DAR ES SALAAM
NA DENNIS LUAMBANO
Vigogo watano wa Halmashauri ya Jiji la Dar es Salaam wamesimamishwa kazi kupisha uchunguzi wa ufisadi wa mamilioni ya shilingi.
Tayari Ofisi ya Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali (CAG) imeanza kufanya ukaguzi huo maalumu kubaini upotevu wa fedha hizo za mapato yanayokusanywa kupitia mashine za POS.
Akizungumza na Gazeti la JAMHURI ofisini kwake, Mkurugenzi wa Jiji la Dar es Salaam, Jumanne Shauri, amethibitisha kuwapo kwa ukaguzi huo.
Waliosimamishwa kupisha ukaguzi ni Mweka Hazina, Tulusuba Kamalamo; Mhasibu Mkuu wa Mapato, James Bangu; Msaidizi Mkuu wa Mhasibu wa Mapato, Deogratius Rutataza; Mtunza Fedha Mkuu, Abdala Mlwale, na Ofisa Masoko Mkuu, Burhani Kaisi.
Uchunguzi huo umekuja baada ya Waziri wa Nchi, Ofisi ya Waziri Mkuu Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa, Ummy Mwalimu, kutilia shaka ukusanyaji mapato wa robo ya kwanza ya mwaka 2021/2022 ambayo ni asilimia 26 ya lengo.
“Ni kweli kuna ukaguzi ila wanaochunguza siyo TAMISEMI, ni CAG na hadi sasa hivi hakuna kiasi cha fedha kilichotajwa kupotea,” amesema Shauri.
Anasema tuhuma zilizopo si za wizi, bali ni kutaka kujua kwanini makusanyo yamegota asilimia 26. Shauri hakutaka taarifa hizo za ukaguzi zichapishwe kwenye vyombo vya habari.
“Kwa kuwa kuna ukaguzi ndiyo maana hao watumishi wa jiji ikabidi wasimamishwe ili uchunguzi ufanyike, kwa sababu isingewezekana wao wabaki ofisini wakati uchunguzi unaendelea.
“Ukaguzi ukishamalizika watarudi ofisini kuendelea na majukumu yao. Tumwache CAG afanye kazi yake na hata akimaliza ukaguzi huo ataandika ripoti yake ambayo itapatikana kuanzia mwakani, hebu tusubiri kwanza,” amesema.
Taarifa zilizopatikana kutoka kwa chanzo chetu cha habari ndani ya Idara ya Fedha na Biashara ya Halmashauri ya Jiji la Dar es Salaam zinasema vigogo hao walipewa barua za kusimamishwa kazi Novemba 4, mwaka huu.
“Hizo barua za kuwasimamisha zimetoka TAMISEMI, kwa sababu kuna special audit. Barua zimetoka masjala ya siri na wakakabidhiwa Alhamisi jioni (Novemba 4, mwaka huu) kisha wote wakajifungia ofisini hadi saa nne usiku kuzijadili.
“Mashine za POS zilianza kutumika mwaka 2004, kwa maana ya kukusanya mapato kwa mfumo au kwa kutumia njia ya kielektroniki tofauti na ule wa zamani wa kutumia ma-cashier.
“Jiji ni kama kuna mtandao wa hao watu ndiyo maana TAMISEMI ikaunda timu ya kuchunguza. Hizo mashine za POS ziko zaidi ya 50 na tuhuma za upotevu wa mapato zimeibuka kwa sababu kuna ushirikiano kati ya vijana wanaokusanya hizo fedha na watu wa IT.
“Kwa mfano, inawezekana zikakusanywa Sh laki tano kwa siku, lakini katika mfumo wa hesabu za makusanyo kule ofisini ikaonekana kwamba kilichokusanywa ni Sh elfu hamsini tu.”
Pia chanzo hicho kinasema vijana wanaokusanya mapato hayo kwa kutumia mashine hizo wanapewa mikataba mifupi ya ajira, sababu inayoweza kuwashawishi kufanya vitendo vya hujuma ya mapato.
“Ni sahihi kabisa kufanya ukaguzi huo kwa sababu vijana wanaokusanya mapato wanapewa mikataba ya ajira ya mwaka mmoja au miwili, ndiyo maana watu wa IT ni rahisi kuwamudu,” kinasema chanzo chetu.
Vijana wanaotumia mashine hizo kukusanya mapato wamekuwa wakihojiwa katika jengo la DMDP lililopo Mnazi Mmoja, Dar es Salaam.
Katika hatua nyingine, chanzo hicho kinasema tuhuma hizo zinaibuka kwa kuwa mtandao idarani hapo umeota mizizi, kwa kuwa kuna baadhi ya watumishi wamedumu muda mrefu katika nafasi zao.
“Kwa kawaida idara yoyote ile inayohusu fedha lazima kuwe na rotation (mzunguko) ya watumishi katika nafasi zao.
Dosari nyingine inayotajwa ni kwa baadhi ya watumishi wa idara, hasa zinazohusu fedha na mipango, kukaa sehemu moja kwa kipindi kirefu sana.
Kunatolewa mfano kuwa wapo baadhi ya watumishi waliodumu kwenye nafasi hizo tangu Charles Keenja akiwa Mwenyekiti wa Tume ya Jiji la Dar es Salaam miaka ya 2000 hadi leo.
Hii ni mara ya kwanza kwa CAG mwenyewe kufanya ukaguzi katika Jiji la Dar es Salaam.
“Kwa kawaida kuna wakaguzi wa nje wanaotoka ofisi ya CAG na wanakuja mara mbili, ikiwamo katikati na kabla ya mwaka wa fedha wa serikali haujafungwa na kuna wakaguzi wa ndani wanaokagua kila siku. Lakini ukaguzi huu maalumu ni mara ya kwanza,” kinasema chanzo chetu.
Mwezi uliopita Waziri Ummy alishitushwa na mapato madogo ya jiji hilo lenye vyanzo na ukwasi mkubwa. Lakini katika hali isiyo ya kawaida, ilibainika kuwa Dar es Salaam ilizidiwa mapato na baadhi ya halmashauri zisizo na vyanzo kama vyake.
“Zamani wakati Mkurugenzi akiwa Isaya walau tumewahi kwa wastani kufikia asilimia 72 za makusanyo kwa mwaka mzima wa fedha, lakini kabla na baada ya hapo tumekuwa tunafikia asilimia 50 au 60.
“Kwa kawaida ili mfikie malengo mnatakiwa kukusanya kwa asilimia 100 na mmekosa sana basi msishuke chini ya asilimia 80. Sasa jiulize, mbona Jiji la Dar lina vyanzo vingi vya mapato lakini makusanyo yake ni hafifu?
“Jibu la swali hilo ni rahisi tu kwamba kuna baadhi ya watu wanafanya kazi kwa mazoea na hawawajibiki ipasavyo na hawawajibishwi. Fikiria Dar es Salaam kuna biashara ngapi kubwa au kuna wafanyabiashara wangapi wakubwa au kuna kampuni ngapi kubwa zinapatikana hapa?”
“Wengi tulidhani kwamba baada ya jiji kuvunjwa na kuhamishiwa katika Manispaa ya Ilala mapato yangeongezeka, lakini imekuwa kinyume. Makusanyo yamepungua,” kinasema chanzo chetu.