Usambazaji umeme vijijini mkoani Iringa umefanyika kwa asilimia 100 ambapo vijiji vyote 360 mkoani humo vimesambaziwa umeme kupitia miradi mbalimbali inayotekelezwa na Wakala wa Nishati Vijijini (REA).
Usambazaji umeme katika vitongoji vya Mkoa huo umetekelezwa kwa asilimia 64.11 ambapo vitongoji 1,188 vimesambaziwa umeme kati ya 1,853.
Hayo yametanabaishwa wakati wakati wa ziara ya Naibu Waziri Mkuu na Waziri wa Nishati, Mhe. Dkt. Doto Biteko mkoani Iringa kwa ajili kuwasha umeme na kukagua miundombinu ya umeme.
Baada ya kuwasha umeme kwenye Kijiji cha Mkangwe wilayani Mufindi, Dkt. Biteko amewataka wakandarasi wa miradi ya usambazaji umeme vijijini kutekeleza kazi kwa wakati ili kuendana na kasi ya maendeleo huku akiiagiza REA kuwachukulia hatua wakandarasi wazembe.
Aidha, amewapongeza Wakandarasi wa umeme vijijini waliofanya kazi ya usambazaji mkoani Iringa ambayo imepelekea vijiji vyote mkoani humo kuwa na umeme kufikia Desemba 2023.
Akiwa katika Kijiji cha Mkangwe, Dkt. Biteko alizindua Zahanati ya Kijiji cha Mkangwe ambapo aliagiza uongozi wa Halmashauri wilayani Mufindi kuhakikisha Zahanati hiyo inaanza kuhudumia wananchi ipasavyo
kufikia jumatatu ya tarehe 26 Februari 2024 baada ya huduma ya umeme kufika kwenye zahanati hiyo na hii ikijumuisha kuwepo kwa Rasilimali Watu na Vitu.
Katika hatua nyingine, Dkt. Biteko amewaasa Wanachama wa Vyama mbalimbali vya Siasa kwenye mkoa huo kupendana na kushirikiana katika shughuli za kiuchumi na kijamii na kamwe itikadi zao za vyama zisiwafanye watengane na kutoshirikiana.
Kuhusu uchaguzi wa Serikali za Mitaa utakaofanyika mwaka huu, Dkt. Biteko amewaasa wananchi kuchagua viongozi wanaowasikiliza, wanaotambua changamoto zao na jinsi ya kuzitatua; pia amewataka wagombea kutozungumza lugha za maudhi wakati wa uchaguzi huo kwani Rais, Dkt. Samia Suluhu Hassan anataka maridhiano kwenye nchi na si kugawanyika.
Hafla ya uwashaji umeme katika Kijiji cha Mkangwe wilayani Mufindi ilihudhuriwa na viongozi mbalimbali akiwemo Mkuu wa Mkoa wa Iringa, Halima Dendego, Mkuu wa Mkoa wa Njombe, Anthony Mtaka, Mbunge wa Mufindi Kusini, Mhe.David Kihenzile na Mwakilishi wa Katibu Mkuu wa Wizara ya Nishati, Mhandisi Innocent Luoga.