Kiongozi bora hafinyangwi wala hachongwi, bali huzaliwa na karama ya uongozi. Kiongozi bora ni mtumishi wa umma anayeongoza watu kwa hekima na busara. Mtawala ni mheshimiwa kwa watawaliwa. Wapo baadhi ya wanadamu miongoni mwetu ambao kwa mapenzi ya Mwenyezi Mungu wamezaliwa na karama ya uongozi. Waziri Mkuu Kassim Majaliwa anayo karama na kipaji cha uongozi bora itokayo kwa Mungu mwenyewe.

Baada ya hadhari nyingi za wahifadhi, hatimaye Waziri Mkuu Majaliwa alifanya ziara ya kikazi mkoani Arusha, mwaka jana na kutembelea Wilaya ya Ngorongoro, tarafa za Ngorongoro na Loliondo pekee bila kutembelea Tarafa ya Sale yenye migogoro mingi ya ardhi ya kabla na baada ya Uhuru wa Tanganyika, hasa Kijiji cha Kisangiro, Kata ya Kirangi na kutoa maagizo ya kutekelezwa na viongozi wa Serikali. Akataka wadau wanaohusika na migogoro ya ardhi Loliondo kuitafutia suluhu ya kudumu. 

Wananchi tulikuwa na matumaini makubwa na Waziri Mkuu kuwa atatoa ‘uamuzi mgumu’ uliomshinda mtangulizi wake kwa kumaliza kabisa migogoro ya ardhi na kulinda maslahi mapana ya nchi, kutetea uhifadhi, kutetea rasilimali za Taifa wanazofaidi wawekezaji matapeli wakishirikiana na NGOs badala ya Serikali kwa niaba ya wananchi. 

Badala yake akatoa maagizo kwa CAG kufanya ukaguzi wa matumizi ya fedha zao huku ikijulikana wazi jinsi wanavyofuja fedha hizo kwa manufaa yao binafsi kinyume cha katiba zao. Tunaamini Waziri Mkuu, ama alipotoshwa na viongozi wa wilaya na mkoa, au anawavutia pumzi.

Pamoja na vitisho mbalimbali ili tarafa za Loliondo na Sale zitulie, hakuna budi wajitokeze watu wa kuthubutu kueleza ukweli bila woga kuwasaidia viongozi wakuu wa Serikali kutambua kinachoendelea Ngorongoro ili kuleta suluhu ya kudumu, vinginevyo migogoro hii haitakoma. 

Kabla ya ziara ya Waziri Mkuu wilayani Ngorongoro, alitanguliwa na ziara ya Mkuu wa Mkoa wa Arusha, Mrisho Gambo, ambaye alitembelea tarafa zote na kwa hakika wananchi wanakiri kuwa alikula na kulala nao vijijini kwa bahati mbaya naye hakupangiwa kutembelea kijiji nilichokitaja hapo juu.

Ziara hiyo ya RC ilikuwa na ajenda za chakula cha njaa Tarafa ya Ngorongoro, Mamlaka ya Hifadhi ya Ngorongoro (NCAA), Baraza la Wafugaji, ugonjwa wa ajabu katika Kata ya Pinyinyi, kukosekana kwa mitandao ya simu kwa baadhi ya maeneo ya Tarafa ya Sale, matumizi mabaya ya fedha za umma na kukamilisha ahadi ya madawati.

Pamoja na ajenda hizo za RC, kwa kutokujua alisahau ajenda muhimu kuwa  Wilaya ya Ngorongoro kuna uharibifu mkubwa wa mazingira katika Pori Tengefu, NCAA na Hifadhi ya Taifa Serengeti (SENAPA), utitiri wa NGOs, migogoro ya ardhi iliyokithiri hasa tarafa za Sale na Loliondo, mifugo kutoka Kenya, wahamiaji walowezi kutoka Kenya, ubovu wa barabara, huduma duni za afya, elimu na utoro shuleni, maji safi na salama, migogoro ya wawekezaji wa sekta ya utalii, utata wa mpaka wa Senapa na Wilaya ya Ngorongoro, utata wa mipaka ya  vijiji na rasilimali za asili za Wilaya ya Ngorongoro kuwa ni mgodi wa watu wachache wanaojaribu kuzifanya mali zao binafsi na yeyote anayejitokeza kuhoji huitwa mchochezi na mara moja hukamatwa. 

