Muda ni saa 3:35 usiku wa Ijumaa ya wiki iliyopita. Nimejipumzisha barazani baada ya kupambana na foleni za Dar es Salaam. Simu yangu inaashia kuingia kwa ujumbe wa WhatsApp. Nafungua na kuanza kuusoma: “Kuna njia gani ya kuwapata hawa wanaume wawili waliomtesa huyu mwanamama kiasi hiki?”

Chini ya ujumbe huo, kuna ‘clip’ mbili za video zilizoambatanishwa na maneno haya ya hadhari: “Sorry for the content”. Huyu aliyeniletea ‘clip’ hizi, anaomba radhi kwa kutambua nitaumia baada ya kuziona hizo picha.

Naziona, najaribu kuzifungua, lakini mtandao uko chini. Namjibu: “Naona network iko chini, ngoja nisubiri kisha nizione”.

Shauku ya kutaka kuziona hizo ‘clip’ inazidi kunipata, na kabla hazijafunguka, aliyeniletea ananiandikia maneno haya: “Wamemtesa sana huyu mwanamama. Sidhani kama kisaikolojia yuko sawa. Na akijua inatembea (inasambaa) ndiyo kabisa!!”

Haya ni maneno kutoka kwa kaka yangu ambaye kwa maudhui ya makala hii, naomba nimhifadhi jina. Yeye ndiye aliyeiona hii video kabla yangu na kuamua kuileta kwangu, si kwa namna nyingine, isipokuwa kwa kuamini naweza kutoa mchango wowote wa kitaaluma.

Baada ya muda, video inafunguka. Naanza kuona sura ya mwanamke mwenye umri ambao bila shaka haujavuka miaka 30.

Wapo katika chumba kinachoashiria ni nyumba ya kulala wageni. Pembeni kuna mwanaume mwingine aliyevalia msuli mwekundu. Mtu wa tatu ni mwanamme ambaye haonekani. Haonekani kwa sababu ndiye anayerekodi hiki kinachoendelea. 

Kwa shida kubwa, naendelea kuitazama video hii, lakini nashindwa kuimaliza. Napatwa na uchungu mkubwa. Najikakamua na kufungua video ya pili yenye wahusika hao hao watatu.

Unaweza kusema heri ile ‘clip’ ya kwanza kuliko hii nyingine. Binti anaingiliwa.

Muda wote binti huyu analia. Ni kilio kisichoambatana na machozi. Anaomba. Anabembeleza asipigwe picha. Anavuta shuka, anafunika uso, lakini ananyang’anywa. Analazimishwa aweke wazi sehemu zake za siri huku akitetemeka mithili ya sungura aliyewekwa kwenye banda lenye chatu! 

Analia, anaomba kwa kutaja jina: “Zuberi naomba usinipige picha, sitarudia tena.”

Anashikwa na huyu aliyekuwa na msuli mwekundu. Mwenye kamera anampa maelekezo kwa kumwita jina: Iddi”. Anamwingilia kwa nguvu huku huyu mwenye kuchukua picha akimwelekeza awe katika mkao gani! Ni kama taniboi (mwenye kamera-Zuberi) alimwelekeza dereva (Iddi) nini cha kufanya.

Binti hana amani kabisa. Anaweweseka kwa hofu kuu. Anafanya kila anachoamuriwa huku akitetemeka na kulia. Anarusha mikono kuomba msaada asiouona. Ni mithili ya mtu aliyefukiwa shimoni akiwa hana namna ya kujiokoa. Kwa kumtazama, anachoomba ni kuachiwa roho yake tu.

Baada ya kuzitazama ‘clip’ hizi, narejea kwa kaka yangu. Naandika maneno haya: “Kaka, hii ‘clip’ imeniumiza sana sana. Nafikiria kama ni mwanangu halafu anaonewa namna hii! Hapo nitafia jela.” 

Nakosa amani na kuanza kuwaza ni kwa namna gani huyu binti anaweza kupata haki kutokana na uonevu huu aliotendewa. Lakini pia napata shaka kama kweli bado yungali hai.

Kaka yangu ananiletea ujumbe mwingine unaosomeka: “Una mbinu ya ku-trace (kujua mahali tukio hili lilipotokea?”)

Namjibu: “Kwanza, nataka nijue ilipo hii lodge”.

Nimekosa amani. Muda ni saa sita usiku, nakwenda chumbani kujipumzisha. Napata usingizi wa mang’amung’amu. Kila nikishituka, nawaza tukio hili ambalo nikiri kuwa ni la kwanza kulitazama.

