Serikali imepiga marufuku utengenezaji na usambazaji pombe maarufu kwa jina la ‘viroba’ kuanzia Machi mosi, mwaka huu.
Uamuzi huu umetokana na ukweli kuwa matumizi ya ‘viroba’ yalishavuka mipaka; na hivyo kuwa chanzo cha maovu na misiba nchini kote.
Hatua hii, licha ya ukweli kuwa imechelewa, bado inastahili kupongezwa kwani inafungua ukurasa mpya kwa afya za Watanzania, hasa vijana.
Matumizi ya pombe hizo yalishafikia kiwango cha kuathiri afya za watumiaji na upo ushahidi usiotiliwa shaka wa namna ilivyochangia ongezeko la ajali kwa magari mbalimbali na pikipiki.
Ulifika wakati ikaonekana kama vile hakuna Serikali, hivyo kila aliyeweza kununua kiroba alifanya hivyo na kunywa hadharani bila kuogopa mamlaka za nchi.
Matarajio yetu ni kuona kuwa uamuzi huu wa Serikali unatekelezwa kwa nguvu zote za kimamlaka, na kamwe haitakuwa ‘nguvu ya soda’.
Uamuzi huu unaweza kuibua manung’uniko kwa waliofaidika na biashara hiyo, lakini ni wazi kuwa Serikali imefanya hivyo baada ya kujiridhisha na ukubwa wa madhara ya viroba.
Pamoja na viroba, wananchi wapenda mazingira wangependa kuona Serikali ikitekeleza amri iliyotoa ya kupiga marufuku matumizi ya mifuko ya plastiki.
Matumizi ya mifuko hiyo yamechangia kwa kiwango kikubwa mno kuchafua mazingira katika maeneo yote ya miji na vijiji.
Pamoja na uchafuzi huo, taarifa za wataalamu zinasema matumizi ya mifuko katika kuhifadhia vyakula vya moto ni chanzo kingine cha maradhi, yakiwamo ya saratani. Utafiti huo unaweza kuwa na ukweli ndani yake kwa kuwa idadi ya watu wanaougua saratani inaongezeka kila uchao.
Serikali ya Mapinduzi Zanzibar imeweza kuzuia kabisa matumizi ya mifuko hiyo. Hatua hiyo imesaidia sana kulinda mazingira katika Visiwa vya Unguja na Pemba. Swali la kujiuliza, kama Zanzibar wameweza, kwanini Bara washindwe? Je, kwanini mambo mema ya upande mmoja yasiigwe na upande mwingine wa nchi?
Matarajio ya wananchi wengi ni kuona upigaji marufuku pombe za viroba na ule wa matumizi ya mifuko ya plastiki unatekelezwa kwa vitendo. Serikali ya Awamu ya Tano inapaswa kujitanabahisha kwa kuonesha vitendo zaidi badala ya maneno.
Tunaipongeza Serikali kwa hatua yake ya kulinda afya za wananchi. Afya za wananchi ni muhimu zaidi kuliko faida wanazopata watengeneza viroba na mifuko ya plastiki.