Viongozi 19 wa dini mbalimbali hapa nchini kutoka mikoa ya Lindi na Mtwara, wiki iliyopita wamerejea nchini kutoka katika ziara ya mafunzo nchini Thailand huku wakiwa wamefurahishwa na mafunzo waliyopata.

Mafunzo hayo yalitokana na jitihada za Serikali katika kuhakikisha elimu kuhusu masuala ya gesi asilia na mafuta inatolewa kwa wananchi wa kada mbalimbali, ili kufahamu mchakato mzima wa upatikanaji wa gesi asilia na mafuta.

Pia mafunzo hayo yalilenga kujua faida za gesi katika nyanja za kiuchumi na kijamii, changamoto zake na namna nchi nyingine zinavyotumia rasilimali hiyo katika kukuza uchumi.

Iwapo viongozi hao wataitumia elimu hiyo kwa kuwaelimisha wananchi kuhusu sekta ya gesi asilia nchini, watawajengea uelewa wa pamoja utakaowafanya wananchi kushiriki na kuwa na mtazamo chanya kuhusu miradi mbalimbali ya gesi asilia nchini.

Wakizungumza kwa nyakati tofauti  baada ya kutua katika Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Julius Nyerere (JNIA), Sheikh Mkuu wa Mtwara, Nurdin Mangochi, amesema iwapo Watanzania watatumia vizuri muda, watu na ardhi, kuna uwezekano mkubwa wa kupiga hatua katika maendeleo.

“Nimejifunza mambo mengi kutoka Thailand; nimefahamu kuwa kama wananchi wa Thailand hawataki utani; wanatumia vizuri muda na ardhi ndiyo maana wamepata maendeleo; kumbe hata sisi tukitumia vizuri muda na ardhi kamwe hatutabaki nyuma kimaendeleo. Wenzetu wanatumia muda vizuri, wanatumia ardhi vizuri, wako mbali kimaendeleo,” amesema.

Kiongozi mwingine ni Mhadhiri Mwandamizi wa Chuo Kikuu cha Mtakatifu Agustino Tawi la Mtwara, Padri Dkt. Aidan Msafiri, amesema kwamba mafunzo waliyopata katika ziara hiyo ilikuwa ni yenye manufaa makubwa kwake na kwa Taifa.

“Tumejifunza mengi hata mfumo wa kusafirisha gesi, nimebaini kuwa ili kusafirisha gesi ni lazima utumie bomba kama tulivyofanya sisi ndiyo gesi  ifike eneo husika,” amesema.

Amesema kwamba Thailand imepiga hatua kubwa baada ya kugundua gesi  miaka 30 iliyopita, kiasi cha kusambaza umeme kwa asilimia 99.8 kwa watu wake wanaotumia umeme.

Mjumbe wa Halmashauri Kuu ya Baraza Kuu la Waislamu  Tanzania (BAKWATA), Mohamed Sinani, amesema Thailand imepiga hatua kubwa katika maendeleo kutokana na sekta ya gesi.

Amesema wananchi wa nchi hiyo ni hodari kwa kufanya kazi na kupanga mipango ya kazi kwa kila siku na hawapotezi muda.

Wameimarisha miundombinu kama ya reli barabara na bahari.

Naye Katibu wa BAKWATA Mkoa wa Lindi, Alhaj Abdillah Salum, amesema kwamba wakati umefika wa kunufaika na rasilimali hizo, hivyo aliwataka wanajamii kujikita katika suala la elimu ili vijana wanufaike na ajira za gesi na mafuta.

Makamu wa Askofu Mkuu wa Kanisa la Anglikana Tanzania kutoka Dayosisi ya Newala, Oscar Mnung’u, amesema pamoja na wananchi wa Thailand kugundua gesi lakini hawakubweteka bali walitafuta njia nyingine ya kuzalisha gesi.