Asubuhi na mapema naamka nikijiandaa kwenda kazini. Nawaza ni kwa namna gani nitajua mahali lilikofanyiwa. Napata akili ya kuperuzi upya ‘clip’ hizi. Natumia utaratibu wa ku-zoom picha na kufanikiwa kuona maandishi haya: “Tith Lodge, P.O.BOX 63 Wami-Dakawa.” Kwa kuwa shuka imejikunja kidogo, hiyo “63” kuna namna fulani inaonekana kama “163”. Linalonipa faraja ni hili jina la eneo (Wami Dakawa).

Naondoka asubuhi kwenda kazini. Baada ya kuwasili tu, akili inanijia kuwa mitandao ya kijamii inaweza kusaidia kupata taarifa zaidi juu ya tukio hili, na hasa kujua kama Wami Dakawa kuna lodge yenye jina hili.

Nafungua JamiiForoums. Chini ya kichwa cha habari “video iliyonitoa machozi’, naandika maneno haya: “Ndugu zangu, jana usiku kaka yangu mmoja kaniletea video iliyonifanya nisipate usingizi. Ni ‘clip’ mbili za dada mmoja aliyetekwa na kuwekwa chumbani na wanaume wawili. Wamempiga picha za uchi na kumtendea tukio baya kabisa.

“Yule dada analia na anajaribu kuficha sura, lakini anapigwa na kuingiliwa kwa nguvu. Wanazungumza Kiswahili. Wanaonesha ubakaji kwa kurekodi. Shuka la nyumba linasomeka Teth Lodge, ya BOX 63. Mahali ilipo hapaonekani vema, lakini ni kama vile Wami Dakawa.

“Sidhani kama huyu dada ataendelea kuishi kama binadamu wa kawaida maana kisaikolojia lazima atakuwa kaumia sana hata akibaini hii ‘clip’ inasambazwa tayari. “Nimeshindwa kuiweka hapa kwa kuwa inasikitisha sana. Naandika nikilengwa na machozi.

“Sihukumu, Mungu anisamehe lakini nadhani hawa wabakaji wanastahili adhabu kali kuliko zote tuzijuazo. Mungu ampe nguvu huyu binti.”

JamiiForums ina wasomaji wengi pande zote – ndani na nje ya nchi. Mara moja, watu wanaanza kuchangia. Nawasiliana na Mkurugenzi wa JamiiForums, Maxence Melo, naye ananipa moyo; na tunajadili namna ya kuhakikisha tukio hili linapatiwa jawabu kulingana na uwezo wetu kitaaluma.

Kutwa nzima nakosa amani, lakini jioni napokea simu kutoka kwa mmoja wa wanawake watetezi wa haki za binadamu. Ameusoma ujumbe niliouweka JamiiForums. Tunashauriana mengi.

Punde, simu yangu inaita. Ni simu ya Waziri wa Mambo ya Ndani ya Nchi, Charles Kitwanga. Ananiuliza kuhusu habari hiyo. Namweleza maudhui yote. Anasikitika. Sauti yake inaashiria mtu aliyekuwa tayari kuamka yeye mwenyewe kwenda kuwasaka wahusika! Ananiambia baada ya muda nitapata mwongozo wa nini kifanyike ili huyo binti aweze kutendewa haki.

Baada ya dakika 10 hivi, Waziri Kitwanga anarejea kwangu na kutamka maneno haya: “Napenda kukupa habari njema. DCI (Diwani Othman), ameshawatuma vijana, na hivi tunavyozungumza tayari watuhumiwa wameshakamatwa.

“Tukio hili ni baya, baya, baya sana. Tutahakikisha wahusika wanafikishwa mahakamani. Hatutaki mchezo.”

Maneno haya ya Waziri Kitwanga yananipa faraja. Najisemea moyoni: “Kumbe polisi wakiamua kufanya kazi, wanaweza”.

Kinachoonekana hapa bila shaka si matokeo ya ujumbe niliouweka JamiiForums uliowaamsha, bali yawezekana walipata taarifa hizi mapema wakaamua kuzifanyia kazi.

Msongo wa mawazo niliokuwa nao unapungua, lakini naendelea kumkumbuka na kumhurumia yule binti aliyefanyiwa upuuzi ule. Baadaye najikuta nikibubujikwa na  machozi.

Kauli hii ya Waziri Kitwanga inanifanya mchana wa Jumapili nimtafute DCI Diwani nikiwa ofisini. Nampigia simu. Anapokea, nami najitambulisha.

Naanza kumpongeza yeye na vijana wake kwa kazi kubwa inayoashiria uzalendo na uwajibikaji wao ambavyo ni ishara ya binti huyu kutendewa haki.

