*Ni wanaotaka kugombea udiwani na ubunge katika maeneo mbalimbali
*Utitiri wa idadi ya wajumbe wapya wanaopiga kura za maoni yawatisha
*Watalazimika kuweka mawakala matawini watakaosimamia kura zao
*Mfumo mpya wa mchujo wa majina ya wagombea wageukamwiba kwao
Na Mwandishi Wetu, JamuriMedia, Dar es Salaam
Mabadiliko madogo ya Katiba ya Chama Cha Mapinduzi (CCM) ya mwaka 1977 yaliyofanyika mwezi uliopita jijini Dodoma yanatajwa ni maumivu kwa wanachama wake wanaotarajia kutia nia ya kugombea nafasi za ubunge na udiwani katika maeneo mbalimbali.
Licha ya mabadiliko hayo kutangazwa katika Mkutano Mkuu Maalumu wa CCM uliofanyika kuanzia Januari 18 hadi 19, mwaka huu chini ya Mwenyekiti wake Taifa, Rais Samia Suluhu Hassan, kutarajiwa kuongeza wapiga kura, kupunguza gharama za uendeshaji wa chama hicho na kudhibiti upangaji wa safu na wajumbe kwa mtu mmoja kujikusanyia kura nyingi lakini yameanza kulalamikiwa na baadhi ya watia nia.
Akitangaza mabadiliko hayo, Katibu wa Idara ya Oganaizesheni ya CCM Taifa, Issa Haji Gavu, amesema yanahusu Ibara ya 47(1), 60(1) na 73(1) ya Katiba ya chama hicho huku Kamati Kuu yake itakuwa na wajumbe 10 wanaochaguliwa kutoka Bara na Zanzibar huku kila upande wakiwa ni watano.

Kwa upande wa wajumbe wa shina CCM, amesema sasa itakuwa na kiongozi wa nyumba zisizozidi 20 zenye wanachama wasiopungua 50 na wasiozidi 80 kwa mijini, huku wanachama 30 na wasiozidi 80 kwa vijijini kutoka 10 waliokuwapo awali.
Katika hatua nyingine, mabadiliko hayo yanajumuisha nafasi za ujumbe wa Kamati Kuu na ongezeko la idadi ya wajumbe watakaoshiriki kupiga kura za maoni kwa madiwani na wabunge.
Kupitia mabadiliko hayo, wajumbe watakaopiga kura za maoni ndani ya chama hicho kwa nafasi za ubunge na udiwani ni mabalozi na wajumbe wanne wa mashina, kamati za siasa matawi, kamati za utekelezaji za Jumuiya ya Wanawake wa CCM (UWT) matawi na kamati za utekelezaji jumuiya ya wazazi matawi yote.
Wengine ni wajumbe wa kamati za utekelezaji za Umoja wa Vijana wa CCM (UVCCM) matawi, mjumbe mmoja wa mkutano wa jimbo kutoka matawi, wenyeviti wa serikali za mitaa na vijiji, kamati za siasa za kata, kamati za utekelezaji za UWT za kata.
Pia wajumbe wa kamati za utekelezaji za wazazi kata zote, kamati za utekelezaji za UVCCM kata, wajumbe watano wa mkutano wa jimbo wa kata, kamati ya siasa wilaya na kamati ya utekelezaji UWT wilaya.
Vilevile wajumbe wa kamati ya utekelezaji wa jumuiya ya wazazi wilaya, kamati ya utekelezaji UVCCM wilaya, sekretariat ya wilaya, madiwani na wabunge wa viti maalumu.
Kutokana na mabadiliko hayo, baadhi ya watia nia wamezungumza na JAMHURI kwa nyakati tofauti (majina yao yanahifadhiwa) wameyalalamikia kwa sababu yamebadilisha upepo na mwenendo mzima wa upigaji kura za maoni tofauti na miaka ya nyuma.
Mtia nia mmoja ametolea mfano wa Jimbo la Busokelo lililopo Mbeya kwamba mabadiliko hayo yamezalisha idadi kubwa ya wapiga kura wanaofikia karibu 8,000.
Amesema huo ni mfano tu lakini karibu majimbo mengi huku Bara wastani wa idadi ya wanaopiga kura za maoni ni kati ya 7,000 hadi 8,000 huku akiwashauri watia nia wengine kupiga hesabu za kiufundi kwa kuwafikia zaidi wenyeviti wa mashina na wajumbe wao wanaofikia karibu 4,600.
“Kwa wastani wajumbe wapya waliongezeka wanafikia karibu elfu nne na kitu kwa majimbo mengi. Mwanzoni kulikuwa na wapiga kura kama elfu tatu. Huu mziki mzito na wengi watashindwa,” amesema.
