Vikao vya wazi na rais vinafaa, pamoja na kwamba Rais Magufuli ‘anatisha’.

Mmoja wa waalikwa wa kikao kilichoitishwa Ikulu na Rais John Magufuli ametamka kuwa Rais “anatisha”. Yapo mazingira yanayohitaji rais kutisha, kama kutisha kunaleta pia uadilifu na uwajibikaji ndani ya utumishi wa umma.

Lakini kutisha kunaweza pia kuzuia taarifa muhimu kumfikia rais. Aliyetishika kasema kuwa si rahisi kuongea yote yaliyo moyoni mbele ya rais, akipendekeza ingekuwa rahisi zaidi kufanya hivyo kwenye kikao na mawaziri husika.

Utaratibu wa kiongozi kukutana ana kwa ana na wadau mbalimbali kupata maoni ya moja kwa moja kutoka kwao unatumika katika nchi kadhaa. Zipo faida na hasara za utaratibu huu.

Uwezo wa binadamu kusimama na kuongea mbele ya hadhira unapishana miongoni mwetu. Wapo wanaomudu, lakini wapo ambao wanatapatapa na kushindwa kuwasilisha hoja iliyonyooka. Tumeshuhudia watendaji waliyoinuliwa mbele ya viongozi na wakababaika na kushindwa kutaja kwa usahihi hata majina yao wenyewe.

Uzoefu wa kuongea kwenye hadhira ni suala moja; uwezo wa kudhihirisha uwezo huo mbele ya rais ni jambo tofauti kabisa. Rais ni rais, siyo jamaa yako unayeongea naye kijiweni.

Wale wenye uzoefu wa kuongea, hata mbele ya rais, wanapopata fursa hiyo hawapati shida kubwa kutaja hitilafu zilizopo kwenye sera, kanuni, sheria, miongozo, na mifumo ya utekelezaji.

Tatizo litajitokeza inapobidi, kama ambavyo inalazimika kutokea, kuanza kunyooshea vidole wale wenye majukumu ya utekelezaji. Nia ya kutekeleza jambo na uwezo wa kutekeleza jambo ni masuala mawili ambayo hayana ulazima wa kuambatana, moja baada ya jingine.

Kubaini matatizo katika utekelezwaji kunahitaji kutaja pia ubovu wa watendaji, ubovu ambao unachangiwa na uwezo mdogo wa kusimamia kazi au masuala mengine ya makusudi kama rushwa.

Watu wenye ujasiri wa kuongea kwenye hadhira iliyoitishwa na rais, pamoja na ujasiri wa kutaja hadharani hitilafu za watendaji wanaoshindwa kusimamia vyema programu za utekelezaji za serikali ni wachache.

Kwenye filamu ya mashujaa wa vita wa nchini Marekani mmoja wa wanaohojiwa anasema kuwa si rahisi kutabiri kwa kumuangalia tu mwanajeshi na kuamua kuwa huyu atakuwa shujaa wa vita, na huyu mwingine hawezi kuwa shujaa wa vita.

Ni mazingira yale ya kukabiliana na adui vitani yanayomlazimisha shujaa mtarajiwa kufikia uamuzi kuwa upo uwezekano mkubwa kuwa mapambano ya silaha anayokabiliana nayo yanamwelemea kwa kiasi kikubwa na kuna nafasi ndogo sana ya kuokoa maisha yake.

Nafsi ya shujaa mtarajiwa ikishakubali kuwa yuko tayari kwa lolote, hata kupoteza maisha yake, basi anabadilika kutoka mwanajeshi wa kawaida tu na kuwa shujaa ambaye anaweza kukabiliana na upinzani mkubwa kabisa ambao huwaacha wachambuzi wakishangaa juu ya uwezo wa mpambanaji mmoja kukabiliana na maadui wengi.

Kuongea bila woga na ikibidi kutaja watu ambao ni vikwazo kwa maendeleo ni suala ambalo linahitaji ujasiri na ushujaa ule ule wa mpambanaji mwenye silaha ambaye hana hakika juu ya hatima yake. Anayesema ukweli uraiani anajiweka kwenye hatari hata ya kupoteza maisha yake.

Kuacha jamii fulani ambazo zina sifa ya kusema yaliyo moyoni bila woga wowote, jamii nyingi za Kitanzania hufumbia macho vitendo vinavyochelewesha maendeleo yao.

Aliyesema Rais Magufuli anatisha angesema pia kuwa Watanzania hawana uwezo mkubwa wa kuweka bayana matatizo yanayojitokeza ndani ya jamii, na hasa kama matatizo yenyewe yanasababishwa na watendaji ambao tunaishi nao na tunafanya nao kazi.

Lakini pamoja na kutaja udhaifu huu, hakuna ubishi kwamba suala la utumbuaji majipu, kama nyenzo muhimu ya kubaini na kuleta suluhisho dhidi ya vikwazo vya maendeleo, ni suala muhimu sana.

Hata hivyo, tukubali kuwa yale tuliyoweza kuyasikia kwa sababu ya kutangazwa mubashara yangekuwa mengi zaidi kama yasingewekwa hadharani na yangetengenezewa mfumo unaowasilisha taarifa zile zile bila kuwekwa wazi.

Lakini hakuna maneno yanaweza kutosha kueleza umuhimu wa vikao hivi vya wazi kwa sababu vinaondoa ukuta unaozuia taarifa muhimu kupenya. Wanaotambua kuwa wao ni vikwazo vya kuleta ufanisi hawatapenda kuanikwa hadharani. Na inapotokea ni hao hao ndiyo wanapewa jukumu la kufikisha taarifa muhimu kwa wakubwa, hizo taarifa hazitafika.

Kama utaratibu huu utaendelea ni muhimu kwamba katika ngazi za awali viongozi wa juu wasihusishwe kwa sababu watakuwa wanafanya baadhi ya kazi ambazo zinapaswa kufanywa na wale walioteuliwa kusimamia majukumu mbalimbali. Kwamba hilo linatokea ni hitilafu ambayo inahitaji suluhisho. Lakini kwa sasa tusidanganyane kuwa tumefikia hatua nzuri ya maendeleo na tukaacha wateule wafanye kazi zao bila kusimamiwa.

Haihitaji utafiti wa kina kubaini kuwa taarifa nyingi kwenye vyombo vya habari zinataja matukio yanayohusu kukosekana kwa uadilifu na uwajibikaji miongoni mwa wateule na viongozi wa kuchaguliwa.

Kwa hiyo ni muhimu iwepo fursa mara chache kila mwaka kwa wadau mbalimbali kukutana na rais, au kiongozi mwingine wa ngazi ya juu, kwa madhumuni ya kukusanya maoni juu ya masuala ya maendeleo yanayoikabili nchi yetu na kusaidia kuimarisha uadilifu na uwajibikaji kwenye utumishi wa umma.

Kama wanaochangia kwenye vikao watakuwa wakweli na siyo wapika majungu, basi vitakuwa vikao vyenye manufaa makubwa kwa taifa.