*Wabunge wawili CCM walipwa fidia Sh milioni 964 bado jengo lauzwa
*Zitto asema kalinunua Fida Hussein
*Ataka Katibu Mkuu Fedha ahojiwe

Wakati Rais Jakaya Kikwete amebadili Baraza la Mawaziri kutokana na shinikizo la Bunge, taarifa zimevuja kutoka serikalini kuwa kuna vigogo na watendaji wakuu wanaouza mali za umma kama zao.

Mawasiliano ya siri yaliyonaswa na Gazeti la JAMHURI yamebaini kuwa waliokabidhiwa jukumu la kulinda mali za umma – ama wameziachia au kwa makusudi – wameamua zitafunwe na wenye meno.

Baadhi ya mambo yanakuwa kama sinema. Desemba 2003 Jengo lililokuwa likitumiwa na wakala wa ukarabati wa magari ya Serikali (TMSC), lililopo katikati ya Jiji la Dar es Salaam, kwenye makutano ya Mtaa wa Jamhuri kando ya Barabara ya Ali Hassan Mwinyi, liliuzwa kwa aliyekuwa Mbunge wa Mvomero (CCM), Suleiman Saddiq.

Saddiq alinunua jengo hilo lililopo Kitalu Na 24 kupitia kampuni yake ya Saddiq Super Service Station (SSSS), baada ya kushinda zabuni akiwa na mshirika wake kibiashara, Richard Ndasa, ambaye naye ni Mbunge wa Sumve kupitia Chama Cha Mapinduzi (CCM).

Wawili hawa walishinda zabuni iliyotangazwa na Serikali, lakini baada ya kulipa asilimia 10 ya zabuni yaani Sh milioni 130, waliokuwa wafanyakazi wa TMSC waliamua kufungua kesi mahakamani. Kesi hiyo iliendelea na ilipofikia mwaka 2009, yaani miaka sita baadaye Ndasa na Saddiq waliamua kuihoji serikalini kulikoni jengo hilo hawakabidhiwi na hatima ya fedha zao walizotoa ilikuwa ipi.

Uchunguzi wa JAMHURI unaonyesha kuwa Wizara ya Fedha kupitia barua mbili – moja yenye kumbukumbu namba TYC/T/200/414/46 ya Aprili 14, 2009 na nyingine TYC/T/200/414/51 – ililiandikia Shirika Hodhi la Mashirika ya Serikali (CHC) kuwataka wasitishe uuzaji wa jengo hilo lenye ukubwa wa kuanzia mtaa mmoja hadi mtaa wa pili karibu na Jengo la Haidery Plaza eneo la Posta Mpya.

Wizara pia iliwataka CHC kuanzisha mazungumzo jinsi ya kuwarejeshea SSSS gharama walizotoa za Sh milioni 130 kama malipo ya awali na fidia ya usumbufu. Kampuni ya SSSS yenyewe ilitaka irejeshewe Sh bilioni 3.9 kwa biashara iliyopotea kati ya fedha hizo sh milioni 500 zikiwa za usumbufu. Mazungumzo kati ya CHC na SSSS yalikwama.

Ijumaa Juni 5, 2009 Bodi ya Wakurugenzi wa CHC ilikutana Dar es Salaam kuamua suala hilo bila mafanikio. Waliohudhuria kikao hicho ni Dk. Raphael Chegeni, Peter Bakilana, Methusela Mbajo, Shuma Kissege na Rosemary Tesha.

Mambo yalitulia hadi Mei 4, 2010 timu ya wataalamu wa Serikali ikiongozwa na Katibu Mkuu wa Wizara ya Fedha, Ramadhan Khijjah, aliyekuwa mwenyekiti wa kikao ilipokutana. Hapa ndipo ulipofanyika uamuzi wa kuitia kitanzi Serikali.

Wengine waliohudhuria kikao hiki ni Joyce Mapunjo, O. N. Assery, E. Mlaki, M. Kejo na J. W. Hellela. SSSS waliwakilishwa na Sulaiman A. Sadiq (MB) na Richard Ndasa (MB).

Ingawa taarifa ya CAG inasema haijulikani nani aliyewateua wajumbe wa Serikali kufanya kazi hii, taarifa hiyo inaongeza: “Hatimaye waliamua SSSS walipwe Sh 964,188,491.17 zinazohusisha Sh milioni 130 walizolipa kama malipo ya awali, Sh 334,188,491.17 zikiwa asilimia 20 ya riba tangu Desemba 2003 hadi Aprili 2010 na Sh milioni 500 kama fidia ya usumbufu.”

Kikao hicho kilimwamuru aliyekuwa Mwenyekiti wa kikao, Khijjah, baada ya kuwa ametia saini na Saddiq makubaliano ya malipo hayo, apeleke nakala ya makubaliano hayo kwa Waziri wa Fedha, Mustafa Mkulo (wakati huo), pia amshauri iwapo walipe fedha hizo au la.

