Nchi imekuwa katika hali ya wasiwasi na ya sintofahamu juu ya Uchaguzi Mkuu wa mwaka huu. Aidha, pamekuwapo minong’ono au ati kuwa huenda uchaguzi usifanyike mwaka huu wa 2015.
Huko nyuma kama tunakumbuka Waziri Mkuu aliwahi kusema bungeni kuwa Uchaguzi Mkuu mwaka huu upo kama ilivyopangwa. Mheshimiwa Rais wa Jamhuri akiwa katika sherehe za kilele cha Siku ya Wafanyakazi (Mei Mosi) mkoani Mwanza, alitamka uchaguzi mwaka huu upo Oktoba.
Licha ya uthibitisho wote huo kutoka kwa wakuu hao, eti bado walijitokeza baadhi ya wanasiasa, tena viongozi wa vyama vya siasa kutokuamini matamshi kutoka kwa viongozi wakuu wa Serikali. Kidini watu namna hii tunawaita akina Thomas wasioamini (doubting Thomas).
Hatimaye Tume ya Uchaguzi ya Taifa imetangaza ukweli wa mambo. Mwenyekiti wa Tume ya Uchaguzi, Jaji mstaafu Damian Lubuva alitangaza mbele ya vyombo vya habari mchana kweupee ratiba yote ya Uchaguzi Mkuu mwaka huu. Hii imekuwa ndiyo mruturutu wa wanasiasa wakorofi na wazushi na kuwakata kilimilimi chao kueneza wasiwasi eti uchaguzi haupo au Serikali ina mbinu za kujiongezea muda wa kukaa madarakani.
Kisheria kuna mamlaka moja tu katika nchi yenye jukumu la kutamka tarehe ya uchaguzi na taratibu zake. Hivyo ilikuwa wakati sahihi kwa Mwenyekiti wa Tume ya Uchaguzi kutamka yale aliyoyatamka. Tume ilitangaza kuwa:-
Uteuzi wa wagombea katika Uchaguzi Mkuu utakuwa Agosti 21. Wagombea watarajiwa watajinadi kwa wapigakura kuanzia Agosti 22 na kuhitimisha kampeni zao Oktoba 24.
Uchaguzi Mkuu kwa Madiwani, Wawakilishi, Wabunge na Rais utakuwa Jumapili ya Oktoba 25, mwaka huu.
Sisi wa Kusini tumezoea kusema “KUCHILE” (Kingoni) KUCHELE (Kiyao) na kwa Kiswahili lugha ya Taifa tunasema tu “KUMEKUCHA”. Sasa mambo yote yako wazi hadharani, hakuna mwanasiasa wa kurubuni wananchi kwa upotoshaji wa aina yoyote ile. Huu ndiyo uwazi unaokuwa unangojewa na wananchi wote. Tamko la mamlaka husika kisheria, na ndilo hili limetoka na Uchaguzi Mkuu upo mwaka huu.
Mimi nimeonelea vema kuwachotea vijana wetu historia ya uchaguzi uliotokea katika nchi yetu na namna wananchi walivyoshiriki.
Nchi yetu ilianza na uchaguzi wa vyama vingi, tukaingia kwenye uchaguzi wa chama kimoja cha siasa na sasa tumerejea kwenye uchaguzi wa vyama vingi vya siasa. Huko ndiko tuendako Oktoba ijayo. Katika suala hili la uchaguzi sisi sote tu wadau, mradi tuwe tumejiandikisha katika lile Daftari la Wapigakura.
Historia ya nchi yetu, Tanganyika iko wazi kabisa katika kudhihirisha uwezo wa vijana wa nchi hii kufanya mambo makubwa. Kwanza, vijana wana nguvu za kufanya kazi kwa muda mrefu. Vijana wasomi wanaelewa upesi sana mambo yanayotokea au yanayotendeka katika dunia ya leo. Imedhihirika duniani kuwa vijana wakishika madaraka ya uongozi wanafanya mambo kwa uhakika. Wanaweza kukabiliana na changamoto mbalimbali za maisha na wako tayari kubuni mambo mapya.
