Hata hivyo, watu wengi wamekuwa wakichanganya tumbo na fumbatio. Wanasema tumbo wakimaanisha fumbatio. Hapa nieleze kwa ufupi kuhusu fumbatio.
Fumbatio (abdomen) ni sehemu ya mwili ambayo ndani yake kumehifadhika sehemu zote zilizo kati ya kifua na eneo la nyonga. Hivyo, fumbatio liko chini ya kifua, limetenganishwa na misuli imara inayojulikana kama kiwambo (diaphragm).
Fumbatio humaanisha ‘kuficha’, yaani chochote kilicholiwa kinafichwa ndani ya fumbatio. Ndani yake kuna mfuko wa chakula (tumbo). Pia kuna utumbo mdogo, utumbo mpana, ini, kongosho, figo, kidoletumbo (appendix), kibofu nyongo (gall bladder) na kibofu cha mkojo. Sehemu kubwa sana ya ufyonzwaji na mmeng’enyo wa chakula hutokea ndani ya fumbatio.
Vidonda vya umio
Vidondo vya umio hutokea katika umio, umio (au koromeo) ni bomba la kumezea chakula; na mara nyingi ni matokeo ya pombe. Vidonda hivi kwa kawaida vina uhusiano na ugonjwa wa kurudi kwa asidi (acid reflux) unaojulikana pia kama gastro esophageal reflux disease (GERD).
Umio hauna kunyanzi za ute kwa ajili ya kujilinda dhidi ya asidi ya tumbo, kama ulivyo mfuko wa chakula (tumbo). Pindi asidi ya tumbo iliyozidi inaporudishwa kutoka tumboni hadi kwenye umio, inaweza kubabua kunyanzi za umio ndani ya muda mfupi. Hali hii baadaye husababisha uvimbe na muwasho wa umio unaojulikana kama esophagatis, na baadaye kuwa kidonda.
Sababu nyingine ni matumizi makubwa ya dawa (NSAIDS), uvutaji sigara, athari ya asidi kutokana na kulazimisha kutapika kwa wagonjwa waliokula kupita kiasi na chakula kimelazimika kutoka kwa kutapika, kurudishwa kwa asidi ambako ni kukali sana au kwa muda mrefu (kiungulia kikali), kuleta mabadiliko katika seli ambazo hufunika umio.
Kisha seli hizi huanza kuonesha viashiria vya kansa, na kisha kansa hujitokeza. Inakadiriwa asilimia 10 ya wagonjwa wote wa kurudi kwa asidi (acid refux) hupata kansa. Vidonda vinavyotokea katika umio vinaweza kukufanya usikie maumivu wakati wa kumeza chakula.
Vidonda kutokana na upasuaji
Hivi ni vidonda vinavyotokea kutokana na upasuaji tumboni, hutokea hasa katika kingo za jejunum au duodeni. Utokaji wa damu katika vidonda hivi ni mkubwa. Vipengele vingi vinavyochangia ni pamoja na matumzi ya sigara/tumbaku, kuongezeka kwa asidi tumboni na matumizi ya dawa (NSAIDs).
Vidonda vinavyotokana na msongo mkali wa ugonjwa
Watu ambao wamedhoofishwa kwa ugonjwa mkali sana (kama vile ugonjwa sugu wa upumuaji au kiwewe kikubwa) na msongo wa mwili ni rahisi kupata vidonda vya tumbo. Hii inahisiwa kuwa ni kutokana na usambazaji dhaifu wa hewa ya oksijeni kwenye kunyanzi za tumbo.
Hivyo, kama uvimbetumbo mkali unaweza kutokea kutokana na msongo mkali wa ugonjwa, kuungua kwa moto au kiwewe, kidonda hicho kitaitwa Stress ulcer. Vidonda hivi hutokea ndani ya mfuko wa chakula na duodeni.
Je, vidonda vya tumbo hutokeaje?
Tumeona kuwa istlahi ya kidonda cha tumbo (Peptic ulcer), kilugha humaanisha mmomonyoko wa tishu katika mfumo wa mmeng’enyo wa chakula. Pia tumeona kuwa istilahi hii inaweza kutumika kuelezea kidonda kilicho katika mfuko wa chakula au kidonda kilicho katika utumbo au umio. Baada ya kufahamu hilo, sasa tutazame jinsi vidonda vya tumbo vinavyoweza kujiunda.
Vidonda vya tumbo mara nyingi huhusiana na asidi nyingi zaidi (hypercidity). Wakati kunyanzi katika mfuko wa chakula (tumbo) na duodeni zinapobabuliwa na maji ya asidi yanayotolewa na seli za tumbo, hapo kidonda cha tumbo kinaweza kujiunda.
Mwili umewekewa mfumo wa kinga kwa ajili ya kulinda tumbo na utumbo mdogo dhidi ya hydrochloric acid na pepsin.
Utando wa ute ambao hufunika tumbo na duodeni, huunda mstari wa kwanza wa ulinzi. Bicarbonate ambayo hutema ute, huzimua asidi ya mmeng’enyo. Vitu vinavyofanana na homoni vinavyoitwa prostaglandins husaidia kutanua mishipa ya damu ndani ya tumbo, kuhakikisha mtiririko mzuri wa afya na kinga dhidi ya jeraha. Prostaglandins pia huaminika kuchochea uzalishaji wa bicarbonate na ute.
Itaendelea