Vijana ni nguvu kazi ya taifa. Wao ndio tegemeo kubwa la kujenga na kuleta maendeleo ya taifa, hasa katika taifa linalokusudia kuleta maendeleo ya kiuchumi, kisayansi na kijamii. Ni yumkini taifa lisilo na vijana ni ufu.
Vijana hawa wapo wa kike na wa kiume ambao kwanza wanahitaji malezi na makuzi bora kutoka kwa jamii.
Jamii ndiyo kiini cha kutoa matunzo na mafunzo ya adabu, ujasiri na thamani ya kuwapo kwa vijana. Pili, hawana budi kupewa maneno ya utu na hekima wawe wananchi wema.
Vijana wanapojikita na kujizatiti katika masomo shuleni na mafunzo vyuoni, wanajenga silka ya kutambua na kuthamini mali na rasilimali za taifa lao.
Wanapofanya kazi kwa juhudi na maarifa, wanapolinda nchi kwa moyo na ujasiri, wanapo heshimu na kuhifadhi utamaduni wa taifa lao, ukweli wanachukua haiba ya kuwa wazalendo.
Vijana wanapokuwa na wingi wa adabu, heshima, utu, uungwana na ujasiri wanajijengea umahiri katika kufanya mambo mbalimbali ya kijamii na wanachukua nafasi ya kuaminika, kukubalika na kupendwa na jamii. Hakika vijana wanakuwa sura, ngao na hazina ya leo na kesho ya taifa.
Vijana wa leo ndio wazee wa kesho, ambao kwamba wanakuwa watu wenye hekima na wakufanya uamuzi wenye busara.
Kutokana na mantiki hii iko haja ya kuwalea na kuwatunza vema vijana. Kadhalika vijana nao wanao wajibu wa kujiheshimu na kujitunza kiafya ili baadaye wawe viongozi na washauri wema.
Hapa Tanzania tunao vijana wengi mno ambao ndiyo nguvu kazi ya taifa. Vijana hawa wanashughulika katika mambo na masuala mbalimbali. Kwa mfano katika michezo, biashara, ufundi, kilimo, kazi na siasa. Suala la kupata elimu, kufanya kazi na kufahamu mwenendo wa siasa nchini ni muhimu pia kwao.
Ni kweli kama tusemavyo siasa ni maisha na siasa ni mpango mzima wa uongozi na utawala katika nchi. “Siasa ni itikadi inayofuatwa na kundi au jamii fulani ambayo ni msingi wa kuendesha uchumi, utamaduni na mwenendo mzima wa maisha ya jamii.”
Katika nchi yetu tunavyo vyama vingi vya siasa, na viongozi wetu wanatokana na vyama hivyo. Ndani ya vyama hivyo wamo vijana ambao ni vuguvugu au joto la harakati za kisiasa nchini. Vijana hawa hawana budi kupewa mafunzo mazuri ya siasa ili wasiishi katika faraja.
Hivi sasa nchi inazingirwa na joto kali la baadhi ya vyama vya siasa kudai Katiba mpya. Viongozi wa vyama vya upinzani wanatia hamasa na tashititi kwa wananchi wakubali kuwapo kwa Katiba mpya kabla ya Uchaguzi Mkuu ujao wa 2025 na serikali inawekwa kiti moto juu ya jambo hili.
Serikali inatambua maana na umuhimu wa katiba. Lakini kwa sasa imesema suala hilo lisubiri kwa sababu inatekeleza mipango mkakati ya uchumi na maendeleo ya kijamii. Kauli hii ya serikali inaonekana kutokubalika kwa hivyo vyama vya siasa.
Hapa vijana katika vyama hivyo vya siasa wanapewa tashititi wapige mayowe ya kuwapo Katiba mpya na wapinge hoja ya serikali.
Vijana tafakuri inatakiwa kabla ya kupiga mayowe. Suala hili la Katiba mpya si geni, lilikuwapo. Ni serikali ndiyo iliyogharamia mchakato mzima wa Katiba mpya.
Mchakato wa katiba ulikwenda vizuri ulipokaribia ukingoni vyama vya upinzani vilitoka bungeni kupinga. Suala likasinyaa.
Suala lipo kiporo. Leo linakuja na kasi mpya. Serikali inaona kupanga ni kuchagua. Hata baadhi ya wanasiasa, wanasheria na wananchi wanakubaliana na serikali.
Katika jambo hili vijana msiyumbishwe na kudhani bila ya Katiba mpya kwa hivi sasa mambo ya nchi yatakwenda shaghalabaghala.
Mambo yataendeshwa kama yalivyopangwa. Matumaini na matarajio ya kisiasa, kiuchumi na kijamii yapo pale pale, chini ya jibu kazi iendelee.
Kinachofanywa na baadhi ya wanasiasa na wananchi ni kuwatia hofu vijana waishi kwa faraja, jambo ambalo si zuri.
Ukweli na usahihi mambo ni murua. Jambo la kuzingatia ni kuwa na nidhamu katika suala la kuwa na Katiba mapya. Jambo hili limo ndani ya uwezo wenu.
Naiomba jamii kulitazama suala hili na ujirani wake na vijana. Na viongozi wa vyama vya siasa na serikali kutafakari kwa kina na kutoka na jibu makini kwa vijana ili kuwa na subira. Katiba mpya itakuja na mikakati ya maendeleo iendelezwe.