DAR ES SALAAM
Na Pawa Lufunga
Desturi za maisha ya jamii zinabadilika kila siku kutokana na mageuzi mbalimbali ya vitu na mazingira.
Mabadiliko haya yanayochochewa na vitu vya asili na hata matendo ya binadamu huchochea pia mabadiliko katika tabia na mifumo ya maisha katika nyanja za uchumi, utamaduni, mitazamo na siasa.
Zipo sifa za makundi ya jamii katika umri, kabila, koo, kanda na dini ambazo huwa kama utambulisho wa jamii, hivyo kuwapo kwa tabia au sifa za vijana/wazee; sifa za kabila fulani, za jamii au kanda fulani, waumini wa dini fulani, wanawake na mambo kama haya.
Mipaka hiyo imesababisha ubaguzi katika fursa mbalimbali ikiwamo uongozi, utoaji uamuzi na shughuli za kijamii.
Zipo jamii ambazo hadi leo kutokana na misingi hiyo, baadhi ya makundi hunyimwa sifa za kushiriki mambo kadhaa muhimu yanayohusu maisha yao, pengine kutokana na mtazamo wa jamii juu ya tabia ya kundi husika.
Hoja ya makala hii ni vijana katika nafasi za uongozi wa juu.
Katika jamii nyingi duniani, vijana wananyimwa nafasi ya kushika nyadhifa za juu katika uongozi.
Pengine ni kutokana na uelewa mdogo juu ya vijana wenyewe uliojengwa na muundo wa elimu isiyowapa muamko juu ya nafasi yao katika masuala ya uongozi na utawala wa nchi zao.
Mambo haya hayana mjadala mpana mahali popote na hata wanasiasa na wanaharakati wengi wa usawa wa kijinsia huishia kujadili nafasi za wanawake (na au wanaume), wakienda mbali kidogo huishia kutetea makundi ya walemavu.
Lakini kundi la vijana limewekwa kando huku ubaguzi huu ukihalalishwa na misingi ya sheria, ikiwamo katiba za nchi.
Kwa mfano, Katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania imetamka wazi kuwa umri wa kugombea urais ni kuanzia miaka 40.
“Mtu hatastahili kuchaguliwa kushika kiti cha Rais wa Jamhuri ya Muungano isipokuwa tu kama ametimiza umri wa miaka 40.” Inasomeka Ibara ya 39(1)(b) ya Katiba.
Inaendelea kusema kuwa ni lazima awe mwanachama wa chama fulani cha siasa.
“Awe ni mwanachama, na mgombea aliyependezwa na chama cha siasa.” Ibara ya 39(1)(c) inaweka bayana.
Sifa hizo zinaweza kuonekana za maana kwa muktadha fulani lakini pia si njema sana kwa upande mwingine kwani zimeweka mfumo wa kubagua jamii na kuweka mipaka ambayo baadhi ya makundi yamezuiwa kushiriki siasa katika nafasi ya urais.
Kwa mujibu wa Mkataba wa Kimataifa wa Vijana (United Nations Youth Universal Charter), kijana anatambuliwa kuwa ni mtu mwenye umri kati ya miaka 15 hadi 35.
Lakini pia, Mkataba wa Vijana wa Afrika (African Youth Charter), kijana ametajwa kuwa ni mtu mwenye umri kati ya miaka 18 – 35.
Kwa kutumia kigezo hicho, ikiwa umri wa mtu kuruhusiwa kuwa kiongozi wa juu kama Rais sharti uanzie miaka 40, basi vijana wamenyimwa nafasi hiyo.
Hoja ya msingi hapa ni; je, sharti la umri wa miaka 40 kuwa ndiyo sifa ya kuwa kiongozi lina maana ya msingi?
Je, miaka 40 ni kipimo cha akili, hekima, nguvu, uzalendo na busara za uongozi bora?
Hivi, walioshiriki kuweka kigezo hicho walikuwa vijana na wazee au ni wazee pekee? Walilenga nini hasa? Haya ni baadhi ya maswali katika mjadala huu.
Wakati wa kulitafakari hili ni vema kurejea mifano kadhaa kutoka katika maisha halisi na nadharia zilizopo juu ya uwezo wa vijana na mahitaji ya nafasi hizo za uongozi.
Maandiko matakatifu, Biblia, yanawataja vijana kama kundi lenye nguvu na uwezo wa kufanya mambo makubwa na kufikia mafanikio.
Mithali 20:29 inamuelezea kijana kuwa na nguvu nyingi na Neno la Mungu linakaa ndani yake, hivyo amemshinda shetani.
