Mamlaka ya kimaadili ni ile hali ya mtu kuwa na tabia njema inayoifanya jamii kumheshimu, kumuamini na hata kuyapa thamani maneno na ushauri wake na kufanywa kuwa chanzo cha mwongozo au mfano wa mwenendo sahihi kwa wanajamii. Huyu ni mtu ambaye anamiliki sifa ya kuwa na maarifa na uadilifu usiotiliwa shaka, inayopambwa na ukweli na uaminifu. Mamlaka ya kimaadili ndiyo iliyoifanya jamii ya Kiquraishi katika mji wa Makkah kumheshimu Mtume Muhammad (Allaah Amrehemu na Ampe Amani), kumthamini na kumtangaza kwa kumwita Mkweli Muaminifu. Tabia zake njema na uadilifu ulimjengea mamlaka ya kimaadili kabla hata ya kutangazwa utume wake.
Binadamu amejaaliwa aina mbili za lugha; lugha ya kauli na lugha ya vitendo. Wanazuoni wa Kiislamu wana msemo mashuhuri kuwa: “Lugha ya vitendo ni fasaha zaidi kuliko lugha ya kauli.
Binadamu muadilifu ni yule ambaye kauli zake njema zinaungwa mkono na vitendo vyake. Yule ambaye asemayo si atendayo, mbali ya jamii kumdharau, kumpuuza na kutomtia maanani, anafanya chukizo kubwa mbele ya Mwenyeezi Mungu kwa kusema yale asiyoyatenda kama tunavyosoma katika Qur’aan Tukufu, Sura ya 61 (Surat As-Saff) Aya ya 2 na 3 kuwa:
“Enyi mlioamini! Kwanini mnasema msiyoyatenda? Yanachukiza vikubwa mno kwa Mwenyeezi Mungu kuwa mnasema msiyoyatenda.”
Ni dhahiri kuwa kiongozi na hususan kiongozi wa dini atakayekuwa anasema yale asiyoyatenda atakuwa amekosa mamlaka ya kimaadili ya kuaminika katika jamii na kauli zake zitakosa nguvu na baraka za Mwenyeezi Mungu.
Kwamba kiongozi wa dini kwa maneno yake anahimiza umoja, mshikamano na utangamano baina ya jamii ya Kitanzania kwa kutanguliza na kuipa umuhimu familia kuu ya ubinadamu lakini kwa matendo yake baada ya kuvaa joho la kisiasa au kunasa katika mitego ya wanasiasa anaigawa jamii kwa misingi ya dini, ukanda, ukabila au ukereketwa na ufurukutwa wa vyama vya siasa, ni dhahiri kiongozi huyo yupo katika hatari ya kupoteza mamlaka ya kimaadili.
Mamlaka ya kimaadili pia inadhihiri kwa mtu ambaye anaamrisha mema ambayo yeye mwenyewe ni mwenye kuyatenda na anakataza mabaya ambayo yeye pia amekatazika nayo.
Kwa kiongozi na hususan kiongozi wa dini kuyashika haya ndiko kutampa mamlaka ya kimaadili katika jamii anayoiongoza na kumpa heshima kwa jamii pana anayoishi nayo. Kinyume chake ataingia katika kundi la watu waliotajwa katika Qur’aan Tukufu, Sura ya 2 (Surat Al-Baqarah) Aya ya 44 kuwa:
“Je, mnawaamrisha watu mema na mnajisahau nafsi zenu, na hali nyinyi mnasoma Kitabu? Basi je, hamzingatii?”
Utangulizi huu umekusudia kutandika jamvi ili kuwakumbusha viongozi wa dini nafasi kubwa waliyonayo katika jamii na nguvu yao ya kuiongoza jamii kwenye heri na mafanikio au kuitumbukiza katika shari na maangamizi.
Viongozi wa dini ndio kimbilio la wanyonge na wale waliokata tamaa ili wawape faraja na kwa kutekeleza jukumu lao la kukataza maovu watumie njia za siri na dhahiri na kunyanyua sauti zao kupinga maovu na dhuluma katika jamii.
