Na Mwandishi Wetu, JamhuriMedia, Dar es Salaam
Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania imeendelea kumuamini Victor Tesha kama mmoja wa viongozi vijana wenye uwezo wa kusimamia mageuzi makubwa ya kitaifa, kufuatia uteuzi wake mpya kuwa Mwenyekiti wa Timu Maalum ya Wataalamu wa Kuishauri Wizara ya Madini juu ya mbinu bora za kuwawezesha wachimbaji wadogo wa madini kiuchumi kupitia uchimbaji wenye tija na endelevu.
Timu hiyo, iliyoanzishwa na Waziri wa Madini, Anthony Peter Mavunde (Mb.), inalenga kutekeleza kwa vitendo maelekezo ya Mheshimiwa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dkt. Samia Suluhu Hassan, kuhusu ujenzi wa mabilionea wa Kitanzania kupitia sekta ya madini—ikiwa ni sehemu ya ajenda ya mageuzi ya kiuchumi kwa kuwatumia wazawa.

Waziri Mavunde alieleza kuwa uteuzi wa Tesha ni sehemu ya mkakati wa kuiimarisha sekta ya madini kwa misingi ya kitaalamu, kiuwekezaji na kibiashara, huku kipaumbele kikiwa ni kuwawezesha wachimbaji wadogo ambao kwa muda mrefu wamekuwa uti wa mgongo wa sekta hiyo lakini wakikabiliwa na changamoto nyingi.
“Victor Tesha ameonesha uwezo mkubwa katika kusimamia mageuzi ya kisera na kiutendaji, hususan katika sekta ya ubunifu. Tunaamini uzoefu wake na maono yake vitaisaidia timu hii kuleta mapendekezo yatakayofungua ukurasa mpya kwa wachimbaji wadogo,” alisema Mavunde.
Timu hiyo itajumuisha wataalamu kutoka sekta mbalimbali, wakiwemo wachumi, wanasheria, wataalamu wa madini, wawakilishi wa wachimbaji wadogo, pamoja na wawakilishi kutoka taasisi za kifedha na zinazotoa huduma za teknolojia ya madini.
Historia ya mafanikio ya Victor Tesha
Victor Tesha si jina geni katika uongozi wa mabadiliko ya kitaifa. Mnamo mwaka 2022, aliandika historia kwa kuongoza Kamati Maalum ya Kuratibu Mjadala wa Namna Bora ya Kusimamia Hakimiliki, jukumu lililozalisha mageuzi makubwa katika Sheria ya Hakimiliki na Hakishiriki.
Kupitia uongozi wake, Tanzania ilianzisha Taasisi Maalum za Usimamizi wa Haki (CMOs), ikatunga Tozo ya Hakimiliki, na hatimaye kuweka misingi imara ya kuwalinda wabunifu na kuwapa heshima na kipato stahiki. Mafanikio hayo yalimuinua kuwa Mwenyekiti wa Bodi ya COSOTA, ambako alisimamia maboresho ya mifumo ya usajili, ukusanyaji na usambazaji wa mapato kwa wabunifu.

Uteuzi wake wa sasa unaonesha namna Serikali ya Awamu ya Sita inavyoendelea kuwapa nafasi vijana wenye uthubutu, ujuzi na maono ya mbali katika kuendesha mageuzi ya kimkakati, kulingana na dira ya maendeleo ya taifa na malengo ya Mpango wa Tatu wa Maendeleo wa Taifa wa Miaka Mitano (2021/22 – 2025/26).
Matarajio ya Timu ya Tesha
Kwa mujibu wa Sera ya Taifa ya Madini ya mwaka 2009 na Ilani ya Uchaguzi ya CCM ya mwaka 2020, Serikali inalenga kuwawezesha wachimbaji wadogo kwa kuwapatia teknolojia rafiki, mitaji ya kuaminika, taarifa sahihi za kijiolojia na mazingira salama ya kazi.
Timu ya Tesha inatarajiwa kuandaa mapendekezo mahsusi yatakayosaidia kufungua fursa mpya, kuongeza mchango wa sekta ya madini kwenye pato la taifa, na kuijenga Tanzania yenye uchumi jumuishi unaotegemea rasilimali watu na ardhi kwa ustawi wa wote.
