Na Mwandishi Wetu, JamhuriMedia, Kagera

Viongozi wa dini mkoani Kagera wamewaasa wananchi kutambua kuwa mafanikio ya kweli hayawezi kupatikana kupitia ushirikina au vitendo vya kikatili, kama kukata viungo vya watu wenye ulemavu wa ngozi. Katika maombi maalum yaliyofanyika Uwanja wa Kaitaba, Bukoba, viongozi hao walisisitiza umuhimu wa uadilifu, mshikamano, na kumtanguliza Mungu katika kila juhudi za maendeleo.

Makamu Askofu wa Kanisa Katoliki Bukoba, Padre Samueli Muchunguzi, alisisitiza kuwa mafanikio yanapatikana tu kwa juhudi halali na baraka za Mungu. Aliwataka wananchi kuachana na fitina na chuki ambazo zimekuwa kikwazo kwa maendeleo ya kijamii na kiuchumi.

Shekhe Abdushahidu Abbas wa Answar Sunna ameeleza kuwa utajiri na nafasi za uongozi zinapatikana kwa bidii, maombi, na ushirikiano wa pamoja, si kwa njia za kishirikina, Nae Shekhe wa Mkoa wa Kagera Haruna Kichwabuta, ameombea upendo, uvumilivu, na mshikamano wa kitaifa.

Aidha Mkuu wa Mkoa wa Kagera, Hajat Fatma Mwassa, ameeleza kuwa tukio hilo lilikuwa sehemu ya kufungua Tamasha la Ijuka Omuka 2024, lenye lengo la kuhamasisha fursa mbalimbali za maendeleo mkoani humo. 

Tamasha hilo litazinduliwa rasmi na Naibu Waziri Mkuu, Doto Biteko, Desemba 19 na kuhitimishwa Desemba 26.

Madhehebu mbalimbali, yakiwemo Tec, Cct, Shia, Bakwata, na Umoja wa Makanisa ya Kipentekoste, yaliungana kwa maombi hayo ya kuombea amani na maendeleo ya taifa.