Vivyo hivyo, Waraka wa Kwanza wa Yohana, 2:14, Yohana amewaandikia vijana kwa kuwa wana nguvu nyingi ili neno likae ndani yao.
Nadharia hii inatuonyesha kuwa vijana wanao uwezo, wanaweza, hata maneno matakatifu yanathibitisha hivyo.
Kubwa zaidi ni kwamba, inaelezwa kuwa, katika imani ya Kikristo kwa mfano, hata Yesu Kristo alianza kufanya mambo makuu akiwa kijana na amefanya makuu yote yaliyoandikwa katika vitabu vitakatifu angali kijana wa chini ya umri wa miaka 33.
Lakini katika mifano halisi ya hivi karibuni; Mwalimu Julius Nyerere alipata nafasi kuwa kiongozi wa juu wa Serikali ya Tanganyika akiwa na umri chini ya miaka 40 inayosimamiwa na Katiba yetu ya leo; kwani wakati wa Uhuru Desemba 1961, alikuwa na umri wa miaka 39!
Mbali na Mwalimu kuwa kiongozi mwenye hekima, nguvu na uwezo mkubwa duniani akiwa chini ya miaka 40, aliyekuwa Rais wa Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo (DRC), Joseph Kabila, aliingia madarakani akiwa na miaka 30 na amefanya mengi mazuri kwa taifa lake.
Kim Jong Un amekuwa mtawala wa Korea Kaskazini akiwa na miaka 35 na ameitetemesha dunia na kama hiyo haitoshi kuonyesha uwezo wa vijana katika uongozi, mwanadada Sanna Marin ameiongoza Finland akiwa na umri wa miaka 34, wakati Jacinda ameiongoza New Zealand akiwa na miaka 39 huku El Salvador ikiongozwa na Nayib Bukele tangu akiwa na umri wa miaka 38, na Ukraine imeongozwa na Oleksiy Honcharuk akiwa na umri wa miaka 35.
Viongozi wote hao wamefanya makubwa na baadhi yao wameongoza mataifa makubwa kiuchumi na kijeshi ulimwenguni.
Je, hoja kuwa Rais wa Tanzania awe mwenye umri usiopungua miaka 40 ina mashiko?
Kwa takwimu hizi na hata kwa hali ya kawaida, vijana ni kundi lenye uwezo mkubwa kiakili, bado wanafikiria kwa haraka zaidi, wana nguvu zaidi na wanaweza kufanya mengi wakakutana na kukabiliana na mikikimikiki mingi bila kuchoka.
Vijana ni kundi ambalo lina ndoto ya kufanya mambo na kufika mahali, hivyo hata katika masuala ya uadilifu na unyenyekevu mbele ya watu huenda likawa katika nafasi nzuri zaidi kuliko mzee ambaye amefanya shughuli nyingi huku na kule na anaamua kutafuta urais ili amalizie uzee; hana cha kupoteza tena.
Pengine kuwaweka kando wazee kwa sababu yoyote linaweza lisiwe jambo la msingi, hoja ya msingi ni ukweli kuwa vijana ni jeshi lenye nguvu zaidi na wanaendana na mabadiliko ya nyakati katika masuala ya fikra za kiutandawazi zinazochochewa na mabadiliko ya teknolojia, tabianchi na tamaduni za jamii mbalimbali ulimwenguni.
Vijana wanaweza, ipo haja kwa wadau wa masuala ya diplomasia na haki za binadamu kuona namna ya kufikiri kiusawa na kwa mustakabali mpana wa maisha ya binadamu na mahitaji ya uongozi katika kuamua sifa za mtu kuwa kiongozi bora katika masuala yote ya mipaka inayogawanya jamii kama masuala ya umri, vyama vya siasa, dini, kabila na kanda kulingana na changamoto inayoikabili nchi au jamii husika, kwani zipo nchi duniani watu wanapata uongozi kwa kuangalia maeneo hayo, yaani jinsia (me/ke), dini, kabila au rangi.
Tanzania suala la umri na lile la vyama vya siasa ni kigezo cha mtu kupata sifa ya kuwania uongozi wa nchi ambalo kimsingi si sahihi kabisa.
Mtu anaweza kuwania na akawa kiongozi bila kufungwa na chama cha siasa wala kuwa na umri wa miaka 50, 40 au 60, bali ni suala la hekima, nguvu, uwezo wa maarifa ya kizalendo na dhamira ya mtu ikisimamiwa na sheria nzuri zinazoelekeza mwelekeo na malengo ya jamii husika.
0622263599