Nimepata kumsikia kiongozi mmoja wa siasa hapa nchini akisema hawezi kuipongeza serikali, yeye ni mzalendo. Serikali kufanya jambo zuri ni wajibu wake. Yeye ni opposition. Yupo hapo ili kuangalia mambo ambayo hayajatekelezwa, hayajafanywa vizuri na serikali.

Anasema serikali ikifanya vizuri ni wajibu wake. Ni wajibu wake, imeomba kura ili ifanye vizuri. Kwa hiyo yeye yupo hapo ‘kuipointi’ serikali ambayo haijafanya vizuri. Yupo kuikosoa serikali kama haifanyi mambo vizuri.

Nimemsikiliza kiongozi huyu wa kutoka mkoa ulioko Kanda ya Nyanda za Juu Kusini akielezea siasa, propaganda na mwenendo wa demokrasia nchini. Binafsi sipo katika dondoo hizi. Isipokuwa nimeguswa na mambo matatu ndani ya mazungumzo yake: ukweli, wajibu na uzalendo.

Kiongozi anapokuwa mkweli katika kauli na matendo yake, anajenga mvuto kwa watu kumsikiliza na kumfuata. Anajenga heshima yake na ya watu anaowaongoza. Anavunja uzandiki na hiana miongoni mwa watu. Katika hili ni viongozi wachache ambao wana tabia ya kuzungumza ukweli, ambao huthibitishwa na matendo yao.

Ukweli ni kama nyundo inayopigilia msumari katika ubao. Ukweli ni kama msumeno unaokata mti mbele na nyuma. Ukweli ni kama mwiba unaochoma unyayo. Ukweli ni kama gharika linaloangamiza kila kitu. Vyote hivi vinafanyika bila kusita, kuwa na shaka au woga.

Ukweli ni tabia nzuri na pendwa inayozungumzwa vinywani mwa watu, lakini ni tabia ngumu kutekelezeka kwa sababu inajengwa na hila, shaka na pinduapindua katika usemi na utendaji. Je, ni viongozi wangapi hawamo ndani ya dimba hili?

Wajibu ni dhima. Kiongozi analazimika kutimiza jambo fulani ambalo kwake ni chachu na kwa watu ni hamira inayoumua mambo na kupata mafanikio. Wajibu ni jukumu ambalo kiongozi yeyote hana budi kulitimiza, kwa sababu amelitaka kwa hiari yake.

Kiongozi mkweli hana tabia ya kusitasita katika kuwajibika kwa sababu kauli yake njema ni mvuto kwa watu na matendo yake mema ni masharti mbele ya jamii. Ni viongozi wangapi hapa nchini mwetu Wanatambua na wanathamini wajibu wao? Ni wajibu kiongozi kusema ukweli na kuwajibika katika majukumu yake.

Neno mzalendo na uzalendo limetopea mno hivi sasa katika vinywa vya viongozi wanapokuwa katika harakati zao za kisiasa. Wanatamka kwa uwanda mpana kushawishi na kuhamasisha watu maana ya uzalendo na kujiaminisha kuwa wao ni wazalendo. Hili si jambo baya, ni jambo zuri.

Uzalendo ni uraia. Kiongozi mzalendo awe raia asili wa nchi. Uzalendo ni utaifa. Kiongozi huyu hana budi kuwa na mapenzi ya nchi yake katika kujiunganisha na watu kuwa taifa moja. Uzalendo ni uananchi. Kiongozi huyu awe mwenyeji wa kuzaliwa au wa kuandikishwa. Kiongozi mzalendo ni mtu anayeipenda nchi yake na yupo tayari kuifia.

Kiongozi ni mwenye sifa ya ukweli, wajibu na uzalendo; huwa na ziada ya uadilifu, ustaarabu na uungwana katika kauli na matendo yake anapojipanga kuwatumikia wananchi wenzake. Kiongozi mzalendo hutoa uamuzi wa dhati na wenye msimamo imara.

Unapokuwa katika aina ya uongozi huu, ni tabu kuyumbishwa, ni shida kugwaya na ni ghali kuchezewa na watu, maadui au viongozi uchwara. Kiongozi wa aina hii ukweli anapata misukosuko kutoka kwa vibaraka, wasaliti, wahaini na mafisadi.  Lakini Mwenyezi Mungu huwa pamoja naye na hatimaye hushinda mapambano.

Ni jambo jema kwa viongozi wa aina yoyote, hasa wa siasa kujenga na kudumisha ustaarabu wa kukosoa na kukosolewa katika nia zao, matendo yao na kauli zao, kuthibitisha uzalendo wao. Uzalendo una rutuba na mboji na hutoa mavuno bora. Viongozi muwe na ukweli, wajibu na uzalendo.