Desemba 8, mwaka huu, Taifa letu lilizindua kampeni ya Uzalendo hapa nchini. Uzinduzi ule ulifanyika Dodoma katika ukumbi wa Jakaya Kikwete na ulifanywa na Makamu wa Rais Samia Suluhu Hassan kwa niaba ya Rais John Magufuli. Hili ni jambo zuri na muhimu sana kwa Taifa kujitambua na kuwaandaa watoto, kizazi kipya wasipotoshwe na tamaduni za kigeni zinazoonekana katika ma-runinga.

Mwaka huu Taifa letu limesherehekea mwaka wa 56 wa Uhuru wetu. Ni kweli tumejikomboa kisiasa, lakini je, kiakili, kifikra, kiuchumi au kiutamaduni, Watanzania tumejikomboa kiasi gani?

Rais wetu nilimsikia katika hotuba yake kwa wananchi ile Jumamosi ya Desemba 9 kwenye kilele cha kusherehekea Uhuru wetu akitamka, “Nchi hii imetawaliwa na wageni wakoloni (wazungu) kwa muda wa miaka 76!”

Nikasema ndiyo maana Rais anaanzisha hii Kampeni ya Uzalendo, kumbe amelinganisha miaka ile 76 tuliyotawaliwa na hii 56 ya kujitawala kwetu akaona bado Watanzania hatujajikomboa kitaifa. Hatuna uzalendo, hatuna mila na utamaduni wa kitaifa unaoeleweka. Basi, heri kuanza kuamsha ari kwa vijana (to stimulate) wajengeke kimaadili na kuwa Watanzania kweli kwa maana ya neno hili “uzalendo” linavyojulikana.

Basi, nianze na kukumbushana hali tuliyokuwa nayo tulipotawaliwa na wakoloni. Wazungu walinyemelea nchi yetu kibiashara pale Mjerumani Karl Peters alipowahadaa wazee wetu kwa mikataba isiyoeleweka mwaka 1884. Kampuni ya Ujerumani iliyoitwa Dentsch Ost – Africa Geselleshaft iliweka makao yake makuu mjini Bagamoyo.

Kuona utajiri wa nchi yetu ulivyokuwa mwingi ndipo Kiongozi wa Ujerumani aliyeitwa Bismarck alijitwalia pande lote la nchi yetu katika ule mkutano wao wa Berlin 1885. Kuanzia hapo Tanganyika likawa koloni la Mjerumani. Gavana Mjerumani wa kwanza alitawala Tanganyika kuanzia mwaka 1891, Mjerumani huyu akiitwa Julius Von Soden. Lakini mwaka 1918 baada tu ya ile Vita Kuu ya Kwanza ya Dunia, mkoloni huyu Mjerumani aliondolewa na Tanganyika sasa ikakaliwa na Mkoloni mwingine ndiye Mwingereza.

Utawala wa Mwingereza ulikoma pale Tanganyika African National Union (TANU) ilipodai na kupewa Uhuru wa nchi hii Desemba 9, 1961. Rais wetu alipolikumbusha Taifa kuwa tumetawaliwa kwa muda wa miaka 76 nafikiri alihesabu toka ule utawala wa Mjerumani nchini tangu 1885 na akatolewa mwaka 1918 hapo ni miaka takribani (1918 – 1885) 33. Mkoloni Mwingereza huyu alidumu humu Tanganyika kuanzia mwaka 1918 hadi Desemba 9, 1961 takribani ni miaka 43!

Kwa hiyo wakoloni wametukandamiza kwa muda wote huo wa miaka 76 aliyoitaja Rais pale Dodoma.

Sasa hebu fikiria kwa muda wa miaka 76 Watanganyika wamekuwa wakipakiwa kasumba za uzungu tu. Mila na tamaduni za uzungu, lugha za kizungu, mavazi ya kizungu hapo badala ya kuwa Watanganyika tukawa tumeloea uzungu. Hatukuwa na hata chembe ya uzalendo wala maadili ya asilia maana kila kitu chetu wao walikiita ni USHENZI.

