Na Mwandishi Wetu, JamhuriMedia, Morogoro
Mamlaka ya Elimu na Mafunzo ya Ufundi Stadi (VETA) kupitia Chuo cha Ualimu wa Ufundi Stadi Morogoro (MVTTC) wametia saini hati ya makubaliano na Chuo cha Taifa cha Usafirishaji (NIT), kuanzisha ushirikiano wa utoaji wa mafunzo yanayolenga kukabiliana na changamoto ya kukua kwa mahitaji ya walimu wa ufundi na ufundi stadi nchini.
Makubaliano hayo yamesainiwa Januari 17, 2024 kati ya Mkurugenzi Mkuu wa VETA, Dkt Prosper Mgaya na Kaimu MKuu wa NIT, Dkt Zainabu Mshana, katika ukumbi wa mikutano wa MVTTC, mjini Morogoro.
Kwa mujibu wa Hati ya Makubaliano (MoU), malengo ni kushirikiana katika kutoa mafunzo, kuandaa na kutekeleza mitaala, ubunifu na utafiti katika nyanja mbalimbali za ufundi na ufundi stadi ili kukabiliana na ombwe la mahitaji ya nguvukazi yenye ujuzi katika maeneo ya uhandisi, usafirishaji na uhawilishaji teknolojia.
MoU imeyataja maeneo mahsusi na ya kipaumbele katika ushirikiano kuwa ni pamoja na kubadilishana taarifa za uandaaji mitaala yenye maudhui ya ualimu wa ufundi na ufundi stadi kuhusiana na fani za uhandisi katika ngazi ya stashahada. (NTA Level 6); kubadilishana taarifa za uandaaji mitaala yenye maudhui ya ualimu wa ufundi na ufundi stadi kuhusiana na fani za uhandisi katika programu za ngazi ya 7 hadi 9 (NTA Level 7 to 9) na ubadilishanaji wa wakufunzi katika program za uhandisi na ualimu wa ufundi na ufundi stadi.
Akizungumza kabla ya utiaji saini wa hati ya ushirikiano, Mkurugenzi Mkuu wa VETA, Dkt Prosper Mgaya, amesema jitihada za Serikali katika kueneza elimu ya ufundi na mafunzo ya ufundi stadi zinaakisi mahitaji makubwa ya walimu wa ufundi na ufundi stadi ili kuwezesha utoaji wa mafunzo hayo kwa ubora.
Amefafanua kuwa ujenzi wa vyuo vya ufundi stadi kila mkoa na kila wilaya, pamoja na uboreshaji wa mitaala ya elimu katika elimu ya sekondari kwa kuingiza mafunzo ya amali utatekelezwa vyema ikiwa walimu wataandaliwa ipasavyo katika kutoa mafunzo hayo.
“Januari mwaka huu, vyuo vipya 29 vya VETA vinaanza kutoa mafunzo. Lakini mpaka kufikia mwaka 2025 kutakuwa na vyuo 147 vya VETA, pamoja na shule za sekondari zinazotoa mafunzo ya amali, ambavyo vyote vinahitaji walimu. Kwa hatua iliyochukuliwa na MVTTC itapelekea upatikanaji wa hao walimu katika vyuo vipya vinavyoanzishwa na shule za sekondari za mkondo wa amali,” amesema.
Ameongeza kuwa kwa sasa walimu wa shule za sekondari wanaendelea kupewa semina ili waweze kuendana na mtaala mpya wa mafunzo ya amali kwa shule za sekondari, lakini pia inahitajika kuwaandaa walimu wa ufundi ambao watakuwa na uwezo mkubwa wa kufundisha mafunzo haya ya amali kwa sekondari.
Naye Kaimu Mkuu wa NIT, Dkt Zainabu Mshana ameunga mkono kwa kusema kuwa nguvu na juhudi zinahitajika ili kuhakikisha walimu wa mafunzo ya amali wanaandaliwa kwa ubora wa hali ya juu.
“Huwezi kumchukua mwalimu wa historia, au kemia au hisabati kwenda kufundisha mafunzo ya amali. Sisi tulikuwa tukifundishwa na walimu waliobobea kwenye ujuzi wa ufundi, hivyo hata sasa nguvu inahitajika kuwaandaa walimu wa ufundi na ufundi stadi,” amesema.
Dkt. Mshana ameahidi kushirikiana na VETA bega kwa bega ili kuhakikisha ushirikiano huo unafikia malengo yaliyokusudiwa.
Mwenyekiti wa Baraza la Uongozi wa MVTTC, Profesa Zakaria Mganilwa, amesema ushirikiano huo ulioanzishwa utachagiza uzalishaji wa walimu mahiri wengi wa Fani za Ufundi Stadi na hatimaye kuleta matokeo makubwa katika upatikanaji wa nguvukazi yenye ujuzi wa ufundi.