Amesema kwamba kwanza walianza kuzalisha gesi kwa kutumia pumba za mpunga, lakini baada ya kubaini kuwa gesi hiyo ilikuwa na gharama kubwa walifanya utafiti na kugundua utumiaji wa kipande cha muhogo.

Kipande  cha muhogo kilizalisha  gesi ambayo inaweza kuzalisha umeme mtaa mzima. Wenzetu wamepiga hatua kubwa sana, mie nimefurahi. Inatakiwa tutembee tuone, amesema Askofu Mnung’u.

Amesema kwamba wananchi wa Thailand hawataki kusikia migogoro baada ya kubaini kuwa haileti maendeleo kwa sababu  imesababisha uchumi wa nchi hiyo kushuka kutoka asilimia saba hadi moja.

“Watu wa Thailand ni wachapakazi, hawataki kusikia migogoro wanataka kazi. Nimetembea kila mahali wanatumia gesi kwa ajili ya umeme na kila mahali kuna sehemu ya kufanya masaji (massage).

“Na si kama za kwetu, hizi zimejaa ujinga na upuuzi mwingi, wale wanajua kazi yao hawafanyi ujinga hata kidogo bwana. Watalii wanajaa kwa ajili ya hilo, wanaingiza pesa mno,” amesema Askofu Mnung’u.

Mkuu wa Wilaya ya Kilwa, Abdallah Ulega, aliishukuru Serikali kwa kuona umuhimu wa kushirikisha viongozi wa dini katika masuala mbalimbali ya kitaifa.

Amesema kuwa viongozi wa dini wamehudhuria mafunzo hayo kwa umakini mkubwa na baada ya kupata uelewa mpana kuhusu gesi asilia na mafuta kutoka nchi nyingine:

“Sasa tutakuwa mabalozi katika kutoa elimu kwa waumini na wananchi kwa ujumla ili kujenga uelewa wa pamoja kuhusu sekta hiyo nchini.

“Pamoja na kujifunza masuala ya gesi asilia na mafuta nchini Thailand, tumepata fursa ya kutembelea eneo maalum la viwanda ambalo ukuaji wake umetokana na kuwapo kwa gesi asilia.

“Shirika la umma linalojishughulisha na masuala ya gesi na mafuta, mamlaka ya uzalishaji umeme, mamlaka ya usambazaji umeme, mtambo wa kuzalisha umeme unaotokana na tungamotaka (biomass), mtambo wa umeme wa jua, na mtambo wa umeme wa bayogesi,” amesema Ulega.

Amesema kwamba kupitia sekta ya gesi, Thailand  imeweka miundombinu mizuri ya gesi, imetengeneza barabara zaidi ya mia moja.

Amesema hayo yote yametokana na kujishusha na kuwa na moyo wa kujifunza, hivyo walikwenda pia nchini Ufilipino na kupata ujuzi kuhusu sekta ya gesi. Amewataka Watanzania kuwa tayari kujifunza ili waweze kumiliki sekta ya gesi.

Amesema kwamba kupata maendeleo katika sekta ya gesi si lazima kuuza gesi, bali hata kwa kukamata fursa za kuanzisha biashara mbalimbali ambazo wazalishaji wa gesi watapata huduma kupitia biashara utakayoanzisha.

“Nilichojifunza kule Thailand ni kwamba si wote wanachimba gesi, bali kuna watu waliojenga mahoteli, watu wanalala, wako wenye nyumba za kupangisha pia kuna maduka. Mzunguko wa biashara ni mkubwa mno. Kuna mwenzagu hapa kazungumzia watu wanaofanya masaji (massage) kwa watalii. Hii inatokana na sekta ya gesi kwa kuwa wanapata umeme, hivyo hata sisi tutafanya hivyo,” amesema.

Amesema Tanzania itafanikiwa kwa kasi kubwa baada ya kutumia muda mfupi katika matumizi ya gesi tangu ilipogunduliwa, kwani sasa kuna magari zaidi ya 50 yanatumia gesi, jambo ambalo ni tofauti na Thailand. Walitumia miaka 30 hadi kutumia gesi tangu ilipogunduliwa.

