Kwanza naomba nianze kwa kuwapa pole waandishi wa habari wote waliokutana na zahama ya kipigo kutoka polisi wakati wakitekeleza majukumu yao halali.
Ni majukumu yaliyoandikwa na Katiba ya nchi ya kutafuta habari ili waweze kuuhabarisha umma, ndani na nje ya nchi. Ni tukio lililojiri siku za hivi karibuni.
Kwa upande wangu, hili ni tukio la aibu iliyopindukia mipaka kufanywa na Jeshi la Polisi. Ni tukio la kujipaka kinyesi, na sasa ni dhahiri jeshi letu linanuka uvundo wa aibu, ambao naamini ungeweza kuonewa aibu hata na polisi wa kikaburu enzi za akina Rais Peter Botha wa Afrika Kusini.
Kama ambavyo ni ukweli ulio dhahiri kwamba hakuna mwandishi wa habari anayeweza kufanya kazi zake kwa usalama bila uwepo wa Jeshi la Polisi, kwa upande mwingine ni ukweli ulio dhahiri pia kwamba kwa wakati wa sasa na wakati mwingine wowote.
Jeshi la Polisi haliwezi kufanya kazi zake kwa mafanikio yanayoonekana bila uwepo wa waandishi wa habari. Kwa mfano, taarifa za mafanikio ya Jeshi la Polisi kudhibiti, kukamata au pengine kuua majambazi hatari yenye silaha, zimekuwa zikisambazwa na waandishi wa habari. Kwa namna moja au nyingine, usambazaji wa taarifa hizo umekuwa ukiwatisha majambazi wengine watarajiwa, na hivyo kuwafanya wasitishe azma ya kutekeleza uovu wao.
Jeshi la Polisi Kanda Maalum ya Dar es Salaam, likiongozwa na Kamanda Suleiman Kova, wamekuwa wakisaidiwa sana na vyombo vya habari, pale wanaposema “Tunawaonya wahalifu wasithubutu, Jeshi la Polisi limejipanga sawasawa”.
Upo wakati mwingine waandishi wa habari wamekuwa wakiwapiku na kuwawahi polisi na makachero wao, kwa kufukunyua taarifa na habari ambazo zimekuwa zikiwasaidia sana polisi wenyewe katika kutekeleza majukumu yao.
Ni siri ya wazi kwamba wakati mwingine umma unawaamini sana waandishi wa habari kuliko polisi. Imekuwa ni rahisi waandishi wa habari kupenyezewa taarifa nyeti kuliko makachero wa polisi (ikizingatiwa kwamba polisi wananuka tuhuma za kuvujisha siri za wasiri wao).
Ni polisi juha tu atakayefikiri anaweza kufanya kazi bila ushirikiano na waandishi wa habari, hali kadhalika, ni mwandishi juha tu anayefikri anaweza kufanya kazi kwa usalama bila uwepo wa polisi.
Pamoja na kwamba Jeshi la Polisi linafanya kazi (tena wakati mwingine kwa weledi wa hali ya juu), lakini kazi hizo zimekuwa zikionekana kupitia mikono na midomo ya waandishi wa habari. Akina Kova leo hii tunawaona kuwa ni wachapa kazi, siri ikiwa ni moja tu — mikono na midomo ya waandishi wa habari.
Uandishi wa habari ni noble profession. Mikono ya waandishi wa habari ina uwezo mkubwa wa kutengeneza amani. Leo hii naweza kwenda Kyela au Nyasa bila hofu yoyote baada ya vyombo vya habari kusambaza taarifa kwamba hakuna vita kati ya Malawi na Tanzania.
Narudia. Kwa vyovyote vile, uandishi wa habari ni kazi ya heshima. Ni fani na taaluma kama zilivyo taaluma nyingine zozote zile. Inapaswa na zaidi, inastahili kuheshimiwa na kuenziwa kama zinavyoenziwa taaluma nyingine.
Hivi nchi haitazizima kwa taharuki siku itakapotokea polisi (wetu hawa) kuwafuata makazini kwao madaktari, walimu, wahandisi, mahakimu na majaji, manesi au wanataaluma wengine, na kuanza kuwatembezea mikong’oto huku pia wakiwasakizia mbwa?
