Na Mary Margwe, JamhuriMwdia, Mbulu

Vijiji vitano vya Gedamar, Qatesh, Landa, Murray na Nahasey katika Halmashauri ya Mji wa Mbulu Mkoani Manyara vinatarajia kunufaika na Mradi wa Maji kupitia Program ya visima 900 chini ya Wakala wa Maji na Usafi wa Mazingira Vijijini ( RUWASA)

Akisoma taarifa ya ujenzi wa Mradi huo mbele ya Mbunge wa Jimbo la Mbulu Mjini Zacharia Paulo Isaay, Kaimu Meneja wa Wakala wa Maji na Usafi wa Mazingira Vijijini ( RUWASA ) John Michael Ombay amesema ujenzi wa Mradi huo uko katika Kijiji Cha Gedamar, huku alisema kuwa kiwango cha upatikanaji wa maji kitapanda hadi asilimia zaidi ya 85%. Kutokana Kasi ya utekelezaji wa Miradi ya maji wilayani humo.

Ombay amesema Mradi huo utawanufaisha wananchi wa Vijiji vitano (5) vya Gedamar Qatesh Landa Murray na Nahasey, na ulianza ujenzi wake mnamo February 20, 2025 huku ukitarajiwa kukamilika Aprili 10, 2025 na ukiwa na gharama ya sh.mil.70

” Mradi huu ni Program ya muda mfupi ya kuhakikisha wananchi wanaanza kupata huduma ya Maji karibu na eneo la kisima wakati Fedha za Usambazaji maji kwenye Kijiji kizima zikiwekwa kwenye mpango wa Serikali ” amesema Ombay.

” Katika Jimbo la Mbulu Mjini Program ya visima 900 imeleta neema katika vijiji vitano ambavyo ni Gedamar, Qatesh, Landa, Murray na Nahasey ambapo kazi ya ujenzi Wake unaendelea, katika vijiji vya Gedamar, Landa Murray na Nahasey ujenzi wake upo asilimia 65 ” amesema Ombay.

Aidha Ombay amesema matarajio ya ujenzi wa Mradi point source ni kukamilika ifikapo Aprili 20,2025, ambapo mifumo ya solar na pump itakua imefungwa na huduma ya Maji kuanza kutumika Kwa wananchi.

” Mradi huu wenye gharama ya sh.mil.70 ikiwa ni kwa ajili gharama ya kumlipa fundi anayejenga, ununuzi wa vifaa vya ujenzi, Solar panels, na pampu, ambapo mpaka sasa hakuna malipo yaliyofanyika” amefafanua Ombay.

Aidha Ombay amesema jumla ya Wananchi wapatao 218,034 kati ya Wananchi 350,573 katika vijiji 110 vinavyohudumiwa na wakala wa Maji na Usafi wa Mazingira Vijijini ( RUWASA ) Wilayani Mbulu Mkoani Manyara wananufaika na Miradi iliyotekelezwa katika kipindi cha Serikali ya awamu ya 6 chini ya Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan

Aidha Kaimu Meneja ameongeza kuwa baada ya mradi wa kisima kinachochimbwa kwa gharama ya million 70 kukamilika, sehemu ya wananchi wa kijiji cha Gedamar wataanza kupata huduma ya maji safi na salama huku Idadi ya watu watakaohudumiwa na mradi huu ikiwa ni 650 Sawa na asilimia 30% ya wananchi wote wa Kijiji cha Gedamar ambao ni 2,152 kwa mujibu wa sensa ya 2022.

Kwa upande Mbunge wa Jimbo la Mbulu Mjini Mhe. Issaay Zacharia Paulo amewahimiza wananchi kutunza vyanzo vya maji na kuhimiza upandaji wa miti ili kukabiliana na athari za mabadiliko ya tabia ya nchi.

” Naomba sana tutunze vyanzo vyote vya maji li navyo ije vitutunze sisi na vizazi vyetu vyote, tuheshimu mipaka yote iliyowekwa katika vyanzo vya maji na pale panapotokea ukiukwaji wa utunzaji na matumizi ya vyanzo hivyo, sheria ichukue mkondo wake” amesema Mbunge Isaay

Nao baadhi ya wananchi akiwemo Sophia Bura akizungumza kwa niaba ya akina mama katika Kijiji Cha Gedamar ameishukuru serikali ya awamu ya sita ya Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan kwa kuwachimba kisima katika kijijini na kwamba itasaidia kupunguza adha ya upatikanaji wa maji kijijini hapo.

Mbunge wa Jimbo la Mbulu Mjini Mkoani Manyara Zacharia Paulo Isaay akiweka Jiwe la Msingi kwenye Ujenzi wa Mradi wa Maji kupitia Program ya Visima 900 katika Kijiji cha Gedamar , ambapo katika Jimbo la Mbulu Mjini jumla ya vijiji 5 vya Gedamar, Qatesh, Landa, Murray, na Nahasey vitanufaika na Program hiyo, Picha na Mary Margwe