Kinyume cha ulemavu wa fikra ni upevu wa fikra. Ili upate upevu wa fikra ni lazima kuelimishwa na juhudi binafsi za kusaka maarifa. Lakini pia kusikiliza na kujifunza kutoka kwa wengine. Kwa viongozi ni muhimu sana kusikiliza maoni kwenye jamii ili waweze kujua fika matatizo na changamoto ndani ya jamii husika.
Kiongozi mwenye ulemavu wa fikra hawezi kuongoza vizuri. Ni muhimu kiongozi kusikiliza na kupata maoni mbalimbali kutoka kwa wananchi ili ayachambue na kuyatafutia ufumbuzi; hii ni njia mojawapo ya kuelekea upevu wa fikra.
Kwa vile mifumo yetu ya kutoa maoni bado si mizuri, na majukwaa ya maoni tuliyonayo sasa hivi bado hayako imara na kujitegemea, ni muhimu viongozi wetu wasome magazeti yote ili wapate maoni mbalimbali kutoka kwa wananchi. Hata magazeti ya udaku yana maoni, viongozi wetu wasione soni kuyasoma.
Ninasema magazeti, na kusisitiza magazeti na si mitandao ya kijamii, maana kule kwenye mitandao ya kijamii kila mtu anajisemea. Hakuna mhariri. Kila mtu ni mhariri na kila mtu kwenye mitandao ya kijamii ni mwandishi wa habari. Kwa vile magazeti yetu yana wahariri na waandishi wa habari, ni bora kuendelea kuyategemea zaidi kwenye kupasha habari muhimu na za uhakika.
Hata hivyo mimi si miongoni mwa wale wanaotaka kuifungia mitandao ya kijamii. Maana mitandao hii iko kwenye mfumo wa teknolojia, na ukweli ni kwamba teknolojia inaendelea kusonga mbele na kila kukicha ni lazima italeta jipya.
Sheria yoyote ya kupambana na teknolojia labda kama ni ya kubadilisha kila mwaka, maana teknolojia itaendelea kuleta mapya na kuizuia ni ndoto. La muhimu ni kutengeneza mfumo wa maadili wa taifa letu. Au kuilazimisha mitandao ya kijamii kuratibiwa, ikawa na mhariri au mtu wa kuwajibika yakijitokeza yasiyofurahisha. Utakuwa mfumo wa busara zaidi ya kufikiria kuifungia mitandao ya kijamii.
Mfano, yakitokea makosa kwenye gazeti, au habari za kupotosha – ni rahisi kuwawajibisha wahusika. Kuna mfumo na watu wanajulikana. Mhariri anajulikana na wamiliki wa vyombo hivyo vya habari wanajulikana. Kwenye mitandao ya kijamii ni vigumu kidogo.
Pamoja na sheria zilizotungwa za kuidhibiti mitandao ya kijamii, bado teknolojia inaendelea kusonga mbele na muda mfupi itakuwa kazi kubwa kuweza kupambana na teknolojia. Ni muhimu kuwajenga watu kifikra ili waweze kuchuja na kuacha, kuliko kupoteza muda kwa kutunga sheria ambazo baada ya muda mfupi zitaonekana ni kichekesho. Tunaweza kupambana na teknolojia kwa kujikomboa kifikra na si vinginevyo.
Kuna utamaduni uliojengeka wa kila Mtanzania kusoma gazeti lenye mwelekeo wake. Kuna magazeti ya vyama vya siasa, kuna magazeti ya serikali, kuna magazeti ya watu binafsi na kuna magazeti ya dini. Na kuna wale ambao wao wanasoma magazeti ya Kiingereza au ya Kiswahili peke yake.
Ni muhimu viongozi wakayasoma yote, ya Kiswahili na ya Kiingereza. Bahati mbaya ni kwamba magazeti karibu yote yametumbukia kwenye siasa za vyama vyingi. Huwezi kulipata gazeti linaloandika bila kuegemea upinzani au serikali na chama tawala. Ni vigumu kuikwepa siasa, hata kama huipendi, maana wanatwambia kwamba maisha yenyewe ni siasa.
Kama wewe ni msomaji makini, ukiliangalia gazeti fulani utaona ni la chama tawala au linaunga mkono chama tawala. Na ukiligeukia jingine, unaona hili ni la chama cha upinzani au linaunga mkono upinzani. Lakini kuna magazeti yanayojitahidi kuwa katikati bila kuegemea upande wowote, ila yakifanya uchambuzi ambao unaigusa serikali, basi serikali itasema hayo ni ya upinzani, na yakifanya uchambuzi unaowagusa wapinzani, watasema hao wamenunuliwa na serikali. Nafikiri hakuna ubaya wowote, kama watu na hasa viongozi wangekuwa wanayasoma magazeti yote. Ni vema kufahamu na upande wa pili wana hoja gani. Hili ni muhimu sana kwa viongozi na hasa wale wanaojitokeza kutaka kuongoza kwa haki na usawa.