“Ndugu zangu sisi tutapiga hatua sana kwa kuwa kwa muda mfupi tumeweza kuitumia gesi kwa kipindi kifupi. Kama mnaweza kuona pale Ubungo kuna kituo cha kujaza gesi katika magari wakati Thailand ilichukua muda mrefu mno,” amesema Ulega.

 

Historia ya gesi asilia ya Thailand

Gesi asilia nchini Thailand iligunduliwa katika Ghuba ya Thailand katikati ya miaka ya 1970. Mwaka 1979 vitalu vikubwa viwili vya gesi viligunduliwa kilomita 425 kusini mwa nchi hiyo na kitalu kingine kiligunduliwa kilomita 170 kusini pia mwa nchi hiyo.

Katika kitalu cha kwanza, gesi asilia inakadiriwa kuwa ya futi za ujazo trilioni 1.6 na iliweza kuhifadhi futi za ujazo bilioni 220.

Katika kitalu cha pili kuligundulika gesi asilia zenye ujazo wa futi za ujazo trilioni 1.3 na inaweza kuhifadhi gesi zenye ujazo wa futi 4,500,000,000,000.

Vitalu vingine viwili vidogo venye uwezo wa kuzalisha gesi futi za ujazo bilioni 500 na kwa nchi nzima gesi inayohifadhiwa inakadiriwa kuwa futi za ujazo 8,500,000,000,000  kwa mwaka 1984.

Tangu Thailand ilipoanza kuzalisha gesi asilia mwaka 1987, ilikuwa na futi za ujazo 162,300,000,000.

Mwishoni mwa mwaka 1979, Benki ya Dunia iliipatia Thailand mkopo wa dola 107,000,000 za Marekani kupitia Mamlaka ya Petroli ya Thailand, ili  kusaidia katika awamu ya kwanza ya matumizi ya uvumbuzi huo.

Historia ya gesi Tanzania

Gesi asilia iligundulika mwaka 1974 katika Kisiwa cha Songo Songo mkoani Lindi. Baada ya hapo ugunduzi mwingine uligundulika katika maeneo ya Mtwara Vijijini, (Mnazi Bay) mwaka 1982 na Ntorya (2012), Mkuranga (Pwani, 2007), Kiliwani (Lindi, 2008). Kiasi cha gesi asilia iliyogunduliwa katika maeneo haya inakadiriwa kuwa futi za ujazo trilioni 4.5  hadi  8.

Katika kipindi cha miaka mitatu iliyopita, kumekuwa na kasi kubwa ya utafutaji mafuta na gesi asilia uliojikita zaidi kwenye maji ya kina kirefu cha bahari. Kiasi cha gesi asilia iliyogundulika katika kina kirefu cha maji inafikia takribani futi za ujazo trilioni 27.

Kiasi cha wingi wa gesi asilia yote iliyogunduliwa nchi kavu na baharini inafikia takribani futi za ujazo trilioni 35.

Kutokana na sheria za nchi yetu zinazotumiwa kugawa mipaka ya mikoa iliyopo kando kando ya bahari (isivuke 12 nautical miles au 22.22 km kuingia baharini), gesi asilia iliyogunduliwa hadi sasa katika Mkoa wa Mtwara pekee ni asilimia 14 tu ya gesi yote iliyogundulika nchini.

Kwa kutumia kigezo hicho cha sheria za mipaka ya kiutawala, gesi iligundulika katika Mkoa  wa Lindi ikiwa ni asilimia 7 ya gesi yote, Pwani asilimia moja na huku katika kina kirefu cha bahari (deep sea) ndicho chenye gesi nyingi ambacho ni asilimia 78  kuliko mikoa yote ikiwekwa pamoja.

