Wafanyakazi wawili miongoni mwa watano waliofukuzwa kazi na Bodi ya Uongozi ya Benki ya Ushirika Kilimanjaro (KCBL) wametoweka na kutelekeza mali za mabilioni ya fedha.

Mali hizo ni pamoja na nyumba za kifahari, magari pamoja na viwanja. Ni mali ambazo kwa sasa zipo chini ya ulinzi wa vyombo vya dola kwa ajili ya uchunguzi.

Wafanyakazi hao ni aliyekuwa Meneja Mkuu wa benki hiyo, Joseph Kingazi na aliyekuwa Meneja Mikopo wa benki hiyo, Ombeni Masaidi, ambao mpaka sasa wanadaiwa ‘kujificha’ kusikojulikana.

Kwa mujibu wa taarifa kwa umma iliyotolewa na Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa (Takukuru) Mkoa wa Kilimanjaro, mali za watuhumiwa hao zimebainika kuwapo katika maeneo mbalimbali katika mikoa ya Tanga, Arusha na Kilimanjaro.

Taasisi hiyo imetoa wito kwa wananchi kutojihushisha kwa namna yoyote na mali za watuhumiwa hao na kuonya kuwa atakayefanya hivyo atakabiliwa na makosa ya utakatishaji fedha chini ya kifungu cha 12 cha Sheria ya Utakatishaji Fedha ya mwaka 2016.

Kulingana na taarifa ya Takukuru, mali zinazodaiwa kumilikiwa na Kingazi ni pamoja na nyumba za kifahari zilizopo katika viwanja namba 204, kitalu GG na namba 345 kitalu GG Barabara ya Arusha, nyumba mbili zilizopo eneo la Olasiti jijini Arusha na nyingine ya kifahari iliyopo eneo la Kwa-Mrefu jijini Arusha.

Katika mji wa Moshi, Kingazi anadaiwa kumiliki mali zilizopo katika viwanja namba 437 kitalu HHHA, section III katika Mtaa wa Kambaita, Manispaa ya Moshi na katika Wilaya ya Siha anamiliki viwanja vitano ambavyo ni chenye namba 1312 kitalu A Ngarenairobi, namba 1998 kitalu B, namba 925  kitalu A, namba 908 kitalu A na kiwanja namba 1025 kitalu A.

Mali nyingine zinazodaiwa kumilikiwa na Kingazi kwa mujibu wa Takukuru ni kiwanja namba 1 na 2 kitalu N kilichopo Wilaya ya Same pamoja na nyumba moja iliyopo eneo la Sony Mponde, Wilaya ya Lushoto, mkoani Tanga.

Kuhusu magari yanayodaiwa kumilikiwa na Kingazi ni lenye namba za usajili T 706 DCL aina ya Toyota Spacio, T 795 AWR Suzuki Escudo, T 936 CMC aina ya Volkswagen Touran, T 604 DKY Toyota IST na pikipiki moja yenye namba za usjaili MCA490 AAZ.

Kwa upande wa aliyekuwa Meneja Mikopo wa benki hiyo, Ombeni Masaidi, Takukuru imetoa orodha ya mali anazodaiwa kumiliki na ambazo zinahusishwa na matokeo ya uhalifu. Mali hizo ni pamoja na jumba la kifahari lililopo katika kiwanja namba 927 kitalu A, Wilaya ya Siha.

Mali nyingine zimetajwa kuwa ni viwanja viwili, kimoja katika namba 1313 kitalu A kilichopo Ngarenairobi na kingine namba 2005 kitalu B kilichopo Wilaya ya Siha pamoja na magari yenye namba za usajili T 167 DBD Toyota Rummi na T 759 DDM Toyota Virtz.

Kutokana na watuhumiwa hao kutoweka katika makazi yao mkoani Kilimanjaro, Takukuru imetoa wito kwa wananchi kutoa taarifa kwa taasisi hiyo au vituo vya polisi ili waweze kukamatwa na hatua za kisheria zichukuliwe dhidi yao.

Kusakwa kwa watumishi hao na Takukuru kunakuja siku chache baada ya Bodi ya Wakurugenzi ya Benki ya KCBL kuwafukuza kazi wafanyakazi hao kutokana na tuhuma za ufisadi wa mabilioni ya fedha mali ya benki hiyo.

Mbali na Kingazi na mwenzake huyo, wengine waliofukuzwa kazi na tayari wamekwisha kuhojiwa na Takukuru ni pamoja na Asha Kisega kutoka Idara ya Mikopo (KCBL), Doe Mashinga aliyekuwa Mtunza Fedha wa benki hiyo na Ukundi Mmochi aliyekuwa Katibu Muhtasi wa meneja mkuu.

