Narudia kutamka kwamba vijana ni nguvukazi mahali popote. Ni kundi kubwa kuliko la wazee katika kufanya kazi.
Ni kundi jipya lenye fikra na mawazo mapya, fahamu pevu, imara na jasiri katika kupambana na vikwazo vya uchumi au mambo ya dunia.
Ukombozi wa uchumi katika nchi yetu utapatikana kutoka kwa vijana wake walioelimika, walio wachapakazi, na wanaotumia juhudi na maarifa katika kupata maendeleo yao na ya taifa. Vijana wa aina hii tunao hapa nchini. Suala ni kujipanga.
Ukweli vijana wanaondoa dhana ya kuamini mvi ni alama ya hekima. “Fikra hii ilikuwa njema sana, lakini wakati wake umepita wala haurudi tena.
“Sasa kama mtu hakuelimika, mvi zake hazihesabiwi kuwa dalili ya hekima. Jambo lisilobadilika ni kuwa kila mzee anastahili heshima ya kila kijana siku zote.” (Shaaban Robert, Kusadikika uk. 10).
Kwa mantiki kama hii, taifa letu linatoa elimu kwa vijana wake, wapate maarifa, uwezo zaidi na hamu ya kufanya kazi. Vilevile kuwapa urithi ulio bora na tija kwa manufaa ya taifa. Taifa lenye vijana wasio na elimu ni taifa maskini.
Vijana wetu hawa wa karne ya 21 hapa nchini wanaelimishwa na kupata stadi mbalimbali kwa lengo la kulijenga na kuliendeleza taifa letu kiuchumi. Elimu yao ina zaidi ya hekima, stadi na kujitegemea. Hii ni falsafa pana katika mapinduzi ya Tanzania.
Kwa hiyo vijana wetu hawana budi kupambanua maana na mantiki ya elimu wanayopata, na kuwa ngangari katika mapambano dhidi ya vikorombwezo vya dunia, kana vile ufisadi, hila, haki na utawala wa sheria, kwani upo mgongano wa masilahi kati ya walionacho na wasionacho.
Vijana wa Tanzania ni juu yenu na kwa kweli ni wajibu wenu kutumia teknolojia na teknolojia ya habari na mawasiliano vema katika kukabiliana na mifumo ya siasa dhalimu na danganyifu. Aidha, kubaini hila na mbinu zinazotumiwa na baadhi ya watu katika matumizi ya utawala wa sheria.
Hekima itumike katika kuangalia na kupambanua kwa kina maana ya utamaduni mamboleo. Utamaduni huu unaleta mambo kinyume cha maadili ya taifa letu.
Kinyume cha taratibu za matumizi bora ya mali na rasilimali za nchi. Na unapumbaza vijana katika kuamini utamaduni wa ughaibuni ndio ustaarabu wetu!
Utamaduni huu kwa aina fulani unatumia teknolojia ya habari na mawasiliano kupitia vyombo vya habari na mitandao ya jamii kama vyombo vielelezo vya muziki pumbazifu, na kuacha makusudi kutoa elimu mafunzo kama vile kazi, kilimo n.k.
Tayari wapo baadhi ya vijana hawataki elimu na stadi mbalimbali ambazo zingewasaidia katika maisha yao; badala yake wanapalilia magugu ili utamaduni mamboleo ustawi vizuri. Huu ni ushamba, na ushamba lazima uondolewe. Ama sivyo tutaumia.
Elimu mnayopewa vijana ni chachu ya kuwawezesha kupanga mipango yenu na ya taifa letu. Taifa letu bado linahitaji wataalamu, mafundi stadi na wachapakazi ili liweze kutoka katika dimbwi la umaskini na kuingia katika bahari ya utajiri.
Umaskini hautoki kwa minenguo ya utamaduni mamboleo au kukumbatia utamaduni wa ughaibuni.
Unatoka kwa kuelewa na kuamini elimu ni hekima, kazi ni ufunguo wa maisha na umoja ni silaha ya mapambano dhidi ya vita ya uchumi.
Mapinduzi ya Tanzania ni pamoja na kupata elimu bora, kufanya kazi kwa juhudi na maarifa na kuukataa umaskini si jadi wala mila zetu za kudumu nazo. Lazima tuondoe dhana hizo na kuweka fikra za kimapinduzi katika kujenga taifa letu.
Vijana kisomo chenu kitoe mikondo ya umoja na utaifa, ari na uwezo wa kupenda kazi, kulinda na kutunza mali na rasilimali za Tanzania. Uthubutu ukitangulia, hakuna sababu za kuzuia Mapinduzi ya Tanzania.