekiti wa Bunge wa Kamati ya Mashirika ya Umma kuhakikisha kwamba mashirika yanaendeshwa kwa mujibu wa sheria na kanuni.
“Philosophia ya ‘eyes on hands off’ ndiyo inayotakiwa itumike. Sitaki micro-management (wizara kuingilia). Na hii si mara ya kwanza. Consolidated Holding nilimwonya [Mustafa] Mkulo kuingilia mashirika alipomsimamisha [Methusela] Mbajo nilihakikisha anarejeshwa kazini.
“Mimi ni muhanga wa kuonewa. Mtu ambaye hajaonewa ndiye anayeweza asimtetee mtu anayeonewa. Katika suala la Tanesco, Waziri na Katibu Mkuu wako wrong (wamekosea).
“Sina masilahi Tanesco, sina biashara Tanesco, sijahongwa, naongea kwa uzoefu. Hata Dk. Rashid wakati anashambuliwa nilisimama kumtetea kwa sababu naamini katika ukweli.
Nimeiambia Kamati kwenye Tanesco ‘they are wrong’ (wamekosea). Waziri Mkuu [Mizengo Pinda] nimemwambia action ya Tanesco is wrong. Inawezekana Tanesco kuna uchafu lakini hatua hazichukuliwi kwa njia hii.
“Nikiwaacha Maswi na Muhongo kufanya haya bila kuhojiwa, itawazuia nini mawaziri wengine kufanya walichokifanya? Nimezungumza nao wote – Waziri Mkuu, Maswi, Muhongo, [George] Simbachawene – nikawaambia mrejesheni ofisini Mhando.
“Kagasheki aliposimamisha watu waliosababisha faru kuuawa, sikusema kwani alifuata utaratibu. [Dk. Harrison] Mwakyembe alipomsimamisha Mkurugenzi Mkuu wa ATC nilimuonya Mwakyembe kuwa ‘you are wrong’ (umekosea), bahati yule Mkurugenzi Mkuu wa ATC alikuwa hajathibitishwa kazini ndiyo ikamuokoa.
“Nilimzuia Mwakyembe kumsimamisha Mkuu wa Chuo cha Mabaharia (DMI), nikamwambia ukim-touch (ukimgusa) tutakumaliza. Inawezekana kabisa wanatetea haki lakini kuna taratibu za kufuata.
“Tanesco walitoa tenda na BP wakabid, Camel Oil wakabid, lakini BP wakabid bei kubwa kuliko wote hawa. Walibidi Sh 1,900 kwa lita wakati wengine walibid Sh 1,800. Baadaye kwa mlango wa nyuma wakaenda ku-negotiate kuuza kwa bei ndogo. Kwa nini waliposhindwa tenda wakaenda mlango wa nyuma kuuza kwa bei ndogo?
“Tunafurahi kwamba tumepata mafuta kwa bei ndogo, lakini Wizara ‘is a different procurement entity’ (taasisi tofauti ya ununuzi), hata kama unafanya hayo manunuzi, kwa nini kwanza usingekwenda kuwafuata hao Oryx na Camel Oil ukasema tupunguzie wakakataa ndipo ukachukua hatua hiyo?
“Katibu Mkuu si ‘procurement authority’ (si mamlaka ya ununuzi). Kwa nini yalitumika mazungumzo kati ya Katibu Mkuu na kampuni? Kwa nini hukuandika barua PPRA kuomba wakushauri? Nikamwambia hii ingekulinda.
“Nimehoji matukio mawili yanatofauti gani? Edward Lowassa ameng’olewa Uwaziri Mkuu si kwa sababu amepewa hela, kwa sababu Richmond haikupewa hata senti tano bali sheria ya manunuzi haikufuatwa. Hilo tu ndilo lililomgharimu Lowassa… kwa nini leo tusema sheria ya manunuzi haiwahusu hawa? Kwa sababu si Lowassa au Rostam [Aziz]?
“Baadhi ya wabunge wanataka Maswi na Muhongo waondoke, mimi nasema hapana.
Isije ikawa kwa sababu tuna ubavu tuwatimue tu, ninachosema Mhando arudishwe kazini. CAG atafanya ukaguzi ukweli ujulikane. Mimi nimekwenda kufanya ukaguzi miezi miwili iliyopita nimekuta PPRA imetoa clean certificate kwa Tanesco. Kama tunahisi kuna uchafu ambao hawakuuona tufuate taratibu,” alisema Zitto.
