Na Mwandishi Wetu, JamhuriMedia, Ludewa

• Waziri Chana afungua mafunzo kuwawezesha kukuza mitaji

Vikundi nane vya Wajasiriamali kutoka Halmashauri ya Wilaya ya Ludewa vimenufaika na mtaji wezeshi kutoka Benki ya CRDB kiasi cha shilingi milioni 101.6 kwa ajili ya kuimarisha biashara zao na kukuza mitaji.

Hafla ya kukabidhi hundi hiyo imefanyika leo Septemba 18,2024 sambamba na ufunguzi wa semina ya siku moja ya kuvijengea uwezo vikundi vya wanawake wajasiriamali na vijana wanufaika wa programu ya Imbeju katika Halmashauri ya Ludewa.

Waziri wa Maliasili na Utalii na Mbunge wa Viti Maalum Mkoa wa Njombe, Mhe. Balozi, Dkt. Pindi Chana amefungua rasmi mafunzo hayo na kuwataka wanufaika kutumia vizuri mafunzo ya ujasiriamali yanayotolewa na Benki ya CRDB.

Vikundi vilivyopokea hundi hiyo ni Faraja Luilo, Hope Women Mlangali, Lake Nyasa, Nipende Group, Tupendane Lupanga, Wanawake Luilo, Wanawake Mwangaza Luilo na Mboga Mboga Group.

Akizungumza wakati wa ufunguzi wa Semina hiyo ya Imbeju inayotolewa na CRDB Bank Foundation, Mhe. Chana ameweka bayana kuwa huo ni mwendelezo wa juhudi za Serikali inayoongozwa na Mheshimiwa Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan katika kuhakikisha anaboresha maisha ya wananchi hasa vijana na wanawake kwa kuweka sera zinazoruhusu uwezeshaji wananchi kiuchumi.

Amesisitiza kuwa ni vyema wananchi hasa wanawake na vijana wakatumia vizuri kila fursa ya mafunzo na kuzingatia mafunzo wanayopewa ili kukuza uchumi wao binafsi.

“Uwepo wa Taasisi ya CRDB Bank Foundation Wilayani Ludewa ni fursa kwa wanawake na vijana wa Halmashauri hii kuelimika na kuanza kufanya biashara kwa malengo makubwa yatakayosaidia kukuza kipato cha mtu binafsi, uchumi wa kaya na taifa kwa ujumla” amesisitiza Mhe. Chana

Naye, Meneja wa Benki ya CRDB, Kanda ya Nyanda za Juu Kusini, Jenipher Tondi amesema akuwa mafunzo hayo yatasaidia kukuza biashara za wajasiriamali, kutanua mitaji yao na kuimarisha kipato binafsi huku akiwataka kutumia mafunzo hayo vizuri kuimarisha kipato na kukuza Uchumi.

“Programu hii iliyozinduliwa mwaka 2023 inalenga kuboresha maisha ya wananchi na kuchochea ustawi wa jamii” amesisitiza.

Hafla hiyo imehudhuriwa na viongozi mbalimbali wa Chama na Serikali pamoja na wananchi kutoka Halmashauri ya Wilaya ya Ludewa.