Na Bwanku M Bwanku
Nchi yetu kwa sasa inaendelea na michakato mbalimbali kuelekea kwenye tukio kubwa na muhimu la uchaguzi wa Serikali za Mitaa unaotarajiwa kufanyika Novemba 27, mwaka huu, takribani wiki ikiwa imebaki.
Tayari michakato mingi kuelekea tukio hili muhimu imefanyika na inaendelea kufanyika ikiwemo kutangaza vijiji, mitaa na vitongoji, wananchi kujiandikisha kwenye Daftari la Mkazi la Wapiga kura litakalotumika kupiga kura, michakato ya kupata wagombea ndani ya Vyama vya siasa ambao ndio wadau na washiriki wakubwa kuleta wagombea, wiki hii ya kampeni n.k.
Kampeni kwa ajili ya uchaguzi zimeanza Novemba 20 na zitakoma Novemba 26, 2024 kabla ya tarehe husika ya uchaguzi Novemba 27. Kipindi hiki cha kampeni wananchi watapata fursa ya kusikia sera mbalimbali za wagombea wa Vyama mbalimbali kabla ya kufanya uamuzi wao wa kuchagua kiongozi wanayemtaka.
Kimahesabu, uchaguzi huu wa Serikali za Mitaa ndio uchaguzi muhimu zaidi kwenye Taifa letu kwasababu unaleta viongozi ambao ndiyo msingi wa kwanza na mkubwa wa maendeleo kuanzia ngazi za chini za uongozi.
Tunafahamu Watanzania wote wako kwenye vijiji, mitaa na vitongoji na huku ndiko msingi wa kwanza wa maendeleo unaanzia ikiwemo wananchi kutambuliwa kero zao, mahitaji yao na mapendekezo yao kuhusu maendeleo na maisha yao.
Viongozi wanaochaguliwa na kupatikana kwenye uchaguzi huu ndio wanaoishi moja kwa moja na wananchi kwenye maeneo yao na wanakutana nao kila saa na wananchi na wao wanatambua kwa undani mahitaji ya wananchi kabla ya kupelekwa kwa ngazi za juu kufanyiwa kazi.
Ni ngumu kwa Mbunge au Diwani au Kiongozi yeyote wa ngazi ya juu mathalani Waziri kukutana na wananchi mara kwa mara lakini huyu Mwenyekiti wa Kijiji, wa Mtaa, wa Kitongoji na wale Wajumbe wa Serikali hizi wanaopatikana kupitia Uchaguzi huu wa Serikali za Mitaa wako na wananchi muda wote kule chini.
Hii pekee yake inadhihirisha umuhimu na unyeti wa uchaguzi huu. Huu ni uchaguzi unaoleta viongozi wanaoweka misingi kwenye Dira ya Maendeleo ya Taifa kwa kubainisha moja kwa moja mahitaji ya wananchi kabla ya Serikali Kuu kuchukua mahitaji hayo na kuyafanyia kazi.
Kwa minajiri hiyo, Uchaguzi wa Serikali za Mitaa sio wa kuuchukulia poa hata kidogo bali wananchi wanapaswa kushiriki kikamilifu kuchagua viongozi imara ambao wataunganisha kero, mahitaji na matamanio yao kwenda kwa watunga sera na watekelezaji kwa ajili ya kusukuma maendeleo kwa haraka.
Rais ambaye ndiye Msimamizi Mkuu wa shughuli za maendeleo kwenye Taifa, Bunge ambalo ndilo chombo kikuu cha kutunga sheria, sera na kuisimamia serikali katika kuleta maendeleo, hivi vyote kama taasisi haviwezi kujua matatizo ya kila mwananchi nchi nzima, matatizo ya kila kijiji, mtaa au kitongoji lakini kupitia viongozi hawa wanaopatikana kupitia uchaguzi huu wanaweza kwa urahisi kuunganisha na kufikisha masuala yote ya wananchi kwa utekelezaji.
Lakini pia mipango ya Taifa kama Mpango wa Maendeleo ya Taifa, Dira ya Maendeleo ya Taifa, utungaji wa sera na sheria vinavyosimamia maendeleo ya Taifa, hivi vyote msingi wake ni kupitia njia ya msingi kule chini kuweza kung’amua maoni na matarajio ya wananchi kwa ajili ya kuwekewa mikakati ya utatuzi na utekelezaji.
Kwahiyo, hakuna maendeleo bila ngazi hii ya chini kabisa ya uongozi ambao unapatikana kupitia uchaguzi wa Serikali za Mitaa.
Wananchi tutumie fursa hii adimu kushiriki kikamilifu kwenye michakato hii michache iliyobaki kuelekea uchaguzi ikiwemo kusikiliza sera za kila mgombea kwa kuhudhuria mikutano ya kampeni, kuepuka wagombea watoa rushwa, kulinda amani na utulivu kipindi chote cha kampeni na uchaguzi ili kuweza kupata kiongozi makini wa kushirikiana nae kwenye shughuli za maendeleo yetu kwenye maeneo yetu.