Nahodha wa Klabu ya Manchester United, Antonio Valencia (33), amesema Meneja wake, Jose Mourinho, amemnyang’anya kitambaa cha unahodha bila sababu ya msingi.

Amesema Mourinho alisingizia kwamba yeye ni majeruhi, jambo ambalo si kweli, huku akisema huo ulikuwa ni uamuzi binafsi wa kocha wake. Amesisitiza kwamba hana jeraha lolote, bali huo ni uamuzi wake binafsi. Kwani hana jeraha lolote.

Hivi karibuni Kocha wa Manchester United, Jose Mourinho, aliibua vita mpya na nahodha wake, Antonio Valencia. Taarifa za ndani ya klabu hiyo zilieleza kuwa Mourinho na nahodha wake (Valencia) hawazungumzi licha ya kocha huyo kudai anaungwa mkono na idadi kubwa ya wachezaji.

Kutokana na mgogoro huo, Valencia ameshindwa kukamilisha maboresho ya mkataba mpya kwa klabu hiyo, hivyo kutokuwa na uhakika wa kuendelea kuwepo katika kikosi cha Manchester United.

Mourinho ametengwa na idadi kubwa ya wachezaji pamoja na Mtendaji Mkuu wa Man United, Ed Woodgard, baada ya kuibua mizozo ya mara kwa mara ndani ya klabu.

Valencia hakucheza mechi ya Kombe la Ligi dhidi ya Derby waliofungwa kwa penalti 8 – 7, baada ya kutoka sare 2 – 2 na aliachwa dhidi ya West Ham United, mchezo ambao Man United ililala 3 – 1.

Baada ya mchezo dhidi ya West Ham, Mourinho alimtolea maneno makali, Alexis Sanchez, akidai ni mzigo, hana mchango ndani ya timu hiyo.

Wachezaji wasiokuwa na uhusiano mzuri na Mourinho ni Paul Pogba, Anthony Martial, Marcus Rashford, Andreas Pereira na beki wa kati, Eric Bailly.

Oktoba, 2018

Valencia alilazimika kuomba msamaha baada ya ‘ku-like’ ujumbe wa picha uliopandishwa kwenye mtandao wa Instagram katika ukurasa wake ambao hutumika kumuunga mkono mchezaji huyo.

Ujumbe huo ulipandishwa na shabiki aliyeeleza kuwa ametazama mchezo wa Ligi ya Mabingwa Ulaya kati ya Manchester United dhidi ya Valencia ya Hispania, huku akitoa msimamo wake kuwa Kocha Jose Mourinho anatakiwa kufukuzwa.

Katika kuomba msahama, Valencia amesema ‘ali-like’ picha hiyo bila kusoma ujumbe uliokuwa umeandikwa hivyo hakujua kama una maneno yasiyofaa kwa kocha wake.

Mourinho amekuwa akikosolewa na watu mbalimbali akiwemo kiungo wa zamani wa klabu hiyo, Paul Scholes, ambaye amedai ni muda mwafaka kwa Mreno huyo kuachia ngazi.

Septemba 2018

Mourinho amethibitisha kwamba kiungo Paul Pogba amepokonywa unaibu nahodha wa timu ingawa amepuuza kwamba kuna uhusiano baridi kati yake na mwanasoka huyo wa zamani wa Juventus ya Italia.

“Ukweli ni kwamba nimefikia uamuzi wa kumpokonya Paul unahodha wa timu lakini si kwa sababu sielewani naye, hakuna shida kati yetu. Mimi ndiye wa kuamua nani atakuwa nahodha na nani atakuwa mchezaji wa kawaida. Mimi ndiye kocha na huu ni uamuzi ambao si lazima niuelezee,” alijitetea Mourinho.

Pogba alikuwa nahodha wa Manchester United wakati wa mechi za Ligi ya EPL dhidi ya Leicester City, Brighton na  Hove Albion na katika mechi ya Ligi ya Europa dhidi ya Young Boys, nahodha wa timu Antonio Valencia alipokosekana kikosini.

Hata hivyo Pogba hakuungana wala kukamilisha kikosi kilichotolewa nje ya Kombe la Carabao na Derby County inayotiwa makali na staa wa zamani wa Chelsea, Frank Lampard.

Katika mechi hiyo walitoka sare ya 2-2 muda wa kawaida, mlinzi Phil Jones alikiingiza kitumbua cha Manchester United mchangani baada ya kupoteza penalti na mechi ikaisha kwa 8 – 7.