Na Zulfa Mfinanga, Jamhuri Media, Arusha
Wiki ya Asasi za Kiraia (AZAKI) inatarajiwa kuanza kesho jijini Arusha ambapo vijana wanapata fursa ya kujadili umuhimu wa kushiriki katika mchakato wa kidemokrasia.
Akizungumza na waandishi wa habari leo jijini Arusha, Mkurugenzi Mtendaji wa HakiElimu John Kalage amesema kupitia kigoda cha vijana watajadili mambo makubwa mawili ambayo ni kushiriki kwenye mchakato wa kuomba nafasi ya uongozi pamoja na kupata viongozi ambao wanaamini wanaweza kuwaongoza.
“Kama tunavyojua tuna matukio makubwa matatu mbeleni ambayo ni mchakato wa kukusanya maoni ya Dira ya Maendeleo ya Taifa 2025/2050, uchaguzi wa Serikali za Mitaa pamoja na Uchaguzi Mkuu mwakani hivyo kupitia kigoda cha vijana watapata fursa ya kujadili umuhimu wao wa kushiriki mchakato wa kidemokrasia ndani na nje ya shule” alisema Kalage.
Mkurugenzi Mkazi wa Shirika la CBM International Nesia Mahenge ambaye pia ni Mwenyekiti wa Kamati ya maandalizi ya wiki ya AZAKI 2024 akizungumza na waandishi wa habari amesema kuwa kwa mwaka huu wiki hii ya AZAKI itawakutanisha takribani watu zaidi ya 600 na mashirika zaidi 400 ambapo Kauli Mbiu ni “Voice, Vision and Value” (Sauti, Dira na Thamani).
Kwa upande wake Mkurugenzi Mtendaji wa Foundation For Civil Society Justice Rutenge amesema sababu ya kuwa na Kauli Mbiu hiyo kwa mwaka huu ni kutokana na kwamba tupo katika kipindi muhimu cha Demokrasia.
Kwamba mwaka huu baadaye kuna uchaguzi wa Serikali za Mitaa, mchakato wa kukusanya maoni ya Dira ya Taifa ya Maendeleo 2025/2050 na mwakani Uchaguzi Mkuu wa Rais, Wabunge na Madiwani.
Kuhusu Dira ya Taifa Rutenge amebainisha kuwa pamoja na tofauti tulizo nazo kama Watanzania mwisho wa siku Dira ni maoni ya Watanzania.
Kwamba kwa upande wa Thamani amesema ni muhimu kuwa na Utekelezaji wa Dira ya Taifa ili kufikia Maendeleo ya Taifa ambapo amebainisha kuwa katika Wiki ya AZAKI Thamani itapatikana kwa kushirikiana katika nyanja mbalimbali.
“Kutakuwa na ushiriki wa Serikali, Sekta binafsi, Sekta ya Umma, mashirika mbalimbali ya ndani na kimataifa na wananchi,” amesema Rutenge.
Mkurugenzi wa Mtandao wa Jinsia Tanzania (TGNP), Lilian Liundi amesema jukwaa hilo litajikita zaidi kuhamasisha ushiriki wa makundi ya pembezoni hususani wanawake ikiwa ni pamoja na kusikia sauti zao kwani kundi hilo bado halijaweza kushiriki ipasavyo kwenye chaguzi mbalimbali kwani hadi sasa tafiti zinaonyesha 2% tu ya wanawake wanaongoza kwenye nafasi ya uongozi wa Serikali za Mitaa na 6% tu ya wanawake wanaongoza ngazi ya vitongoji.
Liundi amesema pia watakuwa na kampeni iliyopewa jina la “Mpe Riziki, Siyo Matusi” ambayo inalenga kutoa elimu kwa jamii kuheshimu jitihada zinazowafanywa na wanawake katika kujikwamua kiuchumi.
“Tukiangalia kwenye biashara nyingi ndogondogo utakuta kundi la wanawake ni kubwa kuliko makundi mengine, lakini wamekuwa wakikumbana na changamoto ya matusi na maudhi mbalimbali ambayo zinawakatisha tamaa, Sasa tumekuja na kampeni hii ili jamii iheshimu jitihada zao na kuwatia moyo Katika mapambano yao” alisema Liundi.
Wiki ya AZAKI inafanyika kwa mara sita tangu kuanzishwa kwake mwaka 2018 ambapo kesho Mgeni Rasmi anarajiwa kuwa Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais, Mipango na Uwekezaji Prof. Kitila Alexander Mkumbo (Mb.)