Nilishangaa sana siku za nyuma kidogo nilipomsikiliza Rais mstaafu wa Awamu ya Tatu, Benjamin Mkapa, akizungumza kwenye mkutano wa Kigoda cha Mwalimu na kulaumu waandishi na wachambuzi kwamba hawakufanya uchambuzi wa kina juu ya kwa nini mchakato wa Katiba ulikwama; hilo lilinifanya kufikia hitimisho kwamba viongozi wetu hawasomi magazeti yote. Inawezekana kabisa Mkapa anasoma magazeti fulani na kubagua mengine:
Nakumbuka, kabla ya Bunge la Katiba kuanza, wakati Tume ya Mabadiliko ya Katiba iliyoongozwa na Jaji Joseph Warioba ikifanya kazi yake, watu waliandika mara nyingi wakipendekeza kwamba ili Bunge la Katiba lifanikiwe, wabunge wa Bunge la Muungano na wale wa Baraza la Wawakilishi wasiingizwe kwenye Bunge la Katiba.
Kama kuna kitu kililikwamisha Bunge Maalumu la Katiba mpya kwa kiasi kikubwa ni kosa hilo la kuwaingiza wabunge wa Bunge la Muungano na la Wawakilishi kwenye Bunge Maalumu la Katiba mpya. Katika nchi nyingine, kama vile Uganda, wale wanaoshiriki kutunga katiba mpya, ambao ni wajumbe wa Bunge Maalumu la Katiba, hawaruhusiwi kugombea ubunge kwa kipindi cha miaka mitano.
Ina maana, wakiwa kwenye Bunge Maalumu, wanakuwa na nia moja ya kutunga katiba bila kuangalia masilahi yao binafsi. Tulipigia kelele jambo ili, tuliandika mara nyingi. Kama Mkapa alikuwa hasomi magazeti yetu hayo, kuibuka na kusema kwamba waandishi hawajadili hoja za msingi ni jambo la kushangaza sana.
Mbali na hili la kutoruhusu wabunge kuingia kwenye Bunge Maalumu la Katiba, tulipigia kelele tunu za taifa letu. Kwamba tuwe na mambo ambayo yeyote atakayechaguliwa, hawezi kuyabadilisha. Kwamba watu waruhusiwe kuendesha siasa zao, lakini watambue kwamba kuna mambo muhimu ya taifa letu ambayo ni lazima kila mtu ayapigie goti. Jambo hili halikufanyika. Tunabaki kutegemea mapenzi ya mtu. Akija kiongozi anapenda jambo fulani, basi litatekelezwa. Akija kiongozi anachukia jambo fulani basi litakatazwa. Tunabaki kuomba kiongozi huyo awe na mapenzi na taifa letu, vinginevyo ni hatari kubwa. Maana, kwa katiba tuliyonayo rais ana madaraka makubwa ya kuweza kufanya chochote jinsi anavyotaka. Kama hana mapenzi na taifa ni hatari.
Pia, tuliandika na kupiga kelele kwamba Bunge la Katiba lisipige kura ya kuipitisha katiba ile. Lakini sote tulishuhudia jinsi ilivyopitishwa hata kwa wafu na wale ambao hawakuwepo kwenye ukumbi kupiga kura ya kuipitisha. Ilipitishwa kwa nguvu na ubabe.
Tumejenga utamaduni ule wa “kiongozi hashindwi” hata kama kushindwa kwake kuko wazi hata kwa mtoto mdogo anayenyonya kidole. Na wale wanaoishi nyakati hizi kwa bahati mbaya, walisema kuipitisha Katiba ile, ni kumpatia Rais mstaafu wa Awamu ya Nne, Jakaya Kikwete, zawadi. Katiba, kitu cha kuyaongoza maisha ya Watanzania wote, kinatengenezwa kama zawadi kwa mtu mmoja. Ni aibu kubwa.
Sipendi kuingilia yale yaliyopendekezwa na wananchi kwenye Tume ya Mabadiliko ya Katiba, lakini yakatupiliwa mbali na Bunge Maalumu la Katiba. Labda kusisitiza kwamba waandishi na wachambuzi waliandika juu ya mambo haya yaliyotupwa na kuonya kwamba kufanya hivyo ni kupuuza maoni ya wananchi.
Magazeti yapo, akiyataka Mkapa tunaweza kumpelekea. Asiendelee kusema kwamba waandishi wa Tanzania hawachambui na kuandika hoja za msingi. Labda aseme wanafanya hivyo kwenye magazeti asiyotaka kuyasoma. Na hilo litakuwa ni tatizo lake binafsi, wala si la Watanzania wote.