Bila kupiga chuku wala uzushi ni kweli kuwa kwa sasa kuna kila dalili kuwa NGOs zilizotapakaa eneo dogo la Loliondo zimekata pumzi baada ya kushikwa pabaya na Serikali ya Awamu ya Tano na pengine malengo ya kumaliza migogoro ya ardhi yaliyowekwa na Serikali yatatimia kwa wakati kama RC Gambo alivyotuambia kuwa kipaumbele chake namba moja 2017 ni kutokomeza migogoro yote ya ardhi mkoani kwake.

Mwalimu Julius Nyerere aliwahi kusema; huwezi kusuluhisha ugomvi wa watu wawili huku mgomvi mmoja unamsaidia, unampa silaha na askari halafu unatoka kule na kwenda kwa mgomvi wa pili na kuzungumzia suluhu. Viongozi wa kiroho kutoka Kenya wana maslahi na NGOs, nao eti ni wasuluhishi wa migogoro ya ardhi Loliondo. Tunaomba RC Gambo ajitokeze hadharani na kueleza umma uswahiba wake na NGOs za Loliondo hasa AndBeyond na anayegharimia msafara wa safari zake kutoka Arusha  hadi Loliondo, kwani kuna baadhi ya watumishi wa umma ambao wameamua kuungana na wawekezaji na NGOs kuipinga Serikali yetu na maslahi mapana ya Taifa. 

Ukiona giza linazidi ujue nuru ipo karibu na neno la Mungu kupitia Nabii Isaya linasema upitapo katika maji mengi nitakuwa pamoja nawe na katika mito, haitakugharikisha uendapo katika moto hautakuteketeza wala mwali wa moto hautakuunguza. 

Pamoja na Waziri Mkuu kuwa na nia nzuri na uwezo wa kujenga hoja akiamini kwamba hoja pekee zitavunja nguvu za NGOs za Loliondo, kumbe ni kinyume chake ndiyo kwanza anawapa nafasi na mbinu za kujipanga upya na kuipinga Serikali.

Hawezi amini watu wakubwa wenye nyadhifa zao Wilaya ya Ngorongoro, ngazi ya Mkoa wa Arusha na ndani ya Chama Cha Mapinduzi waliokabidhiwa mamlaka ya kulinda na kusimamia rasilimali za umma, ndiyo wapiga dili na si watu wadogo wa mitaani wala watu wasiokuwa na nyadhifa. 

Baba wa Taifa aliwahi kusema juu ya usafi wa maadili kwa kutumia kisa cha mke wa mfalme kuwa kosa la mke wa mfalme si kutenda uovu, bali kushukiwa kutenda uovu. Mke wa Kaisari hapaswi kutuhumiwa kwa uchafu achilia mbali kuutenda. Mkuu wa Mkoa wa Arusha na Mkuu wa Wilaya ya Ngorongoro wanatuhumiwa kumshauri vibaya Waziri Mkuu kwa kuwapendelea wawekezaji, NGOs na wahamiaji haramu kutoka Kenya huku wakiendelea kukalia viti kuwaongoza wananchi wakati wanatuhumiwa kutokuwa wasafi. Tunawashauri wachague wa kuwatumikia kati ya wananchi, wawekezaji, NGOs na wahamiaji haramu. 

Waziri Mkuu atambue kwamba migogoro ya ardhi Wilaya ya Ngorongoro, hasa tarafa za Loliondo na Sale ni ya kupangwa na chanzo chake ni utajiri mkubwa wa rasilimali za wanyamapori, ukosefu wa maadili kwa viongozi, ukosefu wa uzalendo na kutokuwajibika ipasavyo kwa viongozi. Ni kiongozi gani aliyewajibishwa kwa makosa aliyoyatenda Loliondo? Wananchi tulikuwa na shauku, faraja na matarajio makubwa kwa mtendaji mkuu wa Serikali kutembelea Loliondo, lakini matarajio yetu yameyeyuka kwa kushindwa angalau kuzifuta asasi za kiraia ambazo zinaendesha shughuli zao Loliondo bila kusajiliwa nchini.

Kwa kuwa hoja ni nyingi, lengo la makala hii ni kumpongeza Waziri Mkuu kwa kuthubutu kutembelea Wilaya ya Ngorongoro na kujionea mwenyewe maajabu mengi ya Loliondo, ingawa alifichwa kwa kutopelekwa sehemu zilizoharibiwa. 

