Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kupitia Mtandao Huru wa Wabunge wa Kupambana na Kifua Kikuu Tanzania, mwishoni mwa wiki iliyopita limesaini makubaliano na taasisi za dini kushiriki mapambano ya ugonjwa wa Kifua Kikuu (TB) unaoua zaidi ya watu 60 kila siku nchini.

Taasisi zilizosaini makubaliano hayo ni Baraza la Maaskofu Katoliki (TEC), Jumuiya ya Kikatoliki Tanzania (CCT), Baraza la Waislamu Tanzania (BAKWATA), Baraza la Maaskofu wa Makanisa ya Kipentekoste Tanzania (CPCT) na Kanisa la Waadiventisti Wasabato Tanzania (SDA).

Katika makubaliano hayo, viongozi wa dini wamekubali kutumia mtandao wao wa nyumba za ibada, jumuiya ndogo ndogo, makambi na hospitali za taasisi hizo kupambana na ugonjwa wa TB ambao ni hatari. 

Meneja wa Mpango wa Taifa wa Kudhibiti Kifua Kikuu na Ukoma Tanzania, Dk. Beatrice Mutayoba, amewaambia washiriki wa mkutano wa kutia saini makubaliano hayo kuwa kwa mwaka 2018 walikufa wagonjwa wa TB 39,000 nchini.

Dk. Mutayoba amesema kati ya vifo hivyo 39,000 kuna vifo 16,000 vilivyotokana na magonjwa mchanganyiko kwa maana ya ukimwi na TB. Ameongeza kuwa katika kipindi cha miaka 200 iliyopita, TB imeua watu bilioni moja duniani.

Kutokana na ukubwa wa tatizo hili, mwaka 1993 Shirika la Afya Duniani liliitangaza TB kuwa ni janga la kidunia. Mwaka 2005 Umoja wa Afrika nao ukaitangaza TB kama janga la Afrika, huku Tanzania ikikitangaza kifua kikuu kama janga la taifa mwaka 2006.

Mgonjwa ambaye hajaanza tiba, ana uwezo wa kuambukiza wagonjwa 20 kwa mwaka kwa njia ya hewa pale anapopiga chafya, kukohoa, kupumua au kupiga miayo. Dalili za ugonjwa huu ni pamoja na kukohoa mfululizo kwa wiki mbili, kupungua uzito, kutoka jasho jingi usiku, kupungua uzito na dalili nyingine za aina hiyo.

Hatari ya ugonjwa huu ni kwamba hadi sasa robo ya watu wote duniani wana vimelea vya TB, ingawa hawajashambuliwa na magonjwa nyemelezi, hivyo watu wanahitajika kupima afya zao mara kwa mara kubaini iwapo wana TB au la. Habari njema ni kuwa ukikutwa na TB ugonjwa huu unatibika.

Dk. Mutayoba ametaja makundi yaliyoko hatarini kupata TB kuwa ni watu wenye makazi duni, kwa maana nyumba hazina madirisha yanayopitisha hewa na mwanga wa kutosha, magereza (wafungwa), shule za bweni, kambi za wavuvi, machimboni, wanaojidunga, wenye VVU na kisukari.

Takwimu zinaonyesha kuwa mwaka 2028 TB iliua watu milioni 1.5, ambapo watu milioni 10 waliambukizwa TB na watu milioni 7 pekee ndio waliopata tiba, hivyo milioni 3, waliendelea kuishi uraiani na kuendelea kuambukiza watu wengine. Kinachoogopesha, ukimwi kwa mwaka jana uliua watu kati ya 900,000 na milioni 1.1, hivyo TB inaonyesha inaongoza kwa kuua watu duniani.

Tanzania ipo katika nchi 30 zenye maambukizi makubwa duniani, ambapo mwaka 2018 watu 142,000 waliugua TB, ila kati ya hao waliopata matibabu ni watu 75,000 pekee, sawa na asilimia 53. Wengine waliishia mitaani ama kufariki dunia au kuendelea kuambukiza ugonjwa watu wengine.

Dk. Germana Lyena kutoka Taasisi ya Lishe, akiwasilisha mada ya pili amesema kuna uhusiano mkubwa kati ya lishe bora na maambukizi ya TB. Amesema chakuna kinafanya kazi ya kuuimarisha mwili, kuujenga na kuukarabati, hivyo mwili wenye lishe bora si rahisi kuambukizwa TB, kwani kinga yake inakuwa iko juu.

Amesema kiwango cha udumavu nchini kutokana na lishe isiyo bora uko katika kiwango cha asilimia 31.7, unyonyeshaji wa maziwa ya mama pekee kwa kipindi cha miezi 6 kwa mtoto aliyezaliwa upo katika asilimia 57.8, ulaji unaostahili kwa watoto baada ya miezi 6 uko katika 30% na upungufu wa damu ni asilimia 28.8 nchini, hali inayoweka mazingira rafiki kwa watu kupata TB.

Dk. Lyena ameshauri watu kula vyakula vya aina mbalimbali kutoka katika makundi tofauti ya chakula, kuongeza ulaji wa mbogamboga za aina tofauti kila siku ili kuboresha kinga ya mwili, kuongeza ulaji wa matunda mbalimbali yanayopatikana kwenye mazingira tunayoishi ili kuboresha kinga ya mwili na kuongeza kula vyakula vyenye asili ya wanyama.

Vyakula hivyo ni pamoja na nyama, samaki, mayai, maziwa na dagaa kila inapowezekana ili kuboresha kinga ya mwili. Pia ameshauri watu kuongeza ulaji wa vyakula jamii ya kunde kama vile maharage, choroko, njegere, kunde, dengu, mbaazi, njugu mawe na karanga.

