DAR ES SALAAM

Na Dennis Luambano

Vigogo 456 wakiwamo marais wastaafu na waliopo madarakani, mawaziri wakuu wa zamani, mabalozi, wauzaji wa dawa za kulevya, mabilionea, wasanii na wana michezo maarufu, wafalme, wanasiasa na viongozi waandamizi serikalini katika nchi 91 wamebainika kumiliki kwa siri ukwasi mkubwa katika maeneo mbalimbali ulimwenguni.

Kwa mujibu wa ripoti ya Taasisi ya Kimataifa ya Waandishi wa Habari za Uchunguzi (ICIJ) iliyotolewa Oktoba 3, mwaka huu, vigogo hao wanamiliki mali na fedha taslimu ambazo thamani yake kwa wastani ni zaidi ya Sh trilioni mbili za Tanzania.

Fedha hizo kwa mujibu wa ICIJ zinatokana na zao la vitendo haramu vya utakatishaji, ukwepaji kodi, rushwa na ufisadi na kama zingetumika hapa nchini zingenunua madawati 25,600,000 na kujenga madarasa 117,647 na kumaliza kabisa uhaba wa madarasa na madawati kwa shule za msingi na sekondari pia zingejenga vituo vya afya zaidi ya vitano na kupunguza adha kwa wananchi wanaotembea umbali mrefu katika baadhi ya maeneo kufuata huduma za afya.  

Kinyume chake, vigogo hao wamekwenda kuzificha katika nchi za Panama, Belize, Cyprus, Falme za Kiarabu, Singapore, Uswisi na Visiwa vya Virgin vya Uingereza, Marekani, Ufaransa na baadhi yao wakiendelea kuzitafuna kwa mambo ya anasa na starehe huku wananchi wao wakizidi kuogelea katika tope la umaskini wa kutisha. 

Miongoni mwa vigogo hao ni Rais wa Kenya, Uhuru Kenyatta, Rais wa Urusi, Vladimir Putin, mawaziri wakuu wa zamani wa Uingereza, Tony Blair na mkewe Claire na David Cameron, Waziri Mkuu wa Czech, Andrej Babis, Rais wa Azabajani, Ilham Aliyev na Mfalme wa Jordan, Abdullah Abdullah II bin Al-Hussein, Rais wa Gabon, Ali Bongo Ondimba na Rais wa Congo-Brazzaville, Denis Sassou – Nguesso.

Pamoja na mambo mengine, ripoti hiyo ya ICIJ inayoitwa Nyaraka za Pandora inaonyesha taarifa kutoka kwa kampuni zilizosajiliwa mataifa ya nje huku zikifichua namna vigogo hao akiwamo Mfalme Abdullah amekusanya kwa siri mali ya thamani ya wastani wa zaidi ya Sh bilioni 219.8 za Tanzania katika nchi za Uingereza na Marekani.

Kisha akanunua nyumba za kifahari katika eneo la Malibu huku akiendelea kununua nyumba nyingine 15 katika maeneo mengine yenye sheria dhaifu za ulipaji kodi katika visiwa vya Virgin vya Uingereza tangu alipochukua madaraka mwaka 1999.

Miongoni mwa nyumba hizo, zipo tatu za kifahari zenye thamani ya Sh bilioni 157 za Tanzania zilizopo fukwe za California, London na Ascot nchini Uingereza.

Ripoti hiyo ya ICIJ inasema licha ya kuendelea kujilimbikizia mali pia Mfalme Abdullah anashtumiwa kwa kusimamia serikali ya kidikteta na maandamano yamefanyika miaka ya hivi karibuni wakati wa kubana hali ya maisha na kuongezeka kwa kodi.

Kwa upande wao, mawakili wa Mfalme Abdullah wanasema mali zote zimenunuliwa na utajiri wake binafsi na anatumia kufadhili miradi kwa Wajordan.

Mawakili hao wanasema ni kawaida kwa watu maarufu duniani kununua mali kupitia kampuni za nje ya nchi kwa sababu za usiri na usalama.