Asiyeona ukali wa ncha ya mkuki anayojichongea mwenyewe ataiona kesho itakapoelekezwa katika kifua chake. Wazo la maridhiano shirikishi ni mhimu sana, lakini unaridhiana na nani? Na wahamiaji haramu kutoka Kenya? Au viongozi wa NGOs ambao wengi wao ni wanasiasa (wabunge, madiwani, wenyeviti wa vijiji, vitongoji, malaigwanan, wafanyakazi wa halimashauri ambao wana mtandao mkubwa hadi kwenye vyombo vya ulinzi na usalama?) Unaridhiana na hao kwa kushauriwa na NGOs ambazo kwa sasa ndiyo washauri wakuu wa mkuu wa mkoa na wilaya katika kumaliza migogoro ya ardhi Wilaya ya Ngorongoro? Au unaridhiana na NGOs zenye vinasaba na Kenya zinazowatetea wawekezaji wa kigeni na maslahi ya nchi jirani? 

Tumesahau, asilimia 99 ya viongozi wa kuchaguliwa Wilaya ya Ngorongoro ni zao la hizi NGOs? Au tunaridhiana na taasisi za dini ambazo Wilaya ya Ngorongoro nyingi zimetoka Kenya tena bila kusajiliwa kutoa huduma Tanzania? Au tunaridhiana na kampuni za uwekezaji zilizoingia mikataba na baadhi ya vijiji ambazo hazilipi kodi za Serikali (labda kipekee OBC Limited ambayo usajili na uwekezaji wake unajulikana)? Ifahamike NGOs siyo wahifadhi wala wadau muhimu kwa uhifadhi. Kuwashirikisha kutafuta suluhu ya migogoro ya ardhi Loliondo na kuwaacha wananchi ni kupoteza muda na rasilimali maana malengo yao ni fedha na suluhu ikipatikana watakosa fedha. 

Wakikosa mapato wamekosa maisha. NGOs hizi viongozi wake ni raia wa Kenya, hivyo si rahisi wakubali uamuzi wenye manufaa na wananchi na uhifadhi kwa ujumla. Hivyo, hizi ni kikwazo katika kumalizika kwa migogoro ya ardhi tarafa za Loliondo na Sale. 

Tanzania ni nchi moja na Loliondo siyo jamhuri, hivyo ni lazima iongozwe na sheria za Tanzania na asiyetaka kutii hili arudi kwao Kenya. Sitaki kuamini kuwa Wilaya ya Ngorongoro mkoani Arusha ni kama nchi inayojitegemea ndani ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, lakini kiuhalisia ndivyo inavyoonekana na rais wake ni NGOs zinazoendesha siasa za kilaghai wilayani humu.

Kitu pekee NGOs za Loliondo kinachowashinda ni nafasi za uteuzi tu na nguvu pekee wanayotumia kwa nafasi hizi ni ushawishi wa fedha, lakini nafasi zote za uchaguzi na watendaji wao ndiyo wenye mamlaka na uamuzi wa mwisho. Mtumishi yeyote anayefuata sheria na kusimamia haki NGOs huamini ni mpinzani wao na mara moja hutafutiwa visa ili aondolewe au ahamishwe. Hivyo, NGOs hizi zina utawala wao. Kwa muktadha huu, bila kuchukua hatua madhubuti tarafa za Loliondo na Sale abadani hazitakuwa na amani ya kudumu. 

Pili, wananchi wanajiuliza inakuwaje ndani ya nchi moja yenye mikoa, wilaya na tarafa zenye rasilimali za Taifa hasa jamii za kifugaji mapato yote huingia mfuko mkuu wa Hazina (consolidated fund), lakini tarafa pekee ya Ngorongoro pamoja na kuwa na miradi ya ujirani mwema na NCAA hupewa chakula cha msaada na Sh bilioni mbili kila mwaka kupitia baraza lao la wafugaji?

Hii siyo ‘double standard/allocation’ huku wananchi hao wakiwa na shughuli zao za kuendesha maisha yao ya kila siku sawa na Watanzania wengine? Kwanini tarafa nyingine za Loliondo na Sale hazipati misaada ya fedha na chakula kama Tarafa ya Ngorongoro? Kwanini misaada hiyo yote isipitie Halmashauri ambako kata zote bajeti zao za maendeleo hupangwa na kupitishwa na Baraza la Madiwani?