DCI anathibitisha kuwa watuhumiwa wote wawili wa tukio hili wameshakamatwa. Mmoja alikamatwa akiwa Mbarali mkoani Mbeya, na mwingine akiwa Makambako mkoani Njombe.

“Nilipoona tukio lile nikasema hakuna sababu ya kuchelewa. Nikawatuma vijana wangu. Vijana hawakulala kabisa. Walifika Wami-Dakawa wakabaini watuhumiwa hawapo. Wakajua walikoelekea. Hawakutaka kulala maana wangeharibu upelelezi. Wakaondoka muda huo huo kwenda walikokuwa wamekimbilia.

“Mmoja wamemkamata akiwa Makambako na mwingine akiwa Mbarali. Nawapongeza sana vijana hawa. Wamefanya kazi nzuri sana bila kujali hali ngumu tuliyonayo.”

DCI anasema upelelezi unaendelea, na lililo dhahiri ni kuwa watuhumiwa watafikishwa mahakamani kujibu mashitaka yanayowakabili.

“Niwaombe wananchi haya mambo ya kijinai sheria zake zipo. Matusi mitandaoni, kashfa na mengine…mwananchi ukiona picha mbaya kama hizi asizitume kwa wengine maana kufanya hivyo ni kusambaza taarifa ambazo ni kosa kisheria,” anasema.

Taarifa zilizopo ni kuwa binti huyo ameshaanza kupambana na athari za tukio hilo. Timu ya polisi ikishirikiana na wataalamu wengine wa saikolojia, wameanza kumsaidia ili arejee kwenye hali yake ya kawaida.

Hilo likiwa linafanywa kumrejesha katika hali ya kawaida, familia yake imemfukuza nyumbani. Kwa sasa anaishi kwa mama yake mkubwa.

Ndugu zangu, tukio kama hili, hata wanyama wa kufugwa au wa maporini, sidhani kama wanaweza kulitenda. Naandika, si kwa kuhukumu, bali kwa kusikitishwa na kile nilichokiona mimi na wengine kwenye video hiyo. Mbwa au mbuzi hawawezi kutendeana  hivi. 

Wala sidhani kama simba au fisi wanaweza kushiriki ubakaji wa aina hii; ndiyo maana napinga tukio hili kuitwa la kinyama kwa sababu hata wanyama wenyewe wasiokuwa na utashi hawafanyi haya! Hapa ndipo unapoweza kuona hata shetani ambaye ndiye tunayeamini ni kinara wa dhambi, naye akitushangaa binadamu kwa kumpiku!

Nimeguswa na tukio hili kwa sababu nimejaribu kukaa upande wa pili wa binti na kumuona ni binti yangu, ni dada yangu, ni mama yangu, ni shangazi yangu, ni binadamu mwenzangu. Ni tukio la kutia simanzi na kuiumiza akili – ya aliyetendewa na anayeliona.

Matukio ya aina hii bila shaka yapo mengi. Hili tumeliona kwenye mitandao kwa sababu wahusika wamekuwa na ujasiri wa kuliweka humo. Je, matukio mangapi ya unyanyasaji ya aina hii yasiyoripotiwa?

Tanzania tunakabiliwa na kashfa ya mauaji ya albino, vikongwe na ajuza. Na sasa yameanza mauaji ya halaiki katika familia. Yalianzia Musoma kwa watu 20 hivi, na juzi Sengerema wameuawa watu saba. Nilidhani hayo yametosha kutuchafua mbele ya walimwengu. Kuongeza mengine ya aina hii, hakika tunazidi kuichafua nchi yetu.

Hata kama huyu binti alikuwa na makosa – hata kama alikula au kunywa vilivyotokana na fedha za wanaume hao, hata kama alifumaniwa, hata kama alikuwa ametenda kosa kubwa kiasi gani, alichofanyiwa ni kitu kibaya mno.

Kina mama na kina baba sote tuna wajibu wa kujitokeza kwa maandishi na kwa sauti kulaani tukio hili na mengine ya aina hii katika jamii yetu. Ukitaka kuujua uchungu wake, hebu kaa upande wa aliyetendwa. Kaa upande wa wewe uwe mzazi wa huyo binti au uwe kaka au dada yake. 

Hongera sana Jeshi la Polisi kwa kazi nzuri mliyoifanya. Wataalamu wa saikolojia na wanaharakati ndiyo wakati wao huu wa kuonesha mshikamano. Nimeandika si kwa kuwahukumu watuhumiwa Idi na Zuberi, bali kwa kuonesha kupinga tukio hili baya. Mungu ampe ujasiri binti huyu mnyonge – ajione bado ana thamani na umuhimu wa kipekee katika jamii na Taifa lake. Mungu wa haki daima yuko upande wa wanyonge.