Serikali imetakiwa kutazama upya mpango wake wa kukopa ndani na nje ya nchi pamoja na kutafakari upya suala la kuanzisha Kodi ya Ongezeko la Thamani (VAT) katika sekta ya utalii.
Bajeti iliyowasilishwa bungeni, Dodoma na Waziri wa Fedha na Uchumi, Dk. Philip Mpango, Serikali ina mpango wa kukopa kiasi cha Sh trilioni 7.47.
Akizungumza na JAMHURI, mtaalamu wa uchumi, Profesa Mohamed Warsame, anasema Serikali inakumbwa na hatari kubwa tatu katika mfumo wake wa mapato, ambayo ni kuwa wafadhili na wabia wa maendeleo wanaweza kuchelewa kutekeleza ahadi zao katika bajeti kuu. Bajeti ya 2016/17 misaada na mikopo inatarajiwa kufikia Sh 3.6 trilioni.
Prof. Warsame anasema Serikali inatakiwa kuwa makini na kukua kwa deni la Taifa, ambalo linakula sehemu kubwa ya mapato ya ndani. Katika bajeti ya mwaka 2016/17 Serikali inatarajia kukopa ndani na nje ya nchi kiasi cha Sh trilioni 7.47 hivyo kwa ujumla deni litaongezeka na kuwa mzigo, suala ambalo ni hatari katika ustawi wa Taifa.
“Mapato yasiyotokana na kodi yanatarajiwa kuongezeka kwa asilimia 140, hivyo Serikali kupata Sh trilioni 2.69,” anasema Prof. Warsame na kuongeza kwamba hilo ni eneo ambalo halitabiriki, hivyo si la kutegemea mno.
Mbunge wa Kigoma Mjini na Mwenyekiti wa Chama Cha ACT-Wazalendo, Zitto Kabwe, anasema Serikali imeanzisha VAT kwenye huduma za utalii wakati nchi jirani katika Jumuiya ya Afrika Mashariki imeondokana nazo.
“Tanzania imeanzisha Kodi ya Ongozeko la Thamani (VAT) kwenye huduma za utalii. Waziri anasema Kenya wanayo, wakati ukweli ni kwamba wakati wa kusoma bajeti yao, Kenya wameondoa kodi hiyo.
“Maana yake ni kwamba watalii wataona Kenya ni rahisi zaidi kuliko Tanzania. Idadi ya watalii ikipungua maana yake mahoteli yatakosa biashara na kupunguza wafanyakazi. Wafanyakazi wakipungua Serikali inapoteza kodi ya PAYE, kuna haja ya Serikali kutazama hili. Sekta ya utalii ni sekta muhimu sana katika kuongeza ajira,” anasema Prof. Warsame.
Katika maelezo yake Prof Warsame anasema, bajeti hii imelenga kuongeza matumizi ya maendeleo huku ikiweka msisitizo katika kuimarisha sekta ya miundombinu, sekta ambayo itaboresha uchumi na kuleta ushindani katika kipindi cha miaka 10 ijayo.
Mtaalamu huyo wa uchumi anasema bajeti itaboresha matumizi ya kijamii katika sekta za afya na elimu, ambazo sasa zinafikia asilimia 22 ya bajeti ukiondoa deni la Taifa.
Hata hivyo, anasema bajeti ya mwaka 2016/17 haijajielekeza katika kupunguza umaskini, kutokana na fedha kidogo kuelekezwa katika wizara inayojihusisha na masuala ya vijana na mamlaka za Serikali za Mitaa.
Anasema ushirikishwaji wa kifedha utaathiriwa na kuanzishwa kwa kodi ya ongezeko la thamani katika ada za benki. Prof Warsame anasema katika bajeti ya mwaka 2016/17 kuna tatizo kubwa ambalo ni kukua kwa matumizi kuliko vyanzo vya mapato, wakati matumizi ni Sh trilioni 29.5, mapato ni Sh trilioni 15.1.
Anasema bajeti ya mwaka huu haijagusa moja kwa moja wananchi wenye vipato vidogo, badala yake imelenga katika mipango ya uwekezaji wa muda mrefu, isipokuwa ahueni kidogo kwa wafanyakazi kama ilivyosemwa awali na Rais John Magufuli, wakati wa sherehe za Mei Mosi, pale mkoani Dodoma, alipoahidi kushusha kodi katika mishahara.
Naye mtaalamu wa masuala ya mifumo ya kielektroniki, Abel Kaseko, anasema bajeti hii imejikitika katika kuweka mazingira mazuri ya kujenga uchumi imara wa viwanda na pia kutatua kero za wananchi ikiwamo ununuzi wa meli mpya.
Serikali wanapaswa kuhakikisha zaidi ya Sh trilioni 4.5 ambazo zimetengwa kwa ajili ya miundombinu zinakwenda kwenye kampuni za ndani zaidi kutengeneza ajira na kukuza pato la Taifa.
“Asilimia 94 ya bajeti ya Nishati itakuwa kwenye maendeleo, hivyo nategemea shirika la Tanesco litaimarisha miundombinu na kuhakikisha usambazaji wa umeme vijijini unafikia asilimia 55 kutoka 40 ya sasa,” anasema Kaseko.
Anasema ukuaji wa biashara na uchumi wa nchi unategemea Serikali kwa kiasi kikubwa, hivyo inapaswa kuliangalia vyema agizo lake la kutaka mashirika ya umma yatumie bima kutoka Shirika la Bima la Taifa.
“Ni lengo zuri la kusaidia NIC ila linaweza kuathiri sekta hii ambayo kwa kaisi kikubwa inategemea biashara na Serikali, NIC wapewe asilimia 30 au 40 ya biashara na nyingine iachwe kwa sekta binafsi ambao wataweza kutoa ajira na kulipa kodi,” anasema Kaseko.
Kuhusu tozo ya ongezo la thamani kwenye ada za malipo ya kifedha anasema litazamwe upya, kwa sababu zitaongeza gharama kwa mwananchi na kuathiri ukuaji wa sekta hii.
“Nchi nyingi za SADC wanakata ongezeko la thamani pekee, wakati sisi na nchi za Afrika Mashariki wanatoza ushuru wa bidhaa na kodi ya ongezko la thamani. Siku zijazo Serikali ifikirie kuondoa kodi ya bidhaa ili kuchochea ukuaji wa sekta ya fedha,” anasema Kaseko
Anasema jitihada za Serikali kuyabana mashirika ya umma na kuwasilisha zaidi asilimia 15 ya mapato yao ghafi (kabla ya kodi) umechelewa, wasiishie hapa ila waendelee kufuatilia utendaji wa mashirika haya na kuhakikisha yana bodi na menejimenti zenye watu walio na sifa, weledi na uzoefu katika kuleta mabadiliko na mafanikio.