Suala la wabunge kufanya biashara na Tanesco, alisema hata yeye amezisikia tuhuma hizo kuwa wabunge hao wanatumiwa na mfanyabiashara mwenye asili ya Kiasia (jina limehifadhiwa), kuuza matairi na bidhaa nyingine kwa Tanesco lakini hana uthibitisho wa taarifa hizo.
Alimshangaa Waziri Muhongo kwa kusema Tanesco inakusanya Sh bilioni hadi 70 na inatumia bilioni 11 tu kulipa mishahara, hivyo akataka fedha zinazobaki wazitumie kulipa madeni.
“Asilimia 86 ya mapato ya Tanesco yanalipa makampuni yanayozalisha umeme – Songas, IPTL, Symbion na mengine. Na hii mikataba imeingiwa na Serikali. Kwa mfano, Symbion sasa wana mkataba wa miaka 20. Mimi nilimwambia Katibu Mkuu kuwa mnawapa Symbion zabuni ya kuzalisha umeme megawati 300 huko Mtwara, hivi Marekani ikiamua kuiteka nchi hii tutatokea wapi?
Zito aliwataka viongozi wa Wizara ya Nishati na Madini na Tanesco kuacha vita ya kupitia kwenye vyombo vya habari, Mhando arejeshwe kazini na CAG afanye ukaguzi maalumu kwenye shirika hilo.
“Sitaki Maswi aonewe, wala sitaki yeyote aonewe. Ninaumizwa mno na vurugu zinazoendelea kati ya wizara na Tanesco. Hii ni vita ya masilahi waachane nayo. Tunataka umeme hatutaki maneno,” alisema Zitto.
Zitto alikemea alichokiita utamaduni wa kuwaona watu wenye maoni fulani na waliyonayo baadhi ya watu kuwa wamehongwa. “Ni utamaduni wa hovyo sana.”
Zitto alisema inawezekana Katibu Mkuu Maswi amefanya uamuzi wa kununua mafuta kutoka BP/Puma kwa nia njema, kisha akamnukuu Mwalimu Julius Nyerere: “Njia ya kwenda Jehanamu imejaa nia njema’.”
Maswi aanika ukweli wa mambo
Katibu Mkuu wa Wizara ya Nishati na Madini, Maswi, kwa upande wake jana alikutana na waandishi wa habari na kusema wabunge wajiepushe na upotoshaji usio wa lazima, kwani Wizara ya Nishati na Madini haikufanya ununuzi wa mafuta, badala yake wizara hiyo ililipa tu na kazi ilifanywa na Wakala wa Vizazi na Vifo (RITA) ambaye kwa amri ya mahakama ndiye mfilisi wa IPTL.
“Ni vizuri ikaeleweka kuwa mwishoni mwa mwaka 2010/11 kulikuwa na mgawo mkubwa wa umeme nchini, hivyo Serikali kulazimika kuingilia kati kuhakikisha mgawo huo unaondolewa na kuitaka IPTL kuwasha mitambo yake katika kiwango cha MW 100. Aliyefanya hivyo ni Mkurugenzi Mtendaji wa Tanesco na si Wizara.
“Ikumbukwe pia wakati IPTL ilipokuwa inasimamiwa na RITA kwa kuwa kulikuwa na amri ya kuifilisi (under liquidation)… Tanesco walipeleka barua RITA wakitaka mafuta ya kuendesha mitambo yapatikane. Ieleweke kuwa ili kuendesha mitambo ya IPTL kwa siku moja tunahitaji MT 500.
“Tarehe 24 Juni 2011, Mtendaji Mkuu wa RITA aliandika barua PPRA yenye Kumb. Na. BD.27/249/01/19 kutoka mwongozo na ushauri juu ya ununuzi wa mafuta ya kuendesha mitambo ya IPTL kwa dharura na barua hiyo ikajibiwa na Mtendaji Mkuu wa PPRA, tarehe 28 Juni, 2011 kwa kumpa njia na mwongozo wa kutumia wakati wa dharura kwa kufuata Sheria ya Manunuzi na bila kukiuka utaratibu.
“Mtendaji Mkuu wa RITA kwa barua yake yenye Kumb. Na. ADG/OR/1/2008/IPT/VOL. II/47A ya Julai 2011 na kupokelewa wizarani siku hiyo hiyo, alionyesha mchakato wa manunuzi uliofanyika na taratibu zinavyotakiwa.