Kuhusu mabadiliko ya mchakato wa upigaji kura, amesema kwa sasa wajumbe wanayapigia kura majina matatu baada ya kuchujwa na vikao vya juu tofauti na zamani waliwapigia kwanza kisha wanaenda kuchujwa.
“Iko hivi, zamani watu wengi walikuwa wanajaza fomu za kugombea nafasi mbalimbali kisha wajumbe wanawapigia kura halafu anapatikana mshindi namba moja hadi wa mwisho na baada ya hapo vikao vinakaa kuwajadili na kumpitisha mgombea mmoja,” amesema na kuongeza:
“Utaratibu mpya ni kwamba watu wanachukua fomu hata kama wako 100 kisha vikao vya kuwajadili vinafanyika na kurudsha majina matatu au vinginevyo kisha wajumbe ndiyo wanakuja kuwapigia kura watu hao.
“Mchakato huo unafanyika baada ya Halmashauri Kuu ya CCM Mkoa kurudisha majina hayo matatu kisha yanaenda kupigiwa kura. Kwa hiyo watia nia hawawezi kuwawezesha fedha wajumbe hadi wawe na uhakika kama majina yao yanarudi. Unatoeaje fedha kama huna uhakika jina lako litarudi?”
Akifafanua zaidi mchakato huo ulivyo, amesema tarehe ya kuchukua fomu na kurudisha itatangazwa kisha watia nia watafuata mchakato huo kama kawaida, vikao vitajadili majina katika ngazi ya wilaya kwa wanaogombea ubunge na watapendekeza kati ya majina manne hadi sita.
“Kisha watapeleka mkoa nako watajadili na kule juu kamati kuu wanapeleka majina matatu ambayo wanaume watakuwa labda wawili lakini mwanamke lazima awe mmoja kwa ajili ya kubalansi mambo ya jinsia.
“Katika udiwani nako utaratibu utakuwa huohuo yanarudishwa majina matatu au vinginevyo kutokana na mabadiliko hayo kisha hao ndio wanakwenda kupambana katika sanduku la kura,” amesema.
Akashauri kwamba kama wapiga kura wako 8,000, walau mtia nia mmoja anatakiwa apambane apate nusu ya kura zote huku wengine wakigawana nusu zilizobaki na hapo atajihakikishia ushindi.
“Kama mtia nia anataka kuwawezesha wajumbe wakupigie kura ina maana inabidi mfuko wako uwe na fedha nyingi na unaweza kujikuta mtu anatenga hadi Sh milioni 200 kuwawezesha wajumbe wote hao.
“Kwa sababu utawawezesha mara ya kwanza halafu kuna ile finishing ya kuamkia siku ya kupiga kura ambayo ni muhimu. Hiyo ni bajeti ya chini kabisa ya kuanzia na ukishinda chama kinamsaidia mgombea kiasi kidogo cha fedha kwa ajili ya kuandaa mikutano ya kampeni na fedha nyingine inabidi mgombea agharamie mwenyewe,” amesema.
Mwaka huu amesema uchaguzi wa ndani ya chama hicho ni mgumu kwa watia nia wote kutokana na mabadiliko hayo ya wajumbe wapya na wanatakiwa wapige hesabu zao kwa umakini mkubwa.
“Mzigo umekuwa mzito kwa wabunge wanaotetea nafasi zao na wale wapya. Unajua katika ilani ya CCM vitu vingi vimetekelezwa kwa hiyo wabunge wengi watahukumiwa kutokana na uhusiano wao na wapiga kura majimboni lakini si kwa sababu ya utekelezaji wa ilani kwa sababu vituo vya afya vimejengwa na hospitali zimejengwa.
“Mambo mengine chungu nzima yamefanyika, hivyo wananchi wameviona vimefanywa kwa hiyo changamoto iko katika uhusiano na watu watahukumiwa hapo kwamba ulikuwa huonekani na hausaidii wapiga kura wako ila sasa hivi unarudi unataka tena?” Anahoji.
Mgombea mwingine wa udiwani katika kata iliyopo Jimbo la Ubungo jijini Dar es Salaam, amesema awali wajumbe waliopiga kura za maoni walikuwa 272 ila sasa hivi wako 900.
Kwa ujumla amesema jimbo hilo lenye kata nane lilikuwa na wajumbe karibu 500 wanaopiga kura za maoni za mbunge ila sasa hivi wameongezeka na kufikia 7,000.
“Sijui kama kuna mtia nia wa ubunge anaweza kuwawezesha wapiga kura wote hao 7,000 kama anaweza ili wampigie kura,” amesema.
Kwa upande wake, Katibu Mwenezi wa CCM Kata ya Mikocheni, Suleiman Akida, amesema awali idadi ya wajumbe waliopiga kura za maoni kwa nafasi ya udiwani katika eneo hilo walikuwa 170 ila sasa hivi wameongezeka na wamefikia 640 huku kwa nafasi ya ubunge walikuwa karibu 600 na sasa wako 8,000.
