Kwa muda mrefu katika Tanzania yetu, viongozi wengi wameyaangalia magazeti kama vyombo vya uzushi na uchochezi. Mtu mmoja atashauri suala fulani lililoandikwa gazetini lifuatiliwe.
Lakini kiongozi atasema kwamba suala hilo lisifuatiliwe kwa kuwa hayo ni mambo ya magazetini yasiyo na ukweli. Hali hiyo imechangia uozo ambao Rais Dk. John Pombe Magufuli amekiri kwamba ameukuta alipoingia madarakani.
Magazeti katika nchi hii yamefanya kazi kubwa ya kufichua maovu na kubainisha kero za wananchi. Lakini viongozi hawakujali. Si mambo ya magazeti tu?
Kwa hiyo, hatua ya majuzi ya Rais Magufuli ya kulisifia gazeti la JAMHURI kwa mchango wake wa kufichua maovu, haikuwafurahisha na kuwatia moyo watu wa JAMHURI tu, bali tasnia yote ya habari imefurahishwa na kutiwa moyo.
Kuna wakati katika nchi hii yetu, Rais aliyemaliza muda wake aliendelea kusifiwa kwa kuyavumilia magazeti yaliyokuwa yakiandika kweli tupu, yaliyoonekana yanaandika mambo ya uchochezi na ya kupotosha watu. Kwa hiyo, yale yote yaliyokuwa yakiandikwa magazetini hakuna aliyeyafanyia kazi.
Tukafikishwa mahali tunapoanza kujenga upya nchi yetu baada ya kuharibiwa na watu wachache kiasi cha kutisha. Hapana shaka Serikali ya Rais Magufuli itaendelea kuyafanyia kazi masuala yote mazito yanayoandikwa magazetini.
Leo napenda nizungumzie vifungu mbalimbali vya Katiba ya Jamhuri ya Muungano vinavyochefua wakati unaposoma Katiba yetu.
Kama tujuavyo, Katiba ni mwongozo wa utawala. Ni mkusanyiko wa sheria kuu za nchi. Ni sheria mama. Katiba ya nchi yoyote isiponyooka au ikipindisha mambo huhatarisha umoja wa taifa. Lakini katiba ya nchi husomwa pia na wageni. Wageni wakiona mambo yanavyowachanganya katika katiba ya nchi fulani, si kama tu wanashangaa bali pia hujaribu kuamini kwamba hiyo ilitungwa na watu waliokosa ujuzi wa kutunga katiba.
Lakini kwa upande wa Katiba ya nchi yetu, si kweli kwamba ilitungwa na watu waliokosa ujuzi. Ilitungwa na watu wenye ujuzi lakini waliotawaliwa na ubinafsi. Waliweka mbele maslahi yao badala ya kuweka mbele maslahi ya Taifa.
Hao walikuwa wabunge wa Chama Cha Mapinduzi (CCM) ambao hawakutaka mfumo wa vyama vingi. Wahisani walipohusisha misaada yao na mfumo wa vyama vingi, wabunge wa CCM wakaamua kutunga Katiba iliyowekea vikwazo vyama vya upinzani na watu wasio wanachama wa vyama vya siasa. Matokeo yake tuna vifungu mbalimbali vya Katiba vinavyochefua.
Angalia watu binafsi walivyozuiwa kugombea uchaguzi! Kwa kuanzia, Katiba inaleta picha kwamba kila raia ana uhuru wa kushiriki masuala ya siasa bila vikwazo.
Ibara ya 20 (1) ya Katiba inasema kwamba “Kila mtu anao uhuru wa kukutana na watu wengine kwa hiari yake na kwa amani, kuchanganyika, kushirikiana na watu wengine, na kwa ajili hiyo kutoa mawazo yake hadharani na kuanzisha na kujiunga na vyama au mashirika.”
Halafu ibara ya 20 (4) inasema “Itakuwa ni marufuku kwa mtu yeyote kulazimishwa kujiunga na chama chochote.”