“Baada ya kupokea barua hiyo na kutokana na hali ilivyokuwa, hakuna aliyekuwa tayari kuhangaika na IPTL wala mafuta hadi nilipoteuliwa kuja kukaimu hapa tarehe 22 Julai 2011 na kuanza kazi tarehe 25 Julai 2011. Fedha zinazosemwa zililetwa wizarani ni za Serikali na si za Tanesco, Afisa Mwajibikaji (Accounting Officer) ni wa Wizara si Tanesco,” alisema Maswi.
Alisema Kanuni ya Ununuzi wa Umma Na. 42 ya Mwaka 2005 inampa mamlaka afisa anayewajibika na fedha kufanya manunuzi hata nje ya mipaka yake kwa masilahi ya uchumi wa taifa.
“Napenda ifahamike wazi kuwa hapa kilichofanyika ni kuwa RITA ndiye aliyefanya ununuzi, sisi wizara tulifanya kazi ya kulipa tu,” alisema na kuongeza kuwa fedha zilizotumiwa ni za Serikali na hazikutoka Tanesco kama inavyoelezwa.
Alisema suala jingine ni kwamba wakati kampuni zilizopewa zabuni awali kuuza mafuta Tanesco zilikuwa zinauza kwa gharama ya Sh 1,800 kwa lita, BP/Puma wanauza lita hiyo hiyo kwa Sh 1,460. Pia BP ni mbia wa Serikali kwa asilimia 50 kwa 50 tofauti na kampuni zinazong’ang’aniwa ambazo ni binafsi. “Kuokoa Sh bilioni 2.7 za walipa kodi si fedha kidogo,” alisisitiza.
Alisema kampuni zilizokuwa na zabuni ya kuuza mafuta Tanesco zilikuwa zikinunua mafuta kutoka BP, walionyimwa zabuni ya kuuza mafuta kisha zinaiuzia Tanesco, kitu alichosema kinahitaji kuchunguzwa kwa nini iwe hivyo.
Mkopo wa Sh bilioni 408 kwa Tanesco
Maswi alisema mkopo huo una riba kubwa na utalipwa na wananchi, hivyo Serikali imeamua kwa njia nyingine wakati taratibu za kufuatilia mkopo zikiendelea, yenyewe imekuwa ikitoa ruzuku kwa Tanesco na hadi sasa imekwishatoa zaidi ya Sh bilioni 222.4. Alisema hadi juzi Serikali imetoa ruzuku ya Sh bilioni 25 kwa Tanesco, hivyo watu wasiibe wimbo wa bilioni 408 ambazo ni gharama kubwa kwa walipakodi.
Maswi asisitiza mambo makuu matatu
Kama ilivyokuwa mwaka jana, siku chache kuelekea kwenye bajeti ya wizara hiyo ilipokataliwa, kuna kila dalili kuwa zamu hii suluba bado itakuwa kubwa kwa viongozi wakuu wa wizara hii; Waziri Profesa Sospeter Muhongo na Katibu Mkuu wake, Eliakimu Maswi, kwani wabunge wameshaanza kurusha mashambulizi.
Kikao cha Kamati ya Bunge Julai 17
Katika kikao cha Kamati ya Bunge ya Nishati na Madini cha Julai 17 kilichofanyika mjini Dodoma, imeelezwa kuwa kilijaa vijembe, maneno mazito na kutunishiana misuli kati ya wabunge na uongozi wa Wizara ya Nishati na Madini.
Huku Kamati hiyo ikiwa na msimamo kuwa Prof. Muhongo na Katibu Mkuu Maswi wajiuzulu kwa wanachokiita kashfa ya kuipatia Kampuni ya Puma zabuni ya kuuza mafuta kwenye mitambo ya IPTL bila kufuata taratibu za ununuzi wa umma, wizarani nako kuna hisia kuwa baadhi ya wabunge wanajifanya kuitetea Tanesco kumbe wanatetea masilahi binafsi yanayobanwa na uongozi mpya wa wizara usiokuwa tayari kuyumbishwa.
Mbunge wa Viti Maalum, Munde Tambwe (CCM), aliliambia Gazeti la JAMHURI kuwa Katibu Mkuu wa Wizara ya Nishati na Madini, Maswi, alimpigia simu Mwenyekiti wa Kamati hiyo, Seleiman Zedi, na kumwambia baadhi ya wabunge wanafanya biashara na Tanesco ndiyo maana wanashinikiza Injinia Mhando arejeshwe kazini.