“Wapiga kura walikuwa watano watano. Idadi kubwa ya wajumbe waliongezeka wako katika mashina na matawi. Katika shina wanatoka mtu mmoja mmoja. Sasa katika Jimbo la Kawe lina mabalozi wa mashina karibu 1000.
“Ukizidisha hesabu ya mabalozi hao mara tano unapata idadi kubwa. Katika kura za udiwani wapiga kura kutoka tawi walikuwa wanatoka 10 ila sasa wameongezeka kwa sababu kamati za utekelezaji unakuta kuna sehemu walikuwa tisa au 10 lakini zamani walikuwa hawapigi kura,” amesema.
Katika jumuiya za chama, amesema walikuwa anaingia katibu na mwenyekiti ila kwa sasa wanaingia watu 10 katika matawi.
“Mathalani Kata ya Wazo ina matawi 14, Kawe ina matawi 12, Kunduchi kuna matawi 12, Mikocheni kuna matawi sita lakini wapiga kura wako 670, je, kama ni hivyo Wazo watakuwa na wapiga kura wangapi? Bila shaka wako chungu nzima. Watia nia wanatakiwa waka chini waumize vichwa vyao kwa kupiga hesabu zao sawasawa.
“Hata mbunge tu anayetetea nafasi yake naye anachanganyikiwa kwa sababu kwa utaratibu huu mpya anaonekana mgeni, anatakiwa kuanza upya kama wagombea wengine kutokana na idadi hii mpya kwa kujitambulisha kwa wapiga kura wale wapya waliongezeka ambao ni mabalozi na watu wake watano,” amesema.
Ameshauri kwamba kupitia utaratibu huo na idadi ya wapiga kura kuongezeka ni lazima kura za maoni zitapigwa katika matawi na hapo kila mtia nia lazima aweke wakala wa kumlindia na kumhesabia kura zake kwa sababu haitowezekana wapiga kura karibu 8,000 wakakusanywa katika ukumbi mmoja.
“Kwa idadi ya wajumbe hao huwezi kutarajia matokeo yapatikane siku hiyo hiyo ya kupiga kura kwa sababu itakuwa vrurugu na utaratibu utakuwa mbovu. Mtia nia lazima atafute wakala wako wa kusimamia kura zao na hiyo ni gharama nyingine,” amesema na kuongeza:
“Sasa hivi kampeni zitapigwa katika matawi na mashina. Kabla ya utaratibu huu watia nia walikuwa wanataka kufanya mambo kwa mazoea kwamba katibu kata wa CCM ndiyo kila kitu kwa hiyo ndiyo walikuwa wanawawezesha. Makatibu kata wameshakula mno fedha za wagombea.
“Yaani kwa idadi hii ya wapiga kura mtia nia wa ubunge aseme tu kwamba anataka kuwawezesha wajumbe wote kwa kuwapa Sh 30,000 labda fanya kwa asilimia 75 ya wapiga kura wote 8,000 maana yake karibu Sh milioni 200 kasoro imekatika, kwa hiyo kutakuwa na vurugu za watia nia za kuwawezesha wajumbe ili wawachague maana mmoja akitoa kiasi fulani na mwingine atatoa zaidi ya hapo.”
CCM Dar watoa neno
Katibu wa CCM Mkoa wa Dar es Salaam, Elias Mpanda, ameiambia JAMHURI wiki iliyopita kwamba wako katika mchakato wa kuanza kutoa elimu kwa watendaji wa chama hicho kuanzia ngazi za wilaya, kata hadi matawi kuhusu mabadiliko hayo.
“Kama mkoa hatuna watu wanaopiga kura bali wako katika ngazi za chini kwa maana kuanzia mashina, matawi, kata hadi wilaya, kwa hiyo sasa hivi tunajipanga kuwaelimisha watendaji katika maeneo yao. Tukishafanya hivyo wakaelewa ndiyo tunaanza na hiyo orodha ya wapiga kura wawajue ni watu gani?
“Hadi sasa hivi idadi kamili ya wapiga kura watu wengi hawaijui japo imeongezeka ambayo ni viongozi wa jumuiya za chama waliokuwa hawapigi sasa watapiga kura kupitia mabadiliko haya. Kwa sasa nao wamekuwa ni sehemu ya wapiga kura,” amesema.
Mbali na hayo, amesema mabadiliko hayo yamefanywa kwa ajili ya kupanua wigo wa demokrasia ndani ya chama hicho.
“Idadi ya watu wanaopiga kura za maoni imeongezeka na sasa si kikundi cha watu wachache kama ilivyo zamani.
“Tumepanua wigo ili kupata maoni ya wanachama wengi zaidi kwa ajili ya kumtafuta mtu atakayewawakilisha bungeni na katika baraza la madiwani,” amesema.