Amewaasa wananchi kupunguza ulaji wa vyakula venye mafuta mengi au sukari nyingi, kuacha au kupunguza unywaji wa pombe za aina mbalimbali na kuacha matumizi ya sigara na bidhaa zitokanazo na tumbaku.

Wakati huo huo, amewataka wananchi kuishi kwenye nyumba au chumba chenye madirisha kuanzia mawili yanayoruhusu mzunguko mkubwa wa hewa, kuepuka kuishi kwenye chumba chenye dirisha moja, kuepuka kulala watu wengi katika chumba kimoja, kuhakikisha kumbi za mikutano, makanisa, misikiti, mabweni ya wanafunzi zinakuwa na mfumo mzuri wa hewa. Pia kuhakikisha kuna umbali wa kutosha kati ya nyumba na nyumba, hivi vyote vikilenga mtu apate hewa ya kutosha.

Viongozi wa dini waliotia saini wamekubali kutoa elimu kwa waumini wao kuboresha makazi yao, kuimarisha lishe, kusambaza habari za TB kupitia nyumba za ibada, vyombo vyao vya habari na wakaitaka serikali kuhakikisha inatoa dawa na vifaa tiba vya kutosha kwa hospitali za dini ili kuwezesha matibabu na ikiwezekana Tanzania ifute ugonjwa wa TB ndani ya muda mfupi. 

Kwa mwenendo wa sasa, wataalamu wamesema Tanzania itaweza kufuta ugonjwa wa TB miaka 200 ijayo, yaani mwaka 2221, hivyo zinahitajika juhudi kubwa.

Kwa hali ilivyo, watu wenye makazi yenye msongamano kama maeneo ya Tandale, Manzese, Kwa Mtogole na kwingine, wanashauriwa majirani kukubaliana kuvunja kuta na kutoa fursa ya hewa safi kuzunguka eneo lao, hali itakayookoa maisha ya watu wasiambukizwe TB.

Waziri Mkuu (mstaafu), Mizengo Pinda, ambaye kwa sasa ni Mwenyekiti wa Taasisi ya Lishe ya Agri Thamani, amelipongeza Bunge kufikia makubaliano na viongozi wa dini na akatoa mifano miwili juu ya ufanisi wa viongozi wa dini katika kumaliza mambo magumu.

“Hili si jambo jepesi sana. Ni kazi kubwa sana. Nakumbuka tulikuwa na la mauaji ya albino. Nilikuja hapa Mwanza tukakaa na kuzungumza na viongozi wa dini… leo ukiniuliza kilitokea nini, nitasema sijui, lakini mauaji hayapo. Viongozi wa dini tuliwapa kazi ya kusaidia jambo hili liishe. Kulitokea jingine, la nani achinje na nani asichinje, nikaona uwaziri mkuu mgumu kweli. Niliwaita viongozi wa madhehebu ya dini wote, tukaitisha viongozi wa madhehebu ya dini, jambo hili lilikwisha… Viongozi wa madhehebu ya dini wana mambo mawili; moja ni ukaribu wao na Mungu, hivyo wakiomba Mungu anawasikiliza, tofauti na sisi tunaosemasema uongo. La pili ni ukaribu wao na jamii. Wana sifa ya ziada, wanasikilizwa na jamii. Wakisema sote tunasema amesema, litakwenda vizuri. Kwa hiyo Kanda ya Ziwa inaweza kuwa ni mahala pazuri pa kupigana vita hii,” amesema Pinda.

Ameongeza kuwa Mwalimu Nyerere alisema maadui watatu wa Tanzania ni, umaskini, ujinga na maradhi. “Hali ya umaskini wa nchi yetu bado haujatoka mahala hapo, walau kufikia 2025 wastani wa pato la kila Mtanzania iwe ni dola 3,000. Ukiondoa umaskini watu wataishi katika nyumba bora. Mikoa kama Dar es Salaam mnayodhani imeendelea, kwenye TB ndiyo inayoongoza. Wako maskini wa kutupa ndani ya Jiji la Dar es Salaam. Mwananyamala, Tandika, Temeke, wanaishi maisha ya dhiki mno… Ujinga nao una sehemu kubwa. Wee njoo Rukwa uone kama nitakusikiliza. Kila ukija ninakwenda kwa mganga wa kienyeji. Tatizo ni ujinga,” amesisitiza.

Mwenyekiti wa taasisi hiyo ya wabunge, Oscar Mukasa, amesema uamuzi uliofanywa na viongozi wa dini kupiga vita ugonjwa wa TB nchini unapaswa kuungwa mkono na kila mwananchi, na si kuachiwa Wizara ya Afya pekee, kwani una madhara makubwa kwa taifa. 

Spika wa Bunge, Job Ndugai, aliyekuwa mgeni rasmi, amewaomba viongozi wa dini kulipa kipaumbele suala la mapambano ya TB sawa na kazi ya kueneza injili wanayoifanya.

Viongozi wengine waliohudhuria ni pamoja na Waziri wa Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia na Watoto, Ummy Mwalimu; Naibu Waziri TAMISEMI, Josephat Kandege; Waziri wa Nchi Ofisi ya Waziri Mkuu, Jenista Muhagama na Mkuu wa Mkoa wa Mwanza, John Mongela.

Viongozi wa dini waliohudhuria ni Askofu Mark Warwa Malekana (SDA); Alinikisa Cheyo (CCT); Sheikh Hassan Said Chizenga (BAKWATA); Nuhu Jabir Muruma (Katibu Mkuu BAKWATA); Askofu Renatus Nkwande, Jacob Chimeleja, Moses Matonya, Pardon Kikiwa, Sadoc Butoke, Hezira Msanya, Padri Robert Shija (TEC) na viongozi wengine.