Pia ripoti hiyo inaonyesha namna Blair na mkewe walivyookoa Sh milioni 926.7 za Tanzania kutokana na kukwepa kodi pindi waliponunua ofisi jijini London baada ya kununua kampuni inayomiliki jengo hilo.

Hata hivyo, hakuna taarifa zaidi kutoka ICIJ zinazofafanua zaidi kama Blair na mkewe wamekuwa wakificha utajiri wao huku risiti zikionyesha kwanini kodi haikulipwa wakati waliponunua nyumba yao yenye thamani ya Sh bilioni 20.25 za Tanzania.

Julai, 2017, Blair na mkewe Cherie wamenunua nyumba hiyo huko Marylebone baada ya kununua kampuni iliyofunguliwa katika maeneo yenye sheria dhaifu za ulipaji kodi iliyoimiliki.

Nyumba hiyo sasa ni makao ya kampuni ya ushauri wa kisheria ya mkewe Blair ambaye ni wakili na inazishauri serikali kadhaa sehemu mbalimbali duniani pia ina wakfu wake wa wanawake.

Blair mwenyewe anadai kuwa wauzaji waliwasisitiza wanunue nyumba hiyo kupitia kampuni zilizofunguliwa katika maeneo yenye sheria dhaifu za ukusanyaji kodi lakini anasema wamerudisha kwa sheria za Uingereza na watawajibika kulipa kodi baada ya kupata faida pindi watakapoiuza siku zijazo.

Risiti zilizovujishwa na ICIJ pia zinamhusisha Putin na mali za siri huko Monaco na zinaonyesha Babis alivyoshindwa kutangaza kampuni ya uwekezaji iliyofunguliwa katika maeneo yenye sheria dhaifu za ulipaji kodi iliyonunua majengo mawili ya kifahari kwa Sh bilioni 37.6 za Tanzania kusini mwa Ufaransa.

Ripoti hiyo ya ICIJ iliyoandaliwa kwa muda wa miaka miwili na jopo la waandishi wa habari zaidi ya 600 kutoka vyombo vya habari 150 vilivyopo sehemu mbalimbali duniani wamechunguza nyaraka zaidi ya milioni 11.9 kutoka kampuni 14 zinatoa huduma za kifedha na imefichua namna watu maarufu na mabilionea wanavyoanzisha kampuni kwa kufuata sheria na kununua mali kwa siri nchini Uingereza.

Pia ripoti hiyo inafichua wamiliki wa kampuni zingine 95,000 zilizofunguliwa katika maeneo yenye sheria dhaifu za kulipa kodi pindi wanaponunua vitu tofauti.

Katika hatua nyingine, ripoti hiyo inaonyesha jinsi Serikali ya Uingereza inavyo ‘puyanga’ kuanzisha orodha ya wamiliki wa mali za visiwa vya Virgin licha ya kuahidiwa mara kadhaa na kuna wasiwasi wanunuzi wa mali wanaficha shughuli za utakatishaji fedha.

Kwa upande wao, Aliyev na familia yake wanashutumiwa kwa kupora fedha na mali za nchi yao wenyewe ya Azerbeijan na kwa mujibu wa ripoti hiyo ni kwamba kwa kushirikiana na washirika wao wa karibu wamehusika kwa siri katika mikataba ya ununuzi wa mali nchini Uingereza yenye thamani ya zaidi ya Sh trilioni 1.2 za Tanzania.

Pia ripoti hiyo inaonyesha jinsi familia ya Aliyev inavyomiliki mali kwa siri nchini Uingereza kwa kutumia kampuni zilizofunguliwa katika maeneo yenye sheria dhaifu za ulipaji kodi licha kushutumiwa kwa ufisadi katika nchi hiyo kwa kununua nyumba 17 za kifahari na jengo la ofisi ya huko London kwa mtoto wake, Heyder Aliyev, mwenye umri wa miaka 11.

