Vikosi vya usalama nchini Venezuela vimerusha mabomu ya kutoa machozi na risasi za mpira dhidi ya raia waliokuwa wameandamana kwa sababu ya matokeo ya uchaguzi wa Jumapili yenye utata.
Maelfu ya watu walikusanyika katikati mwa Caracas Jumatatu jioni, wengine wakitembea umbali wa maili kutoka makazi ya vijijini kwenye milima inayozunguka jiji hilo, kuelekea ikulu ya rais.
Maandamano yalizuka katika mji mkuu wa Venezuela siku moja baada ya Rais Nicolas Maduro kudai kuwa ameshinda.
Upinzani umepinga ushindi wa Bw Maduro na kuuchukulia kama ulaghai, ukisema mgombea wake Edmundo González alishinda kwa kishindo kwa kupata asilimia 73.2 ya kura.
Kura za maoni kabla ya uchaguzi huo zilipendekeza ushindi wa moja kwa moja kwa mpinzani.
Vyama vya upinzani viliungana nyuma ya Bw González katika jaribio la kumng’oa Rais Maduro baada ya kukaa madarakani kwa miaka 11, huku kukiwa na hali ya kutoridhika iliyoenea kutokana na kudorora kwa uchumi nchini humo.
Nchi kadhaa za Magharibi na Amerika Kusini, pamoja na mashirika ya kimataifa ikiwa ni pamoja na UN, wametoa wito kwa mamlaka ya Venezuela kutoa rekodi za kupiga kura kutoka vituo vya kupigia kura.
Kundi kubwa la wanajeshi na polisi, ikiwemo mabomu ya kutoa machozi, walionekana kwenye mitaa ya Caracas kwa lengo la kujaribu kuwatawanya waandamanaji na kuwazuia kukaribia ikulu ya rais.
Umati wa watu uliimba “Uhuru, uhuru!” na kuitaka serikali kuang’atuka madarakani.