Nimewahi kuandika makala kwenye safu hii nikifafanua baadhi ya faida ya taifa lolote kuwa na vijana wengi zaidi ya wazee.

Bara la Afrika lina wakazi wenye wastani mdogo zaidi wa umri kuliko mabara mengine yote; Niger ikiwa nchi inayoongoza Afrika na dunia.

Taarifa ya mwaka 2017 inaonyesha kuwa nusu ya raia wa nchi hiyo walikuwa na umri wa chini ya wastani wa miaka 15.3. Kwenye taarifa hiyo nchi iliyokuwa na wakazi wenye umri mkubwa zaidi ilikuwa Monaco, yenye wastani wa miaka 52.4. Monaco haina mamlaka kamili ya dola ambayo tunayafahamu kushikiliwa na nchi nyingi duniani, lakini inatambulika kuwa na mamlaka ya kutosha kuweza kujumuishwa kwenye takwimu mbalimbali.

Monaco ni moja ya nchi tajiri zaidi duniani, wakati Niger inaongoza kwa umaskini. Zinapochunguzwa takwimu za idadi ya watu kwa nchi kulinganishwa na utajiri wa nchi hizo tunaona kuwa, kwa kiasi fulani, umaskini wa nchi unaambatana na kiwango kikubwa zaidi cha kuzaa.

Katika orodha iliyoandaliwa mwaka 2017 Niger inashikilia nafasi ya mwisho kwa ukubwa wa kipato, wakati Monaco inaongoza.

Pamoja na kuwa wastani mdogo wa umri wa wakazi wa nchi unaweza kuleta manufaa, ni kweli pia kuwa ni nguvu inayoweza kuzua tafrani, maafa, na hasara ndani ya jamii.

Tatizo la mwanzo kabisa ni wingi wa watoto. Wazazi katika nchi maskini wana mzigo mkubwa zaidi wa kutunza watoto na kuwapa huduma muhimu kama chakula, matibabu, mavazi, na elimu. Ni mzigo mkubwa kwa wazazi maskini wakilinganishwa na wenzao wa nchi tajiri, ambao wana uwezo mkubwa wa fedha, lakini jukumu dogo la kutunza watoto.

Nje ya familia serikali inalazimika kuwekeza kwenye huduma za jamii kukidhi mahitaji ya hao watoto na vijana, elimu bora ikiwa ndiyo moja ya masuala ya msingi kabisa.

Kila serikali inayoingia madarakani katika kila nchi inaweka ahadi ya aina moja au nyingine ya kutengeneza ajira. Tishio kubwa kabisa la uwepo wa serikali madarakani ni kushindwa kutimiza ahadi ya kutoa ajira za kutosha kwa wapiga kura.

Tatizo linakuwa kubwa zaidi kwa nchi za Kiafrika zenye milipuko wa watoto na vijana. Ukosefu wa ajira una madhara mengi na unaongeza uwezekano wa kuongezeka kwa uhalifu, kupotea kwa amani, na kuongezeka kwa migongano ya kisiasa na hatimaye kuzorotesha usalama wa nchi hizi.

Inakadiriwa kuwa ikifikia mwaka 2055, kwa mujibu wa taarifa za Shirika la Maendeleo la Umoja wa Mataifa (UNDP), idadi ya vijana wa umri kati ya miaka 15 na 24 itafikia zaidi ya milioni 450. Aidha, kwa mujibu wa UNDP kati ya vijana milioni 12 waliofikia umri wa kusaka ajira barani Afrika mwaka 2015 ni milioni 3.1 tu kati yao ambao walipata ajira.

Maana yake ni kuwa kila mwaka mamilioni na mamilioni ya vijana watakuwa wanabaki bila ajira na kuongeza idadi ya raia ambao wanakosa uwezo wa kujilisha na kujitafutia huduma muhimu. Hili ni bomu ambalo likilipuka bila kuteguliwa litaongeza uzito wa orodha ya matatizo ambayo yanaandama bara letu.

Kwa kawaida, kwenye kila tatizo fursa pia huibuka. Kuna kikomo cha ajira mpya zinazoweza kuundwa na serikali, na kila serikali inaposhindwa kutoa ajira za kutosha inatoa fursa kwa vyama vya upinzani kuahidi kubuni mbinu bora zaidi za kutengeneza ajira.

Kwa kawaida, mchakato huu wa kushawishi nani ni bora zaidi wa kutengeneza ajira hauepuki mbinu za kila aina za kuwavuta na kuwagawa vijana wapiga kura wanaokabiliwa na ukosefu wa ajira wachague upande mmoja kati ya pande mbili au zaidi zinazopingana kwenye uwanja wa siasa.

Uhakika wa kuwapo kwa amani na utulivu katika nchi yoyote inayokabiliwa na wimbi kubwa la vijana wanaokosa ajira ni kwa serikali kuhakikisha kuwa inatengeneza ajira za kutosha. Mahitaji ya msingi ya binadamu yanatoshelezwa na kipato kinachotokana na ajira au shughuli nyingine ya kiuchumi. Mahitaji mengine yanaanza kuonekana ni muhimu binadamu anaposhiba tu. Raia mwenye njaa ni hatari zaidi kuliko anayeshiba.

Mengi ya matukio ambayo yanaitwa matukio ya upinzani siyo ya upinzani kwa maana yake halisi. Ni matukio ya watu wanaopata ghadhabu kwa kukosa kazi, na kukosa kipato kinachowawezesha kukabiliana na mahitaji ya msingi kabisa ya binadamu.

Mikakati ya nchi za Afrika kutengeneza ajira za kutosha au kuwawezesha vijana kujipatia riziki kwa kujiajiri wenyewe ni njia mojawapo ya uhakika ya kuimarisha amani na utulivu wa kudumu katika nchi hizo. Sambamba na hilo ni kuhakikisha kuwa vijana, ambao ndiyo kundi kubwa la raia, wanaingizwa kwenye mfumo rasmi wa uamuzi wa kisiasa, kiuchumi, na kijamii ili uamuzi huo uzingatie kwa kadiri itakavyowezekana mahitaji yao.

Mafanikio yatafikiwa kwa kuwapo viongozi ambao wanapima mahitaji na changamoto za vijana wa nchi zao na kuzingatia maslahi ya watoto ambao watashika nafasi zetu katika miongo ijayo.

Maoni: [email protected]