Gesi asilia imegunduliwa kwenye miamba tabaka (sedimentary rocks) yenye umri wa miaka kati ya milioni 199.6 milioni hadi 23.03. Mipaka ya Bara la Afrika, ya nchi yetu na ile ya mikoa yetu haikuwapo wakati huo!

Utafutaji wa mafuta na gesi asilia pia unaendelea tukiwa na matarajio makubwa ya upatikanaji wa rasilimali hizi katika mikoa ya Arusha, Kilimanjaro, Tanga, Manyara, Kigoma, Mbeya, Njombe, Rukwa, Katavi, Morogoro na Tabora pamoja na kwenye kina kirefu cha maji baharini kuanzia mpaka wetu na Msumbiji hadi mpaka wetu na Kenya.

 

Matumizi ya gesi asilia ya Mnazi Bay (Mtwara) na Songo Songo (Lindi)

Mpaka hivi sasa gesi asilia inayozalishwa na kutumika nchini ni kutoka Mnazi Bay (Mtwara Vijijini) na Songo Songo (Kilwa, Lindi). Gesi ya Mnazi Bay kwa sasa huzalisha umeme kwa ajili ya mikoa ya Mtwara na Lindi.

Mitambo ya kufua umeme kutokana na gesi asilia iliyopo Mtwara Mjini ina uwezo wa kuzalisha MW 18 lakini matumizi ya umeme ya mikoa ya Mtwara na Lindi haijavuka MW 12.

Umeme huo wa Mtwara unafuliwa na TANESCO huku Kampuni za Wentworth na Maurel & Prom zikizalisha gesi asilia (inayotumiwa na TANESCO) kiasi cha futi za ujazo milioni 2 kwa siku.

Uchorongaji wa kisima kimoja cha utafutaji wa gesi asilia nchi kavu unahitaji dola milioni 40 za Marekani, na kwenye kina kirefu cha maji baharini zinahitajika zaidi ya dola milioni 400 za Marekani.

Serikali kwa kushirikiana na Shirika la Maendeleo ya Petroli Tanzania (TPDC) inatumia fedha kwa shughuli za kuvutia, kuratibu na kusimamia utafutaji na uendelezaji wa gesi asilia nchini kote ikiwamo mikoa ya Mtwara na Lindi.

Gesi asilia iliyopo Mnazi Bay (Mtwara Vijijini) inazalisha umeme peke yake kwa ajili ya mikoa ya Mtwara na Lindi. Gesi asilia ya Songo Songo (Kilwa, Lindi) ndiyo inayotumika kuzalisha umeme kwa ajili ya gridi ya taifa, na pia kwa ajili ya wananchi wa Kisiwa cha Songo Songo (Lindi), maeneo ya Somanga Fungu (Lindi) na viwandani (Dar es Salaam).

Tangu Oktoba 2004 wakati mitambo ya kufua umeme ilipoanza kazi hadi leo hii, kiasi cha gesi asilia ya Songo Songo kilichotumika ni asilimia 7 ya gesi asilia yote iliyogunduliwa huko. Kwa hiyo, takwimu zinaonesha kuwa hata uchumi wa Jiji la Dar es Salaam unatumia kiasi kidogo sana cha gesi asilia asilimia 7 iliyopo Songo Songo (Kilwa, Lindi).

Ujenzi wa bomba la gesi asilia hadi Dar es Salaam

Mauzo ya gesi asilia jijini Dar es Salaam ambako ni kitovu cha uchumi wa Tanzania, asilimia 80 kwa mapato ya nchi yetu yanazalishwa Dar es Salaam, ni uamuzi mzuri wa kiuchumi.

Tayari kuna viwanda 34 vinavyotumia gesi asilia ambavyo vinahitaji kupanua shughuli zao endapo gesi zaidi itapatikana. Soko kubwa la gesi asilia lipo tayari Dar es Salaam. Ipo mitambo ya kufua umeme kwa kutumia mafuta.