 

MGOGORO WA ARDHI KIJIJI CHA KISANGIRO KATA YA KIRANGI WILAYA NGORONGORO

Mgogoro huu ulisuluhishwa na Waziri wa Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi Februari 23, 2013 lakini umerudi upya na karibu kila mwaka mgogoro huu hugharimu maisha ya raia wasiokuwa na hatia. Maeneo mengine yaliyosuluhishwa ni kati ya Kijiji cha Maloni na Yasi Mdito eneo la Kibala, Olerian na Magaiduru eneo la Kisiyansui, Kijiji cha Sale na Arash eneo la Oljori; na Kisangiro-Kata ya Kirangi na Kijiji cha Enguserosambu, Kata ya Olgosorok eneo la Naan/Horane.

Maeneo yote mipaka yake imeheshimiwa hadi leo isipokuwa mpaka wa Kijiji cha Kisangiro ambako mgogoro umeanza upya kwa msaada wa diwani ambaye badala ya kuwa mtetezi wa wananchi wake amekuwa mfanyakazi wa NGOs na amefanya mapinduzi haramu ya kuuondoa uongozi wa Serikali ya Kijiji cha Kisangiro kinyume cha sheria na kuunda ‘serikali yake’ ndani ya Serikali halali ya Kijiji kwa maelekezo ya NGOs na katibu wa CCM Wilaya ili kumwondoa madarakani Mwenyekiti wa Serikali ya Kijiji cha Kisangiro.

Mwenyekiti huyu anaoneka kuwa ni kikwazo cha wahamiaji haramu kutoka Kenya kupora ardhi ya Kijiji hicho kinyume cha sheria. Pia ana wajumbe wake haramu anaowaalika kuhudhuria vikao vya Kamati ya Maendeleo ya Kata badala ya wenyeviti halali wa vijiji waliochaguliwa na wananchi. Kwa msaada wa diwani huyo, wahamiaji jamii ya Loita kutoka Kenya wamepora mashamba ya wananchi na kuweka utawala wao ndani ya ardhi yetu katika kijiji haramu cha Naan ndani ya Kijiji cha Kisangiro kinyume cha sheria. Uliona wapi kijiji kimoja kinakuwa ndani ya nchi, tarafa na kata mbili tofauti?

Viongozi wa Serikali wamekosa uadilifu na uungwana. Wameamua kuwalinda wahamiaji hivyo kusababisha uhasama mkubwa na hatimaye mapigano hutokea na kusababisha vifo kwa raia. Watendaji wa Halmashauri na baadhi ya madiwani hushirikiana na maafisa ardhi kupora ardhi za vijiji baada ya kupewa rushwa.

Wapo viongozi na watendaji wa serikali ya wilaya ya Ngorongoro wanaohongwa rushwa za fedha, mifugo, kulimiwa mashamba ya maharage katika ardhi ya Kijiji cha Kisangiro, na mifugo yao kuchungwa kwa nguvu kwenye ardhi ya kijiji kwa msaada wa diwani. Wananchi wake wanasema walichagua diwani wa CCM kwa sababu ya ahadi zake kwa wananchi na uzuri wa ilani ya uchaguzi ya CCM 2015-2020 lakini baada tu ya kuchaguliwa amesigina ahadi zake zote na kuwageuka wananchi. Amekuwa chanzo cha migogoro ya Kijiji cha Kisangiro hivyo kurudisha nyuma maendeleo.

Pamoja na diwani huyu kuhatarisha amani ya kijiji na taarifa zake kutolewa ngazi ya wilaya na kwa Katibu wa CCM Wilaya hadi sasa hakuna hatua zozote zilizochukuliwa.

 

UMUHIMU WA PORI TENGEFU LOLIONDO 

Ukweli na uongo havikai pamoja kama ilivyo nuru na giza na sifa kuu ya ukweli daima hujitenga na uongo mithili ya maji na mafuta. Mafisadi na NGOs wamedanganya vya kutosha sasa Serikali imeanza kuona nuru ya ukweli iliyoongopwa kwa miaka 25 na baadhi ya viongozi na NGOs wilayani Ngorongoro waliodiriki kusema Serikali haina eneo ndani ya Pori Tengefu Loliondo.