Jengo hilo lililopo Mayfair, London limenunuliwa na kampuni inayomilikiwa na rafiki wa familia ya Aliyev mwaka 2009 kisha mwaka 2010 umiliki wake ukahamishwa kwa Hedyer.

Kimsingi, ripoti hiyo inaichefua Uingereza kwa sababu Aliyev na washirika wake wamepata faida ya Sh bilioni 97.3 za Tanzania baada ya kuuza moja ya mali zao jijini London kwa Kampuni ya Crown Estate ambayo inatajwa kuwa ni mali ya Malikia Elizabeth.

Hata hivyo, ripoti hiyo inasema michakato yote hiyo katika risiti mbalimbali hazionyeshi makosa ya kisheria.

Fergus Shiel kutoka ICIJ anasema na kuongeza: “Haijawahi kutokea kitu chochote kwa kiwango hiki na inaonyesha kampuni zilizofunguliwa katika maeneo yenye sheria dhaifu za kulipa kodi zinavyowasaidia watu kuficha fedha. 

“Watu hao wanazitumia kampuni zilizofunguliwa maeneo yenye sheria dhaifu za kulipa kodi kununua mamilioni ya dola za Marekani katika nchi zingine na kutajirisha familia zao, marafiki zao, ndugu zao kwa gharama za jasho la raia wao wenyewe.”

Katika hatua nyingine, Uhuru na watu sita wa familia yake ya Kenyatta wanatajwa kumiliki kwa siri mtandao wa kampuni zilizofunguliwa katika maeneo yenye sheria dhaifu za ulipaji kodi. 

Uhuru na ndugu zake wanatajwa na ripoti ya ICIJ kwamba wanamiliki kwa siri kampuni 11 zenye thamani ya Sh bilioni 94.2 za Tanzania kwa muda mrefu sasa huko Panama na Visiwa vya Virgin.

Ripoti hiyo ya ICIJ inasema wakfu unaoitwa Varies ulianzishwa Panama mwaka 2003 na unamtaja mama yake Ngina Kenyatta kama mnufaika wa kwanza, naye Uhuru kama mnufaika wa pili ikiwa kifo kitatokea.

Hadi sasa, dhumuni la wakfu huo na thamani ya mali yake haijulikani kwa kuwa nchini Panama majina yanatafutwa kwa sababu wamiliki wa kweli wa mali wanajulikana tu na mawakili wao na si lazima waandikishe majina yao serikalini na mali zinaweza pia kuhamishwa bila malipo ya ushuru kwa mrithi.

Pia hakuna makadirio ya kuaminika ya thamani halisi ya mali ya familia ya Kenyatta lakini shughuli zake kubwa za kibiashara zinaonyesha kuwapo kampuni katika sekta za uchukuzi, bima, hoteli, kilimo, umiliki wa ardhi na vyombo vya habari nchini Kenya.

Nao wanachama na wafuasi watiifu wa Waziri Mkuu wa Pakistan, Imran Khan, mawaziri wake na familia zao wanatajwa na ripoti hiyo kumiliki kwa siri kampuni na mali zenye thamani ya mamilioni ya dola za Marekani 

Pia kampuni ya sheria iliyoanzishwa na Rais Nicos Anastasiades wa Cyprus inatoa wamiliki feki kwa minajili ya kumficha mmiliki halisi baada ya kufunguliwa katika maeneo yenye sheria dhaifu za ukusanyaji kodi huku Rais wa Ukraine, Volodymyr Zelensky, naye anatajwa kuhamisha hisa zake katika kampuni zilizofunguliwa katika maeneo kama hayo kabla tu ya kushinda uchaguzi wa mwaka 2019.

Naye Rais wa Ecuador, Guillermo Lasso, anatajwa na ripoti hiyo kuwa amebadilishiwa wakfu na mfanyakazi wa benki nchini Panama na kumsaidia kulipa malipo ya kila mwezi kwa wanafamilia wake wa karibu na mali iliyopo kusini mwa Dakota nchini Marekani.