Serikali inatumia fedha nyingi za kigeni kununulia mafuta ya kufua umeme tunaoutumia kila siku. Takribani dola bilioni  moja za Marekani (sawa na Sh trilioni 1.6) kwa mwaka zitaokolewa kutokana na mitambo iliyopo nchini ikifua umeme kwa kutumia gesi asilia na kuachana na mafuta ambayo ni ya bei kubwa.

Bei kwa uniti moja (KWh) ya umeme unaofuliwa kutumia dizeli na mafuta ya aina nyingine ni kati ya senti 30 za Marekani hadi senti 45 huku bei ya uniti moja hiyo hiyo ni senti za 6-8 za Marekani kwa umeme utokanao na gesi asilia na zinapungua na wakati wa matumizi.

Vilevile, takribani dola milioni 202 za Marekani kwa mwaka zitaokolewa iwapo Jiji la Dar es Salaam litatumia gesi asilia badala ya mafuta katika magari, taasisi na majumbani. Fedha hizo zikiokolewa zitatoa mchango mkubwa kwenye uchumi wa Taifa kwa manufaa ya Watanzania wote.

Umeme mwingi zaidi kutokana na gesi asilia

Bomba la gesi asilia linalojengwa litasafirisha gesi nyingi zaidi ambayo itawezesha mitambo mipya itakayojengwa Kinyerezi (Dar es Salaam) kufua umeme wa zaidi ya MW 990. Umeme mwingine utafuliwa Somanga Fungu (Lindi) wa kiasi kisichopungua MW 520 kitapatikana.

 

Usafirishaji na usambazaji wa umeme

Dar es Salaam ndiko kuliko na miundombinu mikubwa ya usafirishaji na usambazaji wa umeme kuliko mikoa mingine yote, hivyo ni uamuzi wa kiuchumi unaolazimisha kusafirisha gesi asilia kutoka mikoa ya Lindi na Mtwara na kuipeleka Dar es Salaam ambako itatumika kufua umeme, na kutumika moja kwa moja viwandani, majumbani na kwenye magari.

Kwa kuzingatia mahitaji ya gesi asilia yatakayojitokeza, bomba la kusafirisha gesi litawekewa matoleo ya kuchukulia gesi (tie-off) katika maeneo ya Mtwara, Lindi, Kilwa na Mkuranga ili kuhakikisha kuwa miji hii inakuwa na gesi asilia ya uhakika wakati wowote itakapohitajika.

Kwa hiyo, kuweka mitandao ya usambazaji wa gesi kutoka kwenye bomba la gesi asilia linalojengwa kutarahisisha matumizi ya gesi asilia viwandani na majumbani katika mikoa ya Mtwara na Lindi, na kwenye mikoa mingine kwa siku za baadaye.

Serikali imetenga maeneo katika pwani ya mikoa ya Kusini (Lindi na Mtwara) kwa ajili ya uanzishwaji wa maeneo ya viwanda (industrial parks/estates) vikiwamo viwanda vya mbolea, liquefied natural gas (LNG) na petrochemicals. Ujenzi wa kiwanja cha simenti uko katika hatua za mwisho za maandalizi.

Ili kutengeneza mazingira mazuri ya biashara ya gesi asilia na mafuta kwa kampuni za huduma, malighafi na vitendea kazi, Serikali imetenga eneo maalum Mtwara, ambalo litawekewa miundombinu ya msingi ili kutoa vivutio mbalimbali kwa kampuni hizo. Eneo hilo litapewa hadhi ya Ukanda Huru wa Bandari (Freeport Zone).

Shughuli za kusafisha na kusafirisha gesi asilia zitatoa ajira katika maeneo husika. Kwa mfano, kwa mitambo ya kusafishia gesi inayojengwa Madimba (Mtwara Vijijini) na Songo Songo (Kilwa, Lindi), kila mtambo utahitaji wafanyakazi na wengine watatoka mikoa ya Lindi na Mtwara.