Wanadai kisheria eneo hilo ni ardhi halali inayomilikiwa na wananchi kwa mfumo wa vijiji vya Soit-sambu chenye hati ya usajili namba 7275 ya Oktoba 13,1990; Arash hati namba 7264 ya Oktoba 13, 1990, Ololosokwan chenye hati iliyotolewa Januari 25,1996, Piyaya, Engusoresambu, Oloirian/Magaiduru, Loosoito, na Oloipiril kwa mujibu wa Sheria ya Vijiji Namba 5 ya mwaka 1999. 

Kisheria eneo la Pori Tengefu Loliondo lenye kilometa za mraba 4,000 linamilikiwa kihalali na Wizara ya Maliasili na Utalii kwa mujibu wa Tangazo la Serikali Na. 269 la mwaka 1974 kwa lengo la kuhifadhi wa wanyamapori, vyanzo vya maji, mazalia ya wanyamapori na mapito yao [ushoroba] ili kuendelea na mzunguko wao wa Senapa-Ngorongoro-Maasai-Mara na sehemu nyingine. Na umuhimu huo bado upo na siyo kwa vijiji vilivyosajiliwa kiujanja ujanja miaka ya 1990. Huu ni uthibitisho mwingine kuwa Loliondo kuna jamhuri. Haiwezekani kabisa ndani ya eneo moja la ardhi kuwe na wamiliki wawili halali kisheria. Kampuni pekee inayoendesha shughuli zake kihalali ndani ya Pori Tengefu ni OBC Limited na kijiji pekee kilichopimwa na kusajiliwa kihalali wilayani Ngorongoro ni Kijiji cha Engaresero tu. Hivyo, kuna haja kwa Serikali kuvifuta vijiji vyote vilivyosajiliwa kihuni ndani ya Pori Tengefu na wawekezaji wote waliopitia Hifadhi za Jamii (WMA). 

Mkakati wa kugeuza Pori Tengefu kuwa WMA ni mpango hatari sana wenye lengo la kuifuta Senapa na NCAA kwenye ramani ya hifadhi maarufu duniani na kuinufaisha mbuga ya Maasai-Mara nchini Kenya. Mpango sahihi wa kitalaamu na uliofanyiwa utafiti na Taasisi ya Utafiti wa Wanyamapori Tanzania (TAWIRI) ni kutenga kilometa za mraba 1,500 kwa uhifadhi na nyingine 2,500 kwa matumizi ya wananchi. 

Kuanzishwa kwa WMA Loliondo ni kuendelea kuwanufaisha wawekezaji walioingia mikataba na vijiji bila kulipa tozo na kodi mbalimbali za serikali, NGOs, viongozi wa vijiji, na viongozi wa jadi (malaigwanan); na si wananchi maskini kama yalivyo madhumuni ya kuanzishwa kwa WMA. 

Wananchi tunajiuliza, LGCA kuna kampuni nyingi za Kizungu zinazojishughulisha na uwindaji na utalii wa picha, ni kwa nini viongozi wa NGOs wanaiandama sana OBC kuwa haitakiwi na wananchi wakati ndiyo kampuni pekee inayolipa kodi za halmashauri, Serikali na kushiriki kikamilifu kwenye miradi ya maendeleo ya wananchi?

Kama yalivyo mapori mengine nchini ni vizuri wanasiasa nao wakajua kitaalamu umuhimu wa uhifadhi na uwepo wa Pori Tengefu Loliondo kuwa ni uwanda wenye umuhimu wa pekee kwa uhai wa Senapa, NCAA na Maasai-Mara. Nia ya watetezi wa uhifadhi ni kulinda mazingira (ecosystem), vyanzo vya maji kwa matumizi ya wanyama na binadamu, mazalia ya wanyamapori na viumbe wengine adimu (biodiversity/endemic/endangered spp) ili waendelee kuwapo na hatimaye kuwavutia watalii wa ndani na nje kutembelea mbuga zetu ili kuongeza mapato ya serikali na kutoa huduma kwa wananchi.