Yaani, viongozi wa dini wanapaswa kutumia hekima na kauli njema wakati wa kutekeleza jukumu lao hili muhimu. Kiongozi kutumia njia za dhahiri na siri katika kufikisha nasaha, kuamrisha mema na kukataza mabaya ni mbinu alizotumia Mtume Nuhu kama tunavyosoma katika Qur’aan Tukufu Sura ya 71 (Surat Nuh’) Aya 8 na 9 kuwa:
“Tena niliwaita kwa uwazi. Kisha nikawatangazia kwa kelele, tena nikasema nao kwa siri.”
Viongozi wenye mamlaka ya kimaadili ni wale wenye uwezo wa kuamrisha mema na kukataza mabaya bila ya kujali hali, shakhsiya na hadhi ya yule anayeamrishwa au anayekatazwa kwani huyo ni sehemu ya waumini wenye kuhitaji tiba ya kiroho katika kuimarisha imani yao na kujenga nguvu ya kujilinda na shetani na kupambana na nafsi mbaya inayoamrisha maovu.
Viongozi wa dini wanapokosa mamlaka ya kimaadili hushindwa kukataza maovu katika jamii jambo ambalo husababisha mmomonyoko wa maadili katika jamii, kushamiri uovu na ufisadi na jamii husika kuharibikiwa.
Tunasoma katika Qur’aan Tukufu, Sura ya 5 (Surat Al-Maaidah) Aya ya 78 na 79 kuwa:
“Walilaaniwa waliokufuru miongoni mwa Wana wa Israili kwa ulimi wa Daud na wa Isa Mwana wa Maryam. Hayo ni kwa sababu waliasi na wakawa wanapindukia mipaka. Walikuwa hawakatazani maovu waliyokuwa wakiyafanya. Hakika ni maovu yalioje mambo waliyokuwa wakiyafanya!”
Viongozi wa dini nchini Tanzania wana wajibu mkubwa wa kujijengea mamlaka ya kimaadili ili watekeleze jukumu lao kubwa la kuiongoza jamii kiimani na kuinusuru na maangamizi yatokanayo na maovu mbalimbali, kuporomoka kwa utu na maadili miongoni mwa wanajamii, uroho wa madaraka na majanga mengineyo yatokanayo na minyukano ya nguvu za kisiasa, kiuchumi na kijamii.
Hili la ujenzi wa mamlaka ya kimaadili miongoni mwa viongozi wa dini ni lazima lizingatie hali halisi ya nchi yetu kisheria, kisiasa, kiuchumi na kiutamaduni.
Kwa mfano, pale wanasiasa wanapozusha chuki na uadui baina yao na kuambukiza chuki na uadui huo kwa wafuasi wao, viongozi wa dini wanapaswa kusimama kati na kwa uadilifu mkubwa kuwakumbusha kuwa mfumo wa vyama vingi vya siasa nchini Tanzania upo kwa mujibu wa sheria na kwamba si uzalendo wala uasi kuwa mwanachama wa chama chochote cha siasa kwani ni jambo la hiari.
Viongozi wa dini wanaomiliki mamlaka ya kimaadili ndio watakaoaminika kuleta suluhu baina ya wanasiasa wanaogombana katika vyama vyao na pia kuwa mpatanishi bora baina ya serikali na vyama vya siasa katika yale yanayogusa masilahi ya taifa au kuhatarisha usalama, amani na utulivu nchini.
Swali la kujiuliza: Je, viongozi wa dini ambao pia ni wanasiasa wanaweza kuaminika kuifanya kazi hii tukufu kwa wakati mmoja, wakati wao ni wahusika wa majukwaa mawili: Jukwaa la Dini na Jukwaa la Siasa?
Vipi kiongozi wa dini-mwanasiasa ataweza kutumia miongozo miwili, wa kidini na kisiasa, inayopingana (katika baadhi ya mambo/nadharia) na jamii ikamuamini kuwa anamiliki mamlaka ya kimaadili?
Kwa mfano, wakati kwa wanasiasa wakiongozwa na falsafa ya Niccolo Machiavelli wanaamini kufikia malengo yao kwa njia yoyote iwayo nzuri au mbaya (The ends justify the means), Mwenyeezi Mungu anatutaka kufikia malengo mema kwa kutumia njia njema. Kiongozi wa dini-mwanasiasa atatumia muongozo gani katika ya miongozo hii miwili inayokinzana?