Lakini ibara ya 39 (1) na 67 (1) zinazozungumzia uchaguzi wa Rais na wa mbunge zinasema kwamba “Mtu yeyote atakuwa na sifa za kustahili kuchaguliwa kuwa rais au mbunge endapo ni mwanachama na ni mgombea aliyependekezwa na chama cha siasa.”
Hii ni kusema kwamba kila mtu analazimishwa kujiunga na chama cha siasa ambako ni kukiuka ibara ya 20 (4) inayosema kwamba “Itakuwa ni marufuku kwa mtu yeyote kulazimishwa kujiunga na chama chochote.”
Hii inachefua. Kama tutakavyokumbuka, Mchungaji Christopher Mtikila alipinga mahakamani kitendo cha watu binafsi kuzuiwa kugombea uchaguzi na mara zote alishinda kesi. Lakini utawala wa Tanzania unaojipambanua kuwa ni utawala wa sheria uliendelea kukaidi sheria katika kulinda maslahi ya watu binafsi.
Kuhusu madaraka ya Mahakama ya Tanzania ibara ya 107 A (1) ya Katiba ya Tanzania inasema kwamba “Mamlaka yenye kauli ya mwisho ya utoaji haki katika Jamhuri ya Muungano itakuwa ni Mahakama.”
Lakini, ibara ya 74 (12) ya Katiba hiyo hiyo inasema kwamba “Hakuna Mahakama yoyote itakayokuwa na mamlaka ya kuchunguza jambo lolote lililotendwa na Tume ya Uchaguzi.”
Hii ni kusema kwamba chombo chenye kauli ya mwisho ya utoaji haki katika Jamhuri ya Muungano itakuwa ni Tume ya Uchaguzi.
Na kuhusu uchaguzi wa Rais ibara ya 41 (7) ya Katiba inasema kwamba “Iwapo mgombea wa kiti cha Rais ametangazwa na Tume ya Uchaguzi kwamba amechaguliwa kuwa Rais, basi hakuna Mahakama yoyote itakayokuwa na mamlaka ya kuchunguza kuchaguliwa kwake.”
Hapa tena, Mahakama ya Tanzania imenyang’anywa madaraka yake na Tume ya Uchaguzi.”
Kwa jumla, ibara hii si tu kwamba inachefua, bali pia inathibitisha madai ya siku nyingi kwamba Tume ya Uchaguzi imepewa kibali cha kuiba kura kwa niaba ya chama tawala ili Rais wa Tanzania wakati wote atokane na CCM.
Hata waangalizi wa uchaguzi wa Umoja wa Ulaya wanajua kuwa Watanzania hawana uchaguzi huru na wa haki. Ndiyo maana waliondoka Tanzania wakisisitiza umuhimu wa matokeo ya uchaguzi kuhojiwa mahakamani.
Hivi, Tume ya Uchaguzi inapambana vipi na Edward Lowassa anayeendelea kudai kuwa alishinda uchaguzi wa mwaka jana wakati sheria inamkataza kwenda mahakamani kutafuta haki? Akatafute haki mwituni?
Halafu kuna ibara ya 59 B (4) ya Katiba inayosema kwamba “Katika kutekeleza mamlaka yake, Mkurugenzi wa Mashitaka atakuwa huru na hataingiliwa na mtu yeyote na mamlaka yoyote.”
Ibara hii inampa Mkurugenzi wa Mashitaka madaraka makubwa mno ya kuonea watu, kuvuruga haki na kupokea rushwa.
Kwa kweli, nafasi haitoshi kueleza kila kitu kinachohusiana na ubovu wa Katiba ya Tanzania.
Ni vyema Rais Magufuli akafufua mchakato wa mabadiliko ya Katiba ili Tanzania iwe na Katiba inayolinda umoja, amani na haki. Ni bora tukaondokana na Katiba inayochefua.