Ikumbukwe kazi hizi zilipaswa kufanywa na CHC na Khijjah na Sadiq si waajiriwa wa CHC lakini wakaifanya kazi hiyo. Siku sita baadaye CHC iliwaandikia Wizara ya Fedha ikieleza majumuisho ya maafikiano yaliyofikiwa kwenye kikao cha Mei 4, 2010, wakimuomba Katibu Mkuu Khijjah awasilishe uamuzi wa kikao kwa Waziri wa Fedha. Hapa ndipo sanaa ilipotokea.

Barua hii ilikuwa inaandikwa kwa Katibu Mkuu wa Wizara ya Fedha, Khijjah, ambaye kwa bahati mbaya ndiye aliyekuwa Mwenyekiti wa kikao kilichopitisha malipo hayo. Pili kama zilivyo taratibu, Wizara ya Fedha ilipaswa kuwajibu CHC barua hiyo lakini hadi leo hawajawahi kupewa jibu la barua hiyo.

La mwisho na kubwa kuliko yote bila kupitia CHC, Wizara ya Fedha iliamua kuwaandikia SSSS hundi safi ya Sh 964,188,491.17 na waheshimiwa wawili waliotajwa ‘wakavuta mkwanja’.

Ndasa alipohojiwa na JAMHURI alikiri mlolongo huo kufuatwa, ila akasema: “Sisi tulifuata taratibu zote za zabuni na tukashinda, lakini baada ya kuona muda umepita na wafanyakazi wanaendelea kuvutana na Serikali, tukaona hakuna sababu ya kuvutana na Serikali ikitiliwa maanani kuwa sisi ni wabunge wa CCM.

“Serikali ilitwambia inataka kulitumia jengo hilo kujenga ofisi za Serikali na kupunguza gharama ya kupanga majengo mengine, sisi tukaona hili ni jambo jema. Lakini baadaye tukashangaa kusikia kuwa jengo hili limeuzwa kwa Fida Hussein kwa Sh bilioni 3. Tuliona huu ni uhuni mkubwa.

“Tuliondoka mimi na Murad (Saddiq) tukaenda kwa Fida Hussein na kumuuliza aliuziwaje jengo hilo, akasema yeye alilinunua mnadani. Kwamba baada ya wafanyakazi kushinda kesi, mahakama iliamuru liuzwe naye akawapo siku ya mnada akalinunua Sh bilioni tatu.

“Tuliona huu ni uhuni tukaenda hadi Wizara ya Fedha kumuona mtu wa TR (Msajili wa Hazina) anaitwa Masoud, huyu tulivyomuuliza akauma midomo akasema mara Serikali imekata rufaa, hata yeye haelewi vizuri kinachoendelea, tukabaki tunashangaa.”

Gazeti la JAMHURI ilipopiga simu za Murad (Saddiq) na Fida Hussein muda wote zilikuwa zinaita bila kupokewa.

Mbunge wa Kigoma Kaskazini (Chadema), Zitto Kabwe, alisema kilichotokea hakiweza kuvumilika kwani hii ni kuiba fedha za Serikali mchana kweupe.

“Fikiria serikali imelipa Sh milioni 964 kurejesha umiliki wa jengo, hata kama haikufuata taratibu, lakini pia mbali na fedha hizo kulipwa jengo limenadishwa na mahakama sasa analimiliki Fida Hussein si Serikali… huu ni wizi wa mchana lazima maafisa waliohusika watafutwe ili mali ya umma irejeshwe. Jengo lile lina thamani ya Sh bilioni 15, kiwanja kipo katikati ya Jiji la Dar es Salaam na ni kikubwa ajabu, wabunge hatutakubali lazima kieleweke,” alisema Zitto.

Hii ni moja ya kashfa zilizoibuliwa na CAG katika taarifa yake ya fedha, iliyowasilishwa katika kikao cha Bunge kilichomalizika Aprili na ripoti hiyo imeonyesha wizi na matukio makubwa ajabu ya matumizi mabaya ya fedha za umma.

Kutokana na hali hiyo, wabunge walitishia kupiga kura ya kutokuwa na imani na Waziri Mkuu Mizengo Pinda, kwa maana kuwa akiondoka Baraza la Mawaziri lingevunjika na hivyo mawaziri wanaotuhumiwa wakaondoka.

Zitto aliyeanzisha hoja hiyo, alipohojiwa na JAMHURI alisema: “Wabunge tumefanya kazi nzuri, lakini napenda kuwakumbusha kuwa wasijisahau. Moto huu uwe wa kudumu na mawaziri walioteuliwa wajue hawana ‘honey moon’ (fungate).

“Kikao kijacho watapambana na bajeti wakati mawaziri wanaposulubiwa. Wakajipange wachape kazi. Nawapongeza wabunge kwa kazi nzuri waliyofanya na nawataka waiendeleze,” amesema.