Ifahamike kuwa bila uhifadhi hakuna hifadhi za Taifa wala WMA, hivyo mamilioni ya shilingi wanazopata wawekezaji wa utalii, NGOs na vijiji kupitia WMA chanzo chake ni uhifadhi na ndiyo maana kampuni nyingi za kitalii na NGOs wamejazana Loliondo; na si sehemu nyingine nchini kwa kuwa wana uhakika ni eneo tulivu na watalii watakuja kuangalia vivutio vya wanyamapori na kuingiza mapato makubwa. Watalii hawaji kuangalia mifugo. Kwa mfano, mwaka 2015 sekta ndogo ya utalii pekee ilikuwa sekta kiongozi kwa kuliingizia Taifa fedha nyingi za kigeni takribani dola milioni 2 (17.5%). Sekta hii ilizipiku sekta za kilimo; na hata mifugo ambayo ndiyo inayoiua sasa Loliondo.

 

HITIMISHO

Ukitaka kujua ni wapi palipo na tai wengi angalia palipo na mizoga. Wahusika wote wanaochochea migogoro ya ardhi hasa tarafa za Loliondo na Sale wachunguzwe na kuchukuliwa hatua za kisheria bila kujali hadhi zao kisiasa, ukwasi wao kimaisha na katika jamii kwa kuwa ni rahisi kuwajua wanufaika na makuwadi wa migogoro ya ardhi.

Wana ukwasi usioweza kutolewa maelezo sahihi ya upatikanaji wake. Wengi wao wamejificha kwenye shughuli halali kama siasa, dini, biashara, NGOs na wengine ni watumishi wa Halmashauri ya Wilaya ya Ngorongoro na serikalini. 

Ili kumaliza migogoro ya ardhi tarafa za Sale na Loliondo, kunahitajika utashi wa kisiasa na tunaiomba Serikali kushughulikia mgogoro huu kwa haraka ili ufikie tamati kwa faida na maendeleo ya uhifadhi na wananchi.

Kunahitajika mpango bora wa matumizi endelevu ya ardhi ambao ni pamoja na kuvifuta vijiji vyote vilivyoanzishwa na kusajiliwa kinyume cha utaratibu pamoja na kufufua mpango uliokataliwa na NGOs wa Balozi Khamis Kagasheki wa kutenga eneo la uhifadhi, malisho ya mifugo, makazi ya binadamu na kilimo.

Ardhi za vijiji wilayani Ngorongoro zipimwe na kuwekwa mipaka halali, mipaka iwekwe ‘beacon’ na kupewa hati miliki ili viweze kupanga mipango endelevu ya matumizi bora ya ardhi ya vijiji vyao.

CAG aendelee kukangua, kuchunguza na atuambie kila kampuni ya uwekezaji wa utalii kupitia mikataba ya WMA ndani ya Pori Tengefu zinalipa tozo na kodi za Serikali kihalali?

Hivyo, Waziri Mkuu tunakuomba urudi Loliondo na upige marufuku shughuli zote za kibinadamu ndani ya Pori Tengefu kwa manufaa ya kizazi cha sasa na kijacho; uhifadhi na kufuta mikataba yote iliyoingiwa kati ya vijiji na baadhi ya wawekezaji kupitia hifadhi za jamii kwani Pori Tengefu lipo mpakani na kuna uwezekano mkubwa wa watalii kuingizwa na kutoka nchini bila kulipa tozo na kodi za Serikali.

Pia agiza, kusimamiwa, kutekelezwa na kuheshimiwa kwa mipaka ya vijiji wilayani Ngorongoro iliyowekwa na Waziri wa Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi mwaka 2013 hasa Kijiji cha Kisangiro kinachopakana kaskazini na Kenya.

Hakika, waharibifu wa mazingira Pori Tengefu, wachochezi wa migogoro ya ardhi tarafa za Sale na Loliondo, viongozi wa NGOs, kampuni za kitalii, wahamiaji haramu kutoka Kenya kwa pamoja wanaisoma namba ya ziara ya Waziri Mkuu Majaliwa wilayani Ngorongoro. Waziri Mkuu hongera na aluta continua.

Mwisho, tunawaomba mawaziri wengine hasa wa Mambo ya Ndani ya Nchi, Ofisi ya Rais-T awala za Mikoa na Serikali za Mitaa; wizara za Ujenzi, Afya, Elimu na nyingine nao waige mfano wa uchapaji kazi wa Waziri Mkuu na Waziri wa Maliasili na Utalii kwa kutembelea Ngorongoro na kutatua kero zinazowakabili wananchi kwa miaka mingi.

 

Wako,

Wakereketwa wa uhifadhi na mazingira endelevu

Ngorongoro