Nchi inapaswa kuzizima na kutaharuki kutokana na kitendo cha Jeshi la Polisi kuwafuata waandishi wa habari kwenye “maeneo” yao ya kazi na kuwashushia kipondo cha mbwa mwizi. Waandishi hao wamepigwa na polisi wakati wapo kazini wakitekeleza majukumu yao halali ya kutafuta habari ili kuuhabarisha umma — ndani nje nchi.
Ofisi ya mwandishi wa habari ni ndani na nje ya jengo. Lazima atembee huku na kule kutafuta taarifa sahihi ili kuwalisha walaji. Taarifa za kupewa kwa kuitwa, tuseme na polisi, huchujwa sana (angalia taarifa za kipolisi za watuhumiwa wanaokamatwa wazima na baadaye kufia mikononi mwa polisi katika mazingira yenye wingu zito la utata).
Ni kauli ya kebehi na dharau kubwa kwa taaluma ya uandishi wa habari kwamba waandishi wanapaswa kusubiri kuitwa ili wapewe habari. Kwamba waliopigwa hawakualikwa. Ni kauli ya kifedhuli, si ya kistaarabu, kidhalimu na inayosigina waziwazi Katiba ya nchi. Ni muhimu, na tena ni lazima, msemaji wake na walioratibu waandishi kupigwa wakaadabishwa kwa kuburuzwa mahakamani.
Nirudie tena kwa mara nyingine, uandishi wa habari ni fani adhimu. Katika kipindi hiki ambacho karibu mifumo yote ndani ya nchi, imeoza, imevunda, imebomoka na kusambaratika kwa kiwango cha kutisha, kimbilio pekee la wengi, tena wale wanyonge, ni vyombo vya habari, kupitia kwa wanahabari.
Ni siri nyepesi kwamba polisi kunanuka rushwa, Mahakama zetu zimevunda kwa rushwa, TAKUKURU ni dhaifu kama ubua na taasisi nyingine nyingi muhimu pia zimegubikwa kwa tope zito la rushwa!
Licha ya upungufu na udhaifu wake, vyombo vya habari pekee ndivyo vilivyobaki kuwa kimbilio la wanyonge. Mifano ipo lukuki. Nitaurejea mmoja tu. Ule wa mauaji yaliyofanywa na polisi ya wafanyabiashara wasio na hatia kutoka Mahenge, Morogoro.
Vyombo vya habari vilifanya kazi yake. Mamlaka nyingine, hasa polisi (wapelelezi na waandaa mashtaka) walidoda.
Kwa mujibu wangu mwenyewe, kinachofanyika sasa, siyo matukio ya bahati mbaya.
Ni mkakati mahususi unaosukwa kwa umakini wa hali ya juu, kudhoofisha kwa kuudhalilisha uandishi wa habari, kwamba inaonekana ni fani ya ovyo, isiyokuwa na hadhi wala heshima, na waliomo humo ni watu wa ovyo na waganga njaa wasiokuwa na tija yoyote kwa Taifa hili. Kwamba ni fani nyepesi kabisa.
Ni fani inayobakwa, kunajisiwa na kudhalilishwa mchana kweupe na watu ambao pengine wapo pale walipo kwa vyeti vya kufoji, vyeti vya wajomba zao au walipenyezwa kwenye ajira kwa mfumo wa “Idara ya Uhamiaji.”
Vipigo hivi vya polisi kwa waandishi wa habari vinaudhalilisha uandishi wa habari kwa kiwango cha juu sana. Upungufu upo, sawa. Si kwamba waandishi wa habari hawajui mipaka yao ya kazi. Ukiondoa udhaifu wa wachache, wanajua maadili na miiko ya kazi yao.
Freeman Mbowe ni habari, tena habari kubwa tu. Hakuna mwandishi wa habari aliyepewa jukumu la kufuatilia habari zake za kuhojiwa na polisi, angebaki ofisini kusubiri habari za kuletewa na Msemaji wa Jeshi la Polisi, SSP Advera Senso.