Ni vipi katika nchi ya kisekula kama hii inayopaswa kufuata msingi mkuu wa kutenganisha dini na siasa inafumbia macho hali hii ya viongozi wa dini kutiwa katika makapu ya wanasiasa na kuyatamani madaraka ya kisiasa kuliko madaraka ya kiroho?
Nani atawajibika kwa hasara itakayopatikana pale wanasiasa wanakapoifanya jamii igawanyike kidini kutokana na mvuto wa viongozi wa dini-wanasiasa wanaotumia vipawa vya kiroho na mvuto wa kiimani kwa malengo ya kisiasa?
Upi uadilifu wa kiongozi wa dini anayetumia jukwaa la kidini kwa masilahi ya chama anachokishabikia au kilichomtia mfukoni wakati anajua kwamba kuwa mwanachama wa chama chochote cha siasa nchini Tanzania ni jambo la hiari na ni uhuru unaolindwa kisheria na kwamba waumini anaowaongoza wanaweza kuwa wafuasi wa vyama mbalimbali vya siasa vilivyosajiliwa na Msajili wa Vyama vya Siasa kwa mujibu wa sheria?
Kwa nini pale kiongozi wa dini anapoamua kuwa mwanasiasa asiachane na mimbari za misikiti na altare/madhabahu ya makanisa?
Je, tunaruhusu sasa dini kutumika kufikia malengo ya kisiasa (kusiasaisha dini) na siasa kutumika kufikia malengo ya kidini (kudinisha siasa)?
Kiongozi wa dini aliyeamua kuwa mkereketwa au mfurukutwa wa chama kimoja cha siasa na hata kufikia kuwa kiongozi kamili wa kisiasa walhali waumini anaowaongoza ni wafuasi wa vyama mbalimbali vya siasa nchini, haoni kuwa anapanda sumu mbaya ya kuwafarakanisha waumini wake?
Kwa masilahi ya taifa na mustakabali mwema wa nchi yetu Tanzania ambayo ni faradhi kwetu kuipenda na kuilinda, na huo ndio uzalendo wa kweli, hatuna budi kutafuta majibu ya maswali haya na tubaini tulipopotea njia na tukumbushane kuwa nchi salama ni ile yenye misingi imara ya kimaadili na ugavi salama wa nguvu-mvuto na nguvu-kinzani zilizo ndani ya jamii.
Pamoja na uhalisia kuwa viongozi wa dini hawawezi kujitenga na wanajamii wakiwamo wanasiasa, ukweli utabakia kuwa nafasi yao nyeti inapaswa kulindwa na kuheshimiwa kwa kutokubali kutiwa katika makapu ya wanasiasa kwa masilahi ya kidunia wakaacha jukumu kubwa walilonalo la kuilea jamii kiimani.
Viongozi wa dini wanapaswa kuzingatia umuhimu wa kuimarisha mamlaka yao ya kimaadili na kuhakikisha yanakuwa ni pambo lao na wanatumia mamlaka ya kimaadili katika kuamrisha mema na kukataza maovu katika jamii bila ya kuzingatia yamefanywa na nani miongoni mwa wanajamii.
Viongozi wa dini kukubali kunyang’anywa mamlaka ya kimaadili kwa kuendekeza masilahi ya kidunia na kufikia kujisahau na kutojali madhara ya uamuzi wao huo kwa jamii na mustakbali wa nchi ni jambo linalofanana na kuhifadhi madumu ya petroli katika nyumba yenye joto kali – mlipuko ni jambo la kutarajiwa.
Shime viongozi wa dini tuzingatie umuhimu wa kujijengea mamlaka ya kimaadili ili tuweze kuiponya jamii na shari za wanasiasa ambao historia imewashuhudia kuwa kwao vyanzo vya matatizo, machafuko na uharibifu sehemu mbalimbali duniani.
Tukutane Jumanne ijayo, In-Shaa-Allaah!
Sheikh Khamis Mataka ni Mwenyekiti wa Halmashauri Kuu ya Baraza Kuu la Waislamu wa Tanzania (Bakwata) na Katibu Mkuu wa Taasisi ya Masheikh na Wanazuoni wa Kiislamu Tanzania. Simu: 0713603050/0754603050.