Viongozi wa nchi mbalimbali duniani wamelaani shambulio la risasi lililomjeruhi sikioni aliyekuwa rais wa Marekani Donald Trump

Msemaji wa Katibu mkuu wa Umoja wa Mataifa Antonio Guterres amelaani na kuliita tukio hilo kuwa ni vurugu za kisiasa. Kwa upande wake Kansela wa Ujerumani Olaf Scholz amekitaja kitendo hicho kuwa cha chuki, wakati Rais wa Ufaransa Emmanuel Macron akimtakia Trump nafuu ya haraka.

Naye Waziri Mkuu wa Uingereza Keir Starmer amesema amefedheheshwa na kushtushwa na kilichotokea na ametuma salamu za pole kwa walioathiriwa katika tukio hilo.

Miongoni mwa viongozi wengine waliolaani tukio hilo na kutoa pole kwa Trump ni pamoja na Rais wa halmashauri kuu ya Umoja wa Ulaya Ursula von der Leyen, Katibu Mkuu wa Jumuiya ya kujihami ya NATO Jens Stoltenberg, Waziri Mkuu wa Canada Justin Trudeau, Fumio Kishida wa Japan, Narendra Modi wa India na Rais wa Ukraine Volodymyr Zelensky.