Tulisema na kuandika wazi kabisa kwamba vyama vya siasa viliuteka mchakato wa Katiba mpya. Badala ya kuangalia masilahi mapana ya taifa letu, vyama vya siasa vikaweka mbele masilahi ya vyama vyao. Chama tawala cha CCM kilitaka kubaki madarakani, hivyo kilitaka kutengeneza katiba ambayo itakilinda kubaki madarakani. Vyama vya upinzani navyo vikafanya kosa lile lile, vikawa vinataka kutengeneza katiba ambayo itakiondoa Chama Cha Mapinduzi madarakani.
Hili limekuwa kosa kubwa la vyama vya upinzani hadi leo hii. Wanapambana na CCM, badala ya kupambana na mfumo wa “kibabe.” Badala ya kupambana kujenga falsafa nzuri ya kuliongoza taifa letu. Bila kutengeneza falsafa ya kuleta upevu wa fikra, hata Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema), wakiingia madarakani leo hii, watarithi ‘ubabe’ wa madaraka. Maoni haya yameandikwa mara nyingi kwenye magazeti yetu, hasa magazeti ya Kiswahili. Viongozi wetu kama wanasoma magazeti ya Kizungu, labda hawakuyapata haya.
Tuliandika na kupiga kelele kwamba watu waache utamadui huu wa kuchanganya mapenzi ya vyama vya siasa na utaifa. Maana ilifikia wakati ambapo wale wa chama tawala waliwaangalia wa vyama vya upinzani kama wasaliti au watu wa kutoka taifa jingine, na kujiaminisha kwamba ukiwa CCM, wewe ndiye mtanzania. Tulipigia kelelele jambo hili. Kama Mkapa hakutaka kuyasikia haya huko nyuma, hawezi kujitokeza sasa hivi na kusema kwamba waandishi wa Tanzania hawajui kuchambua na kujadili hoja za msingi.
Kuchambua na kujadili hoja za msingi si lazima uegemee kwa yale ambayo mtu unayapenda na kuyaunga mkono. Ni pamoja na yale yote yanayoigusa jamii yetu ya Tanzania na dunia nzima kwa ujumla. Si lazima yawe mazuri kwa upande wa mtu mmoja mmoja au yawe mabaya kwa mtu mmoja mmoja, ni kila upande kukubali kupoteza na kupata, kukubali kutoa sadaka na kujitoa mhanga kwa faida ya watu walio wengi, ni uzalendo na kulipenda taifa.
Huo ndio kuwa na upevu wa fikra. Mtu anayefikia hatua hii anakuwa kabisa amejikomboa kifikra. Na hii ni muhimu sana kwa viongozi wetu, maana wao wakiwa na fikra pevu ni lazima wataisambaza kwa wananchi wote wanaowaongoza na wala si kuwatawala.
Tumeandika mara nyingi na kufanya uchambuzi wa kina ili kuonyesha kwa nini ni muhimu kuirudisha Rasimu ya Tume ya Warioba. Ni nani anasikiliza? Rasimu ya Tume ya Warioba haikuangalia vyama vya siasa. Iliangalia masilahi mapana ya taifa letu.
Ni kweli inawezekana ina upungufu wa hapa na pale, maana ni vigumu kuwa na Katiba iliyokamili na kujitosheleza, lakini mzee Warioba ni lazima apewe sifa, maana alikubali kuweka mapenzi ya chama chake cha CCM pembeni ili atengeneze Katiba ya Watanzania wote. Wajumbe wote wa Tume ya Warioba ni Watanzania waliotukuka, maana walikuwa wanatoka vyama tofauti na itikadi tofauti, lakini walikubali kuzika tofauti zao ili kututengenezea rasimu ya kizalendo.
Kama kuna kitu Tanzania imeweza kufanikisha kama taifa moja lililoungana ni Rasimu ya Katiba Mpya, iliyotolewa na Tume ya Katiba kwa kuongozwa na mzee Warioba. Hapana shaka kwamba amani na utulivu vitakuja kwenye taifa letu tukiikumbatia rasimu hii iliyozikwa na Bunge Maalumu la Katiba. Tunaomba Rais mstaafu wa Awamu ya Tatu, Benjamin Mkapa, ayasome haya. Na tunawaomba viongozi wetu wayasome haya na kusikiliza maoni ya Watanzania ili wapate upevu wa fikra.
Ni bahati nzuri kwamba bado tuna rais wastaafu watatu. Hawa wakikubali kuyasoma maoni ya Watanzania yanayochambuliwa kila siku kwenye magazeti yetu, ni wazi watakuwa msaada mkubwa wa kusukuma wazo hili la Katiba mpya. Wazee hawa kwa busara na hekima zao wanaweza kumsaidia Rais John Magufuli kukubali na kuona uhitaji wa haraka wa Tanzania kuwa na Katiba mpya. Yote haya yatawezekana tu kwa kukumbatia na kukubali upevu wa fikra.