Sikio halilali njaa, wapenzi wa muziki wa Bongo Fleva baada ya kukanyaga na kutimua vumbi mitaani kwa nyimbo za vijana wa kundi la Wasafi (WCB) sasa ni muda wa Vanessa Mdee, maarufu kama Cash Madame na wimbo wake wa ‘Moyo’.

Vanessa Mdee ambaye kwa mashabiki wake anafahamika zaidi kama V. Money, ameachia wimbo wa ‘Moyo’ wiki iliyopita ukiwa ni sehemu ya mpango wake wa kuachia EP (Extended Play) yake ya ‘Expensive’.

Video ya wimbo huo baada ya V. Money kuiachia kwenye mtandao wa Youtube  kabla ya kutimiza saa 24 ilikuwa tayari na watazamaji zaidi ya 130,000 na kati ya watazamaji hao, 7,300 walionyesha kuvutiwa nayo na kuipenda huku watu 117 wakionyesha kutoipenda ama kuvutiwa nayo.

Video ya wimbo wa ‘Moyo’ ina dakika mbili na sekunde 26, mashairi yaliyomo kwenye wimbo huu wa ‘Moyo’, V. Money anayaimba kwa kueleza jinsi moyo wake unavyomkosea japo anautegemea katika uamuzi wa mambo yake mengi.

Wimbo huo umetengenezwa katika studio za Pluto na mtayarishaji wake akiwa S2Kizzy. Mbali ya wimbo huu kutengenezwa na kijana mdogo mwenye bahati ya kutengeneza nyimbo kali kwa sasa, hata V. Money ameutendea haki.

Kama inavyofahamika V. Money ni msanii maarufu anayejituma na mwenye nyimbo nyingi zilizoshika umaarufu kama vile ‘Niroge’, ‘Come Over’, ‘Never Ever’ na ‘Kisela’ alioimba na Mr. P wa kundi la P Square kabla halijavunjika.

Kabla ya wimbo wa ‘Moyo’ kutoka, Vanessa alikuwa anatamba na vibao vya ‘That’s for Me’ na ‘Bambino’ alivyoviachia mwaka huu miezi kadhaa iliyopita.

Nyota yake ya muziki ilianza kung’aa rasmi mwaka 2011 alipopata nafasi ya kutumbuiza katika ufunguzi wa michezo ya TUSKER CECAFA CUP, ambapo shindano hilo lilimfungulia njia ya kukua kimuziki na kumpa nafasi ya kusainiwa na ‘lebo’ ya muziki ya BHitz akiwa kama msanii wa kwanza wa kike kusainiwa katika ‘lebo’ hiyo.

Wimbo wake wa ‘Closer’ aliouachia Januari 2013 unatajwa kuvunja rekodi ya nyimbo zilizokaa kwenye chati ya nyimbo za Bongo Fleva kwa kipindi kirefu, ambapo wimbo huo ulikaa kwenye chati kwa wiki 13.

Kutokana na wimbo huo kuwa na wapenzi wengi baada ya kuachiwa kwenye mitandao ulipakuliwa mara 30,000 ndani ya wiki moja ya kuachiwa kwake, rekodi ambayo haijavunjwa na msanii yeyote wa Bongo Fleva hadi leo.

Video ya wimbo wa ‘Closer’ baada ya kuachiwa kwenye mitandao inatajwa kumuongezea mashabiki pande zote za Afrika na duniani kote, kwani alianza kukubalika nchi zote za Afrika Mashariki, Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo (DRC) na zile za Afrika ya Kati na Magharibi hasa Nigeria.

Katika hali ya kuonyesha kukubalika kwake, V. Money ni msanii wa kwanza wa Bongo Fleva kualikwa nchini Nigeria mwaka 2013 kwenda kutumbuiza kwenye tamasha kubwa la muziki la Harp Rhythm Unplugged.

Katika hali inayoonyesha jina lake kushika kasi kwenye soko la muziki mwaka huo wa 2013 jina lake lilitajwa mara tatu katika Tuzo za Kilimanjaro Music Tanzania Awards (KMTA) na katika kinyang’anyiro hicho aliibuka na tuzo mbili.

Pia mwaka 2014 jina lake likatajwa tena mara tatu katika kuwania tuzo hizo za KMTA na kumfanya kuibuka na tuzo moja ya msanii bora wa mwaka wa nyimbo za RNB.