Kabla ya kufukuzwa kazi maofisa hao walipewa barua za kusimamishwa kazi kupisha uchunguzi wa tuhuma za ufisadi na baada ya uchunguzi kukamilika wakapewa barua za kufukuzwa.

Hatua ya kufukuzwa kazi kwa maofisa hao inahusishwa pia na malalamiko ya siku nyingi kutoka kwa baadhi ya wanahisa wa benki hiyo juu ya mwenendo usioridhisha wa benki hiyo uliodaiwa kutokana na usimamizi mbovu.

Mwenyekiti wa Bodi ya Uongozi wa KCBL, Gervas Machimu, pamoja na kukiri kufukuzwa kazi kwa wafanyakazi hao, hakuwa tayari kuingia kwa undani kuhusu tuhuma zilizochangia benki hiyo kuwafuta kazi.

“Ni kweli kama ulivyoona hilo tangazo lakini hili suala ni zito sana, si vizuri kuzungumza kwenye simu, naomba nitakutafuta tuzungumze ana kwa ana,” alisema mwenyekiti huyo.

Mmoja wa wajumbe wa bodi hiyo aliyezungumza kwa sharti la kutotaka kutajwa jina lake ameliambia JAMHURI  kuwa maofisa hao wamefukuzwa kazi kutokana na kuhusika kwa namna moja ama nyingine katika ufisadi wa mabilioni ya fedha ambao umeifanya benki hiyo kuyumba mara kwa mara.

Mjumbe huyo ametaja eneo ambalo limeiweka pabaya benki hiyo na kufikia hatua ya kusimamisha utoaji wa huduma ni Idara ya Mikopo, ambapo maofisa hao wanatuhumiwa kujihusisha na utoaji wa mikopo usiozingatia taratibu za benki.

Ametolea mfano wa Vyama vya Ushirika wa Mazao (AMCOS) vipatavyo 18 pamoja na Chama Kikuu cha Ushirika cha Same (VUASU) ambavyo vilivuka na deni la zaidi ya Sh bilioni 1.173 katika msimu wa 2016/2017, kwamba hadi sasa vyama hivyo vimeshindwa kurejesha mkopo huo.

“Kwa utaratibu chama kinapewa fedha kulingana na kiwango cha kahawa wanayokusanya lakini vyama vingi vimepewa pesa nyingi isiyoendana na kiwango cha kahawa wanayoratajia kukusanya na matokeo yake wameshindwa kuzirejesha mpaka sasa,” amesema.

JAMHURI limeona orodha ya vyama hivyo na kiasi cha mkopo walichopewa na kiasi cha fedha iliyorejeshwa KCBL na kati ya Sh bilioni 1.9 zilizotolewa kwa vyama hivyo katika msimu huo, Sh milioni 700 tu ndizo zilizorejeshwa hadi kufikia Juni 30, 2017 huku Sh 1,173,869,049 zikiwa mikononi mwa vyama hivyo hadi sasa.

Vyama hivyo vya ushirika wa mazao ni miongoni mwa wanahisa 245 wa benki hiyo wakiwamo pia watu binafsi 307 pamoja na vyama vya Akiba na Mikopo (SACCOS) na ilikuwa ikihudumia wilaya sita za Mkoa wa Kilimanjaro.

Benki hiyo inayomilikiwa kwa asilimia 69 na Chama Kikuu cha Ushirika Kilimanjaro (KNCU) ilianzishwa mwaka 1996 ikiwa na lengo la kuwakwamua kiuchumi wakulima wa zao la kahawa mkoani humo kwa kunufaika na mikopo yenye riba nafuu kupitia vyama vyao vya msingi vya ushirika.

Januari mwaka jana benki hiyo ilikuwa miongoni mwa benki tatu zilizopewa miezi sita na Benki Kuu ya Tanzania (BoT) kutimiza matakwa ya kisheria ya kuwa na mtaji wa Sh bilioni tano lakini mpaka sasa benki hiyo imeshindwa kutimiza matakwa hayo.

Baada ya tangazo hilo la BoT, KNCU ilitangaza kuuza shamba lake la kahawa la Lerongo lililopo Wilaya ya Hai likiwa na ukubwa wa ekari 581 kwa ajili ya kuinasua benki hiyo dhidi ya ‘rungu’ la BoT kabla ya Waziri Mkuu Kassim Majaliwa kuzuia uuzwaji wa shamba hilo.