Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam, Paul Makonda amesema kuwa, njia itakayotumika kuwapima saratani ya tezi dume wanaume wa Dar es Salaam ni njia ya damu na sio kwa kutumia kidole kama inavyodhaniwa na baadhi ya watu.
Ameeleza kwamba, anao mkakati wa kupita nyumba kwa nyumba ili kuwapima wanaume saratani tezi ya dume kwa sababu ugonjwa huo unawasumbua sana na hakuna mwamko katika jamii wa kukabiliana nao.
“Kuna kasumba kuwa saratani ya tezi dume inapimwa kwa kidole, jamani siyo kweli, kuna kipimo cha damu na ni rahisi hivyo nina mkakati wa kupita nyumba kwa nyumba katika mkoa wangu kuhakikisha hii kasi ya vifo kwa kinababa inapungua kwa kuwagundua mapema na kuwaanzishia matibabu,” amesema Makonda.
Alisema hayo jana Aprili 21 wakati akifungua rasmi warsha ya chanjo ya saratani ya mlango wa kizazi kwa wasichana wote wenye umri wa miaka 14 inayotarajiwa kuanza kutolewa Jumatatu wiki ijayo.
Makonda aliyekuwa ameambatana na wataalamu wa afya, viongozi mbalimbali wa dini na siasa alitanabaisha kwamba, wakati saratani ya mlango wa kizazi ikiwaathiri wanawake nchini, tezi dume inaumiza zaidi akina baba ambao hata hivyo hakuna mwamko wa kulizungumzia jambo hilo katika jamii.
Pia, ametoa wito kwa viongozi wote wa serikali za mitaa na viongozi wa dini kuhakikisha wanatoa elimu kwa jamii ili wasichana wote wenye umri huo wafike kwenye vituo kwa wingi kupata chanjo.
Amewataka wasichana watakaopatiwa chanjo hiyo kuhakikisha wanakamilisha matibabu kama watakavyolekezwa na watalaamu wa afya ili wawe salama.