Na Lookman Miraji, JamhuriMedia, Dar es Salaam
Vijana wa kike nchini wameaswa juu ya uthubutu katika shughuli za masuala ya ujenzi na uhandisi.
Ushauri huo umetolewa hapo jana katika mkutano wa mkuu wa nane wa masuala ya ujenzi uliofanyika katika ukumbi wa Diamond jubilee ulioko Upanga, Dar es salaam.
Mkutano huo umefanyika wakati maonesho ya ujenzi yakiendelea jijini Dar ea Salaam.
Akizungumza katika hafla ya kongamano hilo la wanawake , Bi:Lightness Salema ambae ni kiongozi wa taasisi ya wanawake katika masuala ya uongozi barani Afrika, amesema kuwa dhamira kuu ya kuandaliwa kwa kongamano hilo ni kuwasogezea fursa watanzania ya kupata uelewa zaidi juu ya masuala mbalimbali katika sekta ya ujenzi.
“Kikubwa kilichotusukuma kuandaa kongamano hili ni kuhakikisha kwanza tunawapa fursa watanzania kuelewa katika sekta ya ujenzi, kujua ni fursa zipi zinaweza kupatikana na wanaweza wakazifanyia kazi. Tumehamasisha watu kuhudhuria hili ili kujua unahitajika kuwa na nini ili uweze kunufaika ambapo pia tumetoa mafunzo mbalimbali na wasemaji waliohusika katika kongamano hili wametoa elimu juu masuala mbalimbali katika fani ya ujenzi.”
Kongamano hilo limefanyika huku likihusisha wadau wakuu wa mbalimbali katika sekta ya ujenzi na maendeleo ya wanawake pia.
Kwa upande wa wadau wa wadau wa sekta hizo miongoni mwake pia alikuwepo Bi:Maida Waziri ambae ni mkurugenzi mkuu wa kampuni ya ujenzi ya Ibra contractors na rais wa sauti ya wanawake wajasiliamali nchini.
Wakati wa hafla hiyo Bi: Maida amezungumzia mambo muhimu ya kuzingatia hasa katika fani ya ujenzi ambapo miongoni mwa mambo hayo ni kuhusu elimu juu ya kusajili, kumiliki pamoja na kufuata sheria katika ufunguaji wa kampuni na uendeshwaji wake ikiwa sehemu pekee ya kujijengea uaminifu kwa mashirika na makampuni ya uwekezaji mbalimbali kutoka nnje ya nchi.
Aidha pia msemaji huyo pia amegusia kuhusu mchakato wa uombaji wa tenda kupitia teknolojia ya mtandao. Maelezo ya hayo ameyasema huku akitambua wimbi kubwa la vijana waliopo katika jamii waliokosa elimu juu ya mambo ya teknolojia ya habari na mawasiliano ambapo kwa kutambua changamoto hiyo ametoa wito kwa vijana kujiandikisha katika kozi hiyo ambayo itakuwa ikiendeshwa katika chuo cha mafunzo Afrika mashariki kilichopo chang’ombe, Dar es salaam.
“Leo nimefarijika sana kukutanishwa na vijana pamoja na wanawake kuja kuona mambo mbalimbali yanayohusiana na ujenzi. Kubwa leo nimezungumza na vijana wetu hawa kuona ni namna gani wanaweza kurasimisha biashara zao ili kuweza kufikia fursa mbalimbali ambazo zinazowazunguka.”
“Pia nimezungumza nao kuhusiana masuala ya kuomba tenda yaani kama hauko katika mifumo inaweza ikakusumbua kuweza kufikia katika malengo uliyoyataka kwani kila kitu kwa sasa kinakwenda kwa teknolojia.”
“Hivyo baada ya kuzungumza nao maneno hayo nikawaambia kwamba kwakuwa mimi ni mkurugenzi wa chuo cha biashara Afrika mashariki kilichopo hapa Dar es salaam natoa nafasi za kujiunga na mafunzo ya usimamizi wa biashara pamoja na fani ya teknolojia ya habari na mawasiliano hivyo waweze kuikimbilia fursa hii kwani ni sehemu ya wao kuongeza ujuzi juu ya uendeshwaji biashara kisasa kupitia mtandao.” Alisema.