Ni lazima angelazimika kwenda karibu na eneo la tukio, kwani mbali ya Mbowe mwenyewe kuwa ni habari, uwepo wake bado una uwezo wa kuzalisha habari nyingine motomoto. Bahati mbaya waliofanikiwa kuzalisha habari motomoto za ziada kutokana na uwepo wa Mbowe, ni polisi wenyewe.
Kuwapo eneo la tukio ili kuripoti habari sahihi ni wajibu wa mwandishi. Ben Kiko (miaka hiyo) hakusubiri kuletewa habari za vita wakati majeshi yetu shupavu yakimsulubu nduli Idi Amin. Walikuwapo msitari wa mbele na hatukusikia wakipigwa risasi kwa madai ya kuingilia shughuli za kijeshi vitani.
Uandishi wa habari ni fani maalum yenye majukumu maalum. Nakumbuka wakati fulani hata Baba wa Taifa, Mwalimu Julius Nyerere, aliwahi kuvisifu vyombo vya habari nchini kwa kufanya kazi nzuri kuliko hata vyama vya siasa.
Vipigo vya polisi dhidi ya waandishi wa habari si vya kukenuliwa meno na kuchekewa. Waandishi wa habari wenyewe na sisi wananchi wa kawaida ambao tegemeo letu kubwa na la pekee kwa sasa ni vyombo vya habari, tunapaswa kuungana pamoja na kuvikemea kwa nguvu zetu zote.
Ni vitendo vinavyoanza kuota mizizi taratibu vikitaka kuifanya kuwa nyonge fani ya uandishi wa habari. Ni vitendo ambavyo hatupaswi kuviacha vikue na kushamiri. Tusiviache vikageuka kuwa ni utamaduni wa kawaida.
Tukigeuza kuwa ni utamaduni wa kawaida, waandishi wa habari watadhalilika, na vyombo vya habari vitapuuzwa.
Ni vitendo vinavyoanza kama mzaha.
Tukio kubwa la kwanza ni polisi kumlipua kwa bomu mwandishi wa habari wa Kituo cha Televisheni cha Channel Ten, Daudi Mwangosi. Mkubwa wao aliyesimamia mauaji hayo, akapongezwa bungeni na kupandishwa cheo. Mwandishi wa habari aliyeuawa akachukuliwa kama aina fulani ya mdudu — unaweza kufananisha na nzi.
Katika tukio hilo la mauaji ya Mwangosi, waandishi wengine walipigwa na polisi. Mbegu ya polisi kuwadhuru wanahabari inapandwa, inamwagiliwa na kupaliliwa ili ianze kukua.
Vitisho dhidi ya waandishi vinaendelea kukua. Katika matukio ambayo polisi walionesha wazi kupuuzia kuyafanyia kazi kwa weledi wanaojigamba kuwa nao ni pale waandishi akina Ndimara Tegambwage na Saeed Kubenea walipovamiwa ofisini kwao, kucharangwa mapanga na mwingine kumwagiwa tindikali, Absalom Kibanda kupondwa na vitu vizito, kunyofolewa kucha na kutobolewa macho.
Vipo vifo tata vya waandishi wengine kama akina John Lubungo. Wakati anakufa Kova alikuwa RPC Mbeya. Zipo taarifa kwamba alikuwa akifuatilia mtandao uliokuwa ukijihusisha na biashara ya dawa za kulevya, ambao pia ulikuwa ukiwagusa baadhi ya wakuu wa huko.
Kuonesha kwamba polisi wanawadharau na kuwapuuza waandishi wa habari, weledi wao hufanya kazi kwa kasi ya ajabu pale polisi wenyewe wanapodhuriwa. Hapa napo nitoe mfano mmoja tu hai. Mauaji ya kamanda Barlow kule Mwanza.
Polisi hawajawahi kuwa rafiki wa kweli wa kikazi na waandishi wa habari. Nina uzoefu wa kutosha. Polisi wanawahitaji waandishi wa habari, lakini kamwe hawajawahi kuwapenda. Katika harakati zangu za uandishi wa habari nashukuru kukurupushana na polisi wakati bado walikuwa hawajavumbua “Teknolojia” mpya ya kuwalipua waandishi wa habari kwa mabomu.
Ila vitisho vya kufungiwa jiwe kubwa shingoni na kwenda kutoswa nikiwa hai katika mto Ruaha, nilikuwa nikivipata. Kwa hila na njama za polisi hao, hata gerezani nilikaa.
