Vipimo ni muhimu sana kwa maendeleo ya afya. Kupitia vipimo tunaweza kutambua mustakabali wa afya zetu, hivyo kujiweka kwenye nafasi nzuri katika kupambana na maradhi mbalimbali. Hivi karibuni takwimu kutoka Shirika la Afya Duniani (WHO) zilionyesha kuwa idadi ya wanaume watu wazima wanaopatiwa vipimo vya afya ni ndogo kuliko idadi ya jinsia nyingine.

Kupata vipimo sahihi na kwa wakati sahihi ni kitu muhimu sana ambacho mtu anapaswa kukifanya kwa afya yake. Kufanya vipimo kunasaidia kuyagundua magonjwa mapema kabla hayajaanza kuonyesha dalili, wakati ambao ni rahisi zaidi kutibika.

Magonjwa kama saratani, kisukari, yakigundulika mapema itamsaidia mgonjwa kumuepusha na matokeo hasi ya magonjwa hayo kama vile kusababisha kupoteza nguvu za jinsia, uwezo wa kuona na hata vifo vya mapema.

Kupitia makala hii tutaviona baadhi ya vipimo muhimu sana ambavyo wengi  hawavitilii maanani. Lakini ukweli ni vipimo muhimu sana na vikiendelea kusahaulika, madhara yake kwa afya ni makubwa sana.

Vipimo vya tezi dume

Ukweli ni kwamba ni wanaume wachache sana wanaofikiria kupata vipimo hivi vya tezi dume. Mwanamume anakuwa hatarini zaidi kupata tezi dume kadiri umri unavyozidi kusogea, kuanzia umri wa miaka 50 hivi.

Shirika la Afya Duniani limethibitisha kuwa tezi dume ni ugonjwa unaoua zaidi wanaume ukiongozwa na saratani ya mapafu, na sababu kubwa ni kutopata vipimo mapema.

Habari njema ni kwamba tezi dume ni moja ya magonjwa machache ya aina za saratani ambayo uwezekano wa kupona upo kwa zaidi ya asilimia 90 iwapo itagundulika katika hatua za awali. Hivyo, ni vema kufanya vipimo vya saratani mara kwa mara, hasa kuanzia umri wa miaka 55.

Vipimo vya saratani ya utumbo mpana

Saratani ya utumbo mpana ni moja ya saratani zinazoua kwa kasi sana. Japo takwimu zinaonyesha kuwa wanaume wana nafasi ndogo zaidi ya kupata ugonjwa huu kuliko wanawake, lakini hii haimaanishi kuwa wanaume wajisahau kuhusu saratani ya utumbo mpana, hasa tukizingatia ukweli kuwa saratani inaweza kumpata mtu yeyote.

Mara zote saratani ya utumbo mpana inaanzia kwa kuota uvimbe mdogo ndani ya ukuta wa utumbo na kadiri vimbe hizo zinavoongezeka ndipo zinapotengeneza saratani ya utumbo mpana.

Njia ya kuzuia saratani hii ni kuondoa hizi vimbe zinazoota mapema kabla hazijatengeneza saratani. Na njia pekee ya kuzigundua vimbe hizi ni kupata vipimo mapema.

Inashauriwa kuanza vipimo vya saratani ya utumbo mpana mara kwa mara kuanzia umri wa miaka 50 kwa sababu katika umri huu mtu anakuwa hatarini zaidi kupata ugonjwa huu.

Vipimo vya saratani ya ngozi

Ngozi kwa kuanza kubadili rangi na mwonekano halisi wa ngozi.

Wanaume wapo hatarini kupata aina hii ya saratani mara tatu zaidi ya wanawake kutokana na sababu za kibailojia. Lakini sababu hatarishi za ugonjwa huu kwa ujumla wake ni kupigwa jua kwa muda mrefu.

Hivyo, inashauriwa watu kupata vipimo vya ngozi mara kwa mara, hasa pale dalili mbalimbali zinapojitokeza kwenye ngozi, kama vile kubadilika kwa maumbile ya ngozi, kubadilika kwa rangi ya ngozi na kujitokeza kwa chunusi sugu mara kwa mara, kwa kuwa hizi ndizo dalili za saratani ya ngozi (melanoma).

Tiba ya magonjwa ya ngozi inaleta tija zaidi wakati ambapo vipimo vikifanywa kwa wakati na kugundua tatizo.