Viongozi wa ulimwengu, makasisi na umati wa watu mapema hii leo walikusanyika kwenye Uwanja wa Mtakatifu Petro mjini Vatican kwa ajili ya mazishi ya Kiongozi wa Kanisa Katoli ulimwenguni Papa Francis.
Kadinali wa Italia Giovanni Battista Re aliongoza Ibada ya Misa Takatifu baada ya jeneza la Papa Francis kufikishwa kanisani na kuwekwa mbele ya madhabahu.
Re amemuelezea Papa Francis kama “papa wa watu, mwenye moyo safi” na aliyependa kushirikiana na jamii iliyotengwa, kuwasiliana moja kwa moja na watu binafsi, aliyekuwa na shauku ya kuwa karibu na kila mtu, na hasa waliokuwa na shida.
Rais Donald Trump wa Marekani ni miongoni mwa wakuu waliohudhuria mazishi hayo, pamoja na Rais Volodymyr Zelensky wa Ukraine na Emmanuel Macron wa Ufaransa, zaidi ya makadinali 200 na makasisi wapatao 4,000.
