Katika toleo la 12 la mfululizo wa makala haya, Dk. Khamis Zephania alieleza dalili za tumbo kujaa gesi na tatizo la kufunga choo. Sasa endelea kumfuatilia katika sehemu hii ya 13.

Kiungulia: Pia huitwa acid reflux, au GERD. Wakati asidi inapokuwa chini, usagaji wa chakula huwa chini pia na mgumu. Matokeo yake ni kwamba chakula hukaa ndani ya tumbo kwa muda mrefu na kutoa gesi ambayo huchoma ndani ya tumbo na koo.

 

Kupungua damu (anemia): Huu ni upungufu wa madini ya chuma. Tatizo hili mara nyingi huhusiana na maambukizo ya H. pylori. Wakati H. pylori anaposababisha asidi ndogo ya tumbo huwa vigumu kumeng’enya protini (ambayo ina madini ya chuma). Hali hii husababisha kupungua damu. Pia kuchuruzika damu kwa muda mrefu huweza kusababisha kupungua damu.

 

Pumzi mbaya: Viumbe hivi vinavyofahamika kama H. pylori vinavyokaa ndani ya asidi ya tumbo hutengeneza ammonia, ambayo matokeo yake huleta pumzi mbaya.

 

Maumivu ya kifua: Wakati H. pylori anaposababisha uvimbe ndani ya tumbo, taarifa za maumivu kutoka tumboni huweza kuakisiwa kifuani, begani na maeneo ya tumbo.

Kuharisha: Kuharisha huweza kutokea mara chache, au pia huweza kutokea kila siku kutegemeana na usugu wa H. pylori.

 

Kichefuchefu na kutapika: H. pylori husababisha kichefuchefu, lakini sababu yake haiko wazi sana. Isipokuwa inadhaniwa kwamba mwili wenyewe unajaribu kumuondoa H. pylori. Dalili hizi zinaweza kufikiriwa kimakosa na hali za kutapika kwa akina mama wajawazito.

Uvimbetumbo (gastritis): Uvimbetumbo ni uvimbe wa kunyanzi za tumbo. H. pylori hutumia umbile lake la kizibuo (corkscrew) kuchimba ndani na kujeruhi kunyanzi za tumbo, ambapo matokeo yake ni uvimbe unaowaka.

 

Dalili nyingine za vidonda vya tumbo ambazo hazina sura maalum ni hofu, wasiwasi, mfadhaiko, uchovu au kuwa na nguvu kidogo, maumivu ya kichwa au kipanda uso, matatizo ya ngozi, kusongeka kabla ya hedhi (pre-menstrual stress), matatizo katika uwazi wa puani na matatizo ya usingizi.

 

Kupungua nguvu za kiume: Vidonda vya tumbo huweza kupunguza nguvu za kiume. Kwa sababu hudhuru sehemu za jirani zinazohusika na utendaji wa nguvu za kiume kama vile ini, n.k.

 

MAGONJWA MAPYA NA DALILI ZA HATARI

Karibu asilimia 0.46 ya watu duniani hufa kutokana na madhara yaletwayo na vidonda vya tumbo.

 

Watu wanafahamu kuwa vidonda vya tumbo vinaleta maumivu katika tumbo, lakini wengi hawafahamu kama vidonda vya tumbo ni tishio la maisha. Vidonda vya tumbo vinaweza kuzalisha magonjwa mapya na kufanya matibabu kuwa magumu.

 

Vidonda vingi vya tumbo vinaweza kutibiwa kabla havijazaa magonjwa mapya. Hata hivyo, katika baadhi ya watu, vidonda vya tumbo vinaweza kuzalisha matatizo makubwa kama vile kupenya katika viungo vingine (penetration), kutoboa (perforation), utokaji wa damu (hemorrhage), kuziba (obstructon) na saratani (cancer).

 

Magonjwa mapya kama vile kutoka damu (bleeding) au kupasuka, huambatana na dalili za shinikizo la damu la kushuka (low blood pressure), kama vile kizunguzungu na udhaifu.

 

Dalili za hatari hizi ni: Shida ya kumeza chakula au kucheua (regurgitation), kudumu kujisikia kichefuchefu na kutapika, kutapika damu au matapishi yenye sura ya unga wa kahawa, choo cheusi kinachofanana kama lami (chenye damu iliyomeng’enywa iliyotolewa kutoka katika kidonda), kupungua uzito ghafla, kupungua damu (kukwajuka na kudhoofika), maumivu makali ya ghafla tumboni ambayo humuondolea mtu nguvu na kupungua nguvu za kiume.

 

Hapa tutajadili magonjwa mapya ambayo huweza kuzalishwa na vidonda vya tumbo, magonjwa ambayo huweza kuleta dalili tulizozieleza.

 

Kupenya katika viungo (penetration): Kidonda kinaweza kupenya na kuingia kwenye kuta za misuli ya tumbo au duodeni (sehemu ya awali ya utumbo mdogo) na kuendelea hadi kwenye kiungo cha jirani.

 

Upenyaji huu husababisha maumivu makali ya kuchoma na ya kudumu, ambayo yanaweza kuhisiwa nje ya eneo linalohusika – kwa mfano, mgongo unaweza kuuma pindi kidonda cha duodeni kinapopenya kwenye kongosho.

 

yanaweza kuongezeka pale mtu anapobadilisha namna ya ukaaji. Kama dawa hazitaweza kutibu upasuaji unaweza kuhitajika.

 

Itaendelea