Hebu turudi nyuma tulikotoka katika nchi yetu. Wakati wa harakati za kutafuta Uhuru wa nchi yetu vijana ndio waliokuwa mstari wa mbele kushabikia Uhuru wetu. Walipanga mikakati yakinifu kwa ubunifu mkubwa, wakashikamana na wazee katika mapambano yale ya kudai Uhuru. Sote tunajua TANU ilivyozaliwa. Miongoni mwa wale waasisi 17 wa chama hiki, mmoja tu ndiye aliyekuwa mzee- ndiye Mzee John Rupia. Kwa umri huyu ni mzee. Wale 16 wote walikuwa vijana wa enzi zile. Umri wa vijana wale ulikuwa kati ya miaka 24 – 34 tu, ndiyo kusema walikuwa bado wabichi.
Rais wa Kwanza wa TANU Mwalimu Julius Kambarage Nyerere alikuwa na umri wa miaka 32 tu. Katibu wake Zuberi Mtemvu alikuwa na miaka 26 tu mwaka ule wa mwaka 1954. Katika waasisi wale, labda Japhet Kirilo na Kasela-Bantu walifikia umri mkubwa kidogo. Wengine wote walizaliwa kati ya mwaka 1922 – 1929.
Kwa faida ya kizazi cha leo hapa nawaorodhesha vijana mashujaa wale na ndio waasisi wa Uhuru wa Taifa letu. Julius Kambarage Nyerere (Jimbo la Mashariki), Germanus Pacha (Jimbo la Magharibi). Yosefu Kimalando (Kaskazini) Japhet Kirilo (Kaskazini) Constantine Oswald Milinga – yungali hai na mkongwe bado anaishi Morogoro (Mashariki), Abubakar Ilanga (Ziwa), Lameck Bogohe Makaranga (kafariki Aprili 2015 hii – Ziwa) Saadan Abdi Kandoro (Ziwa), SM Kitwana (Ziwa), Kisung’uta Gabara (Ziwa), Tewa Saidi Tewa (Mashariki), Dossa Aziz (Mashariki), Abdul W. Sykes (Mashariki), Patrick Kunambi (Mashariki), Ally Sykes (Mashariki), na Mzee John Rupia (Mashariki).
Nimeonesha majimbo walikotokea kuja hapa Dar es Salaam kwa ule mkutano muhimu uliounda TANU tarehe 7 Julai 1954 pale Lumumba. Siku hizo majimbo yalikuwa manane tu hapa Tanganyika. Basi unapoona Jimbo la Ziwa ni kote Mwanza, Musoma na Kagera lilikuwa Jimbo moja tu. Mashariki ni pamoja na Dar es Salaam, Pwani na Morogoro, wakati Kaskazini ni Kilimanjaro, Arusha na Manyara -Jimbo moja tu.
Baada ya ufafanuzi huo wa kihistoria juu ya vijana waliojitolea kudai Uhuru wa Taifa hili na maeneo walikotoka, tuone Serikali ya kwanza iliongozwa na watu wa namna gani.
Desemba 9, 1961 tulipopata Uhuru, madaraka yote makubwa kiutawala yalishikwa na vijana wa siku zile waliopigania Uhuru. Baraza la Mawaziri liliongozwa na Waziri Mkuu kijana Mwalimu Julius Kambarage Nyerere akiwa na umri wa miaka 39. Mawaziri wake karibu wote walikuwa na umri kati ya miaka 40 (Chief Abdallah Fundikira) na miaka 33 (Oscar Kambona). Hao ndio viongozi waliopewa dhamana ya Uhuru wa Taifa hili. Waliunda Serikali ya vijana watupu.
Mwaka 1962 Tanganyika ilipokuwa Jamhuri, ndipo Rais wake Mwalimu Nyerere alikuwa na umri wa miaka 40. Ukaja Muungano wa Jamhuri ya Tanganyika na Jamhuri ya Zanzibar tarehe 26 Aprili 1964.
