Utapeli wa kutisha umefanywa na uongozi wa Manispaa ya Temeke, Dar es Salaam, juu ya uuzaji viwanja katika eneo la Gezaulole.
Imebainika kwamba uongozi wa Manispaa hiyo, kwa makusudi, umetumia majina ya baadhi ya watu na familia maarufu nchini, kujitwalia viwanja kwa kisingizio kwamba watu hao wameviomba.
Hatua hiyo ya utapeli imewasaidia kujenga hoja kwenye ugawaji viwanja, na hivyo kwenye mgawo vimetolewa viwanja vingi kwa waombaji, lakini ukweli ni kwamba mwisho wa siku vimeishia mikononi mwa ‘wajanja’ wachache, ambao sasa wanaviuza kwa bei ghali.
Baadhi ya majina ya watu wanaohusishwa kwenye utapeli huo ni vigogo wa Ikulu, wizara, Chama Cha Mapinduzi (CCM), wabunge, Ofisi ya Makamu wa Rais, Ofisi ya Waziri Mkuu, wakuu wa mikoa na wilaya, marais wastaafu na wafanyabiashara wenye ukwasi mkubwa.
Viwanja zaidi ya 1,800 viliidhinishwa na Serikali kuuzwa kwa wananchi katika eneo la Gezaulole, nje kidogo ya jiji la Dar es Salaam, kwa ajili ya ujenzi wa mji mpya, lakini idadi kubwa ya wenyeji wa eneo hilo haimo kwenye mgawo huo.
Habari zinasema kigogo mmoja wa Halmashauri ya Manispaa ya Temeke amejitwalia viwanja zaidi ya 100 ambavyo sasa anaviuza kati ya Sh milioni 3.5 na Sh 6.5 kwa kiwanja, kutegemeana na hali ya kiwanja. Anafanya biashara hiyo kupitia kwa dalali (jina tunalo).
Uchunguzi umebaini kwamba kila anayenunua kiwanja kwa Sh milioni 3.5 analazimika kwenda kukilipia tena Sh milioni tano, na anayenunua kwa Sh milioni 6.5 analazimika kwenda kukilipia tena Sh milioni 10 kwenye akaunti ya Halmashauri ya Manispaa ya Temeke kupitia Benki ya Uwekezaji Tanzania (TIB).
JAMHURI imefanikiwa kupata nyaraka zenye majina ya orodha ya mgawo wa viwanja hivyo. Wakizungumza na JAMHURI kwa sharti la kutotajwa majina, walisema wananchi walionyimwa viwanja kutokana na kutokuwa kwenye orodha ya vigogo waliolengwa, ni zaidi ya nusu ya idadi ya viwanja vilivyogawanywa ambapo kwa sasa vimerudishwa sokoni na kuchangamkiwa na matajiri.
“Unajua viongozi hao hawakuhitaji viwanja kwa dhamira ya kujenga nyumba au kuviendeleza, ndiyo maana sasa wanaviuza kwa kasi na kugawana fedha na madalali wanaowatumia kutafuta wateja wanaomiminika kila siku katike eneo la Gezaulole kununua viwanja hivyo,” kimesema chanzo chetu cha habari.
“Zaidi ya nusu ya wenyeji wa Gezaulole, yaani wananchi wa kawaida walioomba kugawiwa viwanja katika eneo hilo hawakupewa, badala yake uongozi wa Manispaa ya Temeke ulijali kuwagawia viongozi wengi wa Serikali na chama… hii ndiyo Tanzania yetu,” kimelalamika chanzo hicho.
Meya wa Halmashauri ya Manispaa ya Temeke, Mabaad Hoja, alipoulizwa na JAMHURI kwa njia ya simu, alikiri kuwapo kwa zoezi la uuzaji viwanja katika eneo la Gezaulole, lakini akakana tuhuma za viongozi akiwamo yeye kumiliki viwanja vingi na kutumia madalali kuviuza kwa matajiri.
Hoja pia alikana kuhusika na tuhuma kwamba viongozi na watumishi wa Serikali na CCM wamependelewa katika ugawaji wa viwanja katika eneo hilo.
Sehemu ya mahojiano hayo ya JAMHURI na Hoja ni kama ifuatavyo:
JAMHURI: Kuna malalamiko kutoka kwa wananchi kuwa umetumia majina ya ndugu zako na watu maarufu kujigawia viwanja vingi katika eneo la Gezaulole, na kwamba kwa sasa umewapatia madalali fomu za viwanja zaidi ya 100 kwa ajili ya kukusaidia kuviuza kwa matajiri, unasemaje kuhusu hilo?
Hoja: Du! Hiyo mpya sasa, hao wanatumia jina langu vibaya. Hao labda wamechukua kwa utaratibu wa kawaida, mimi sihusiki hapo.
JAMHURI: Unasemaje kuhusu malalamiko ya wananchi dhidi yako kwamba ulitumia cheo chako kufanya upendeleo wa kugawa viwanja vingi zaidi kwa viongozi na watumishi wa Serikali na CCM, huku ukiyatupilia mbali maombi ya wananchi wa kawaida?
Hoja: Si sahihi, ni kweli viongozi wamepata viwanja lakini watu wengi walioomba, hawawezi kupata wote, waliopata wamepata kwa utaratibu usio na upendeleo.
JAMHURI: Unadhani ni kwanini watu wengi waliopata viwanja hivyo wameanza kuviuza kwa matajiri?
Hoja: Mimi sijui kabisa.
JAMHURI: Mchanganuo wa bei za viwanja vinavyouzwa huko Gezaulole ukoje hasa?
Hoja: Hilo kamuulize Afisa Mtendaji na Afisa Ardhi.