Hata hivyo sikutoka bure huko gerezani. Baada ya kuachiwa huru, kwa ujasiri kabisa niliandika maovu mbalimbali yaliyomo gerezani.
Mwaka 1996 niliwahi kuandika habari katika moja ya magazeti hapa nchini, hasa habari maarufu ya “Alfajiri hadi alfajiri Keko, au mfululizo wa makala zenye kichwa cha habari, “Mfungwa anamiliki roho, mwili ni mali ya gereza”.
Kwa mujibu wangu mwenyewe tena, waandishi wa habari wenyewe kwa namna moja au nyingine mmekuwa mkichangia kudharaulika kwa fani yenu. Huo ni ukweli mchungu. Mmemeguka vipande vipande, hamna umoja wa dhati, ikithibitishwa na utitiri wa kutisha wa vyama vyenu ndani ya taaluma pana ya uandishi wa habari. Kuna ugonjwa pia wa kutopendana.
Inasikitisha, wapo waandishi wa habari ambao huonekana kushangilia madhila yawapatayo waandishi wenzao. Ni aibu. Walikuwapo waandishi waliomsuta marehemu Mwangosi kwamba alijitakia kifo, kwamba alikuwa mwanaharakati! Kilichopaswa kuwaunganisha ni kuuawa kikatili na polisi kwa mwandishi mwenzao wa habari.
Si vibaya. Mnaweza kuwaiga hata hao polisi. Huwa wanashikamana kwa umoja wa hali ya juu pale baadhi yao wakikabiliwa na tuhuma fulani. Wanaotoswa ni wale wenye gundu tu, au walio dhaifu hutolewa kafara kuwalinda wenye nguvu.
Mifano ni mingi. Zipo taarifa kwamba washtakiwa wa mauaji ya wafanyabiashara wa Mahenge walikimbizwa haraka haraka mahakamani bila kushtakiwa kijeshi, hivyo walionekana bado wapo kazini, na jamaa zao waliendelea kukinga mishahara yao kila mwezi. Upelelezi ulikosewa makusudi, mashtaka yao yaliandaliwa ovyo kwa makusudi! Hao ni polisi. Hubebana sana kwenye maovu (solidarity in evil).
Mfano mwingine ni ule wa Askari wa Usalama Barabarani, walionaswa na kamera za mwanahabari Jerry Muro wakikusanya rushwa wazi wazi barabarani. Wenye gundu walitoswa, wengine tunawaona bado wanadunda kazini, wakiendelea kukusanya pesa za rushwa barabarani kama kawaida.
Waandishi wa habari wasiungane kwa kuiga uovu huo, bali waungane kulinda hadhi na heshima yao. Utamaduni ulioanza kujengeka wa kupigwa na kudhalilishwa na polisi wakati wakitekeleza majukumu yao must be nipped at the bud. Ukomeshwe sasa na wakati wote usirudiwe. Labda tu tuambiwe sasa kuwa uandishi wa habari ni uhalifu ndani ya nchi hii.
Katika kipindi hiki ambacho polisi wanafanya juhudi kubwa kudhalilisha na kudhoofisha uandishi wa habari, ni muhimu pia kuangalia upungufu wa kitaaluma na kuufanyia kazi ili kulinda hadhi na heshima ya tasnia ya habari nchini.
Sisi wananchi wanyonge tuko nyuma yenu. Mnafanya kazi nzuri katika mazingira magumu, yakiwamo maslahi duni, hasa kwa waandishi wa habari wa kujitegemea ambao ndiyo roho ya vyombo vingi vya habari nchini.
Nyinyi ndiyo handaki letu salama ambao mmekuwa mkitupigania. Sauti zenu zikizimwa watakaotamba ndani ya nchi ni maovu, mafedhuli, manduli, majizi, majambazi, wauaji, wabaka haki za raia na mafisadi wa kila dizaini na kila sampuli.
Nihitimishe tu kwa kusema ‘a pen is mightier than a gun’.
Mungu wabariki waandishi wa habari Tanzania. MUNGU IBARIKI TANZANIA
0765-892 476.