Kwa Muungano ule sasa Serikali ya Jamhuri ilipata viongozi vijana na wazee. Rais wa Jamhuri hiyo mpya Mwalimu Nyerere alikuwa na miaka 42, Makamu wa Kwanza Sheikh Abeid Amani Karume alikuwa na umri wa miaka 59, na baadhi ya mawaziri kama akina Aboud Jumbe alikuwa na umri wa miaka 44.
Kwa kuwa sheria ya nchi yetu imetamka wazi kuwa uzee ni kuanzia miaka 60, hapo ni dhahiri, Tanzania ki-uongozi kwa miaka mingi imeongozwa na vijana na watu wazima. Wazee hawakuwapo katika nyadhifa za uongozi katika Serikali. Basi, kwa historia namna hii, Watanzania tumeona kuwa vijana wa Taifa hili wameweza kuendesha nchi hii kwa amani, utulivu na kwa mafanikio makubwa sana wakalifikisha Taifa hapa tulipo.
Vijana wale wa mwaka 1954 walikua katika umri, walipevuka katika uongozi wa Serikali na hatimaye walipozeeka wakabuni njia ya amani ya kukabidhi uongozi kwa njia ya awamu na ya kistaarabu.
Uzee una upungufu kadhaa. Nguvu za kutenda kazi zinapungua, fikra ya kubuni mambo mapya zinafifia. Ule wepesi wa kusafiri huko na huko kukagua maendeleo unapunguka. Wazee walipojitambua upungufu namna hiyo kimwili (physical) na ya kiakili (mental), wakaleta neno KUNG’ATUKA (neno la Kizanaki) maana yake kuachilia madaraka na kwenda kupumzika! Sote tunajua Baba wa Taifa- mwasisi wa neno “kung’atuka”, aliachilia madaraka ya utawala katika Serikali mwaka 1985. SASA ALISTAHILI KUTAMBULIKA KAMA Mzee, maana mwaka huo alitimiza umri wa miaka 63.
Mwaka huo wa 1985 ndipo akaona uongozi endelevu unafaa kuachiwa watu chini ya miaka 60; umri ambao mtu anakuwa bado ana nguvu za kimwili na za ki akili.
Nchi za magharibi nazo zilifikia wakati, uongozi waliachiwa vijana, wazee wakapumzika. Hii ilitokea Marekani pale Taifa lile lilipomchagua mwaka ule 1961 kijana John Kennedy (miaka 44 tu) kuwa Rais wao. Huko Uiongereza chama cha mamwinyi (Conservative) kilimpa uongozi kijana Cameroon mwaka 2011 kuwaongoza akiwa ana umri wa miaka 45 na ndiye anayetawala hivi sasa.
RaisBarack Obama wa Marekani alipokea dhamana ya kutawala Marekani akiwa na umri wa miaka 47 tu. Kumbe inaonekana kuwa Kennedy alikuwa na miaka 44, Obama alikuwa na miaka 47, na Cameroon alikuwa na miaka 45. Huu umekuwa ni mtindo wa siku hizi kuwapa uongozi vijana wenye nguvu za kumudu mikikimikiki ya utandawazi wa dunia yetu ya leo.
Mwaka huu nchi yetu itafanya Uchaguzi kwa Madiwani, Wabunge, Wawakilishi na Rais. Tumeanza na kaulimbinu “Tufunge Safari” tunasikia katika Channel Ten kuelekea huko kwenye Uchaguzi Mkuu mwezi Oktoba. Inshallah Mungu atatujaalia.
Sasa kunasikika miruzi mingi hapa nchini kuhusu Uchaguzi. Wapo vijana, watu wazima na hata wazee wanatarajia kujitokeza kuwania nafasi mbalimbali katika uchaguzi huu. Wapo wenye kuwania urais na wapo wale wanaowania ubunge na udiwani. Hapa ndipo inafaa tujiulize vyama vyetu vya siasa vimewaandaa vipi vijana kwa kuwania uongozi katika nafasi mbalimbali? Taifa linawafikiriaje vijana wake?
>> ITAENDELEA>>
Mwandishi wa Makala hii, Francis Mbenna ni Brigedia Jenerali mstaafu wa Jeshi la Ulinzi la Wananchi wa Tanzania (JWTZ), mwenye makazi yake jijini Dar es Salaam.