Idadi ya vifo kutokana na mashambulizi ya angani ya Israel huko Gaza imefikia 77, saa chache baada ya kutangazwa kwa makubaliano ya kusitisha mapigano na kuwaachia mateka.
Wizara ya Afya ya Gaza imesema watu 81 wameuawa katika kipindi cha saa 24 zilizopita na karibu 188 wamejeruhiwa. Shirika la huduma za dharura la Kipalestina limesema watu 77 kati ya hao waliuawa tangu makubaliano ya kusitisha mapigano yalipotangazwa.
Makubaliano hayo ya kusitisha mapigano yalifikiwa jana kwa juhudi za upatanishi wa Qatar, Misri, na Marekani.
Misururu ya malori ya misaada imekusanyika katika mji wa mpakani wa Misri, El-Arish, ikisubiri kuvuka mpaka na kuingia Gaza mara tu utakapofunguliwa tena.
Waziri Mkuu wa Israel, Benjamin Nentanyahu, amechelewesha mkutano wa baraza la mawaziri uliopangwa kufanyika Alhamisi ili kuidhinisha makubaliano hayo, huku akiwashutumu Hamas kwa kuweka masharti ya dakika za mwisho kwenye makubaliano.
Hata hivyo, afisa mwandamizi wa Hamas, Izzat el-Reshiq, amesema kundi hilo limedhamiria kuheshimu makubaliano hayo.