Mimi naona “mtima” wa utaifa wa asili kwa maana ya UZALENDO haukuwepo na wala hatukufikiria. Sote tulitamani tuwe kama wale wanaotutawala, tustaarabike kizungu kwa maneno mengine, tuwe kama wazungu ati!

Baba wa Taifa Mwalimu Julius Nyerere akaona iko hatari kwa taifa changa kukosa ule moyo wa utaifa na hasa hali ya uzalendo. Hapo akatoa angalizo mapema hata kabla ya Uhuru wa wananchi kupatikana. Alikiandika kijitabu kidogo akakiita “Barriers To Democracy” kikachapwa na rafiki yake Thakers wa P.O.Box 937 DSM.

Katika ukurasa wa kwanza tu wa kitabu kile tunasoma maneno ya angalizo haya, nayanukuu: “Of all the multi – ratial countries in Africa, none has the opportunities which Tanganyika has to establish a lasting self – governing democracy. The European community is so small and so heterogeneous, that unlike the larger and more homogeneous whitecommunities in Kenya and in the Rhodesia (leo Zambia na Zimbabwe), it can never seriously entertain hopes of dominating the non – European community.

“The Asian Community is a business community and could not, even if it had the desire ever dominate the other communities. Both these communities are hardly 2% of the total population. If every non – African vote were to be magnified by law to count for ten African votes, the non – African Votes could still be insignificant compared with African Votes. The African knows this and therefore although he has his own prejudices against the two migrant communities, he is not afraid of them…” (Nyerere: Barriers to Democracy uk. 1).

Maneno haya ya Mwalimu kabla ya Uhuru yalimaanisha kuwahakikishia wazawa (Africans) kuwa utawala wao wananchi hapa Tanganyika hautaathirika na wakazi wageni (hapa amewaita “the two migrants” yaani Wazungu na Waasia) ambao kiuhalisia siyo wazalendo (patriots) bali ni wageni (aliens).

Ikaja siku ya Uhuru, tuliosherehea Desemba 9, 1961. Waafrika hawakujiamini maana walikuwa bado wana woga woga (inferiority complex) ndipo wakachachamaa kudai Serikali ya TANU iwainue Waafrika na hapo wakaleta dai la kile kinachojulikana kama “Africanisation” katika Serikali yao. Waafrika walitaka Serikali yao mpya isiyo kuwa na mseto wa Wazungu na Waasia.

Kilichokuwa kinadaiwa ni UTAMBULISHO WA UZAWA wao ambao mimi hapa ndio nauita UZALENDO. Kutokana na madai yale, Mwalimu alihisi kuna ombwe katika Utanganyika wetu, kuna kitu kinakosekana nacho ni ile hali ya kujiamini uzawa wako katika nchi na katika Taifa. Kitu kile kilichokosekana ndicho leo tunakiita uzalendo – upendo wa nchi, uchungu wa nchi ambamo wewe mtu umezaliwa. Pale familia yako imejengeka, pale ukoo wako una kitovu chake na pale kabila lako limeotea mizizi yake.

Sasa basi, Serikali ya TANU imetuunganisha sote tumekuwa Taifa la Tanganyika. Tumejengeka kifikra baada ya Uhuru tukawa Watanganyika. Kwa ujumla wetu wote Waafrika, Wazungu na Waasia ndio tuliostahili kuitwa Watanganyika mara tu baada ya Uhuru.

Yakatokea mambo yasiyofanana na ule Utanganyika. Wale wenye elimu na kazi nzuri wakaanza kuonesha kasumba za uzungu na kuwa kama Wazungu kimatendo ingawa walikuwa Waafrika weusi. Mathalani, walianza kuchukia majina yao ya asili na kuijigeuza yasikike kizungu kizungu au kiarabu-arabu. Mtu akiitwa Athuman sasa akajiita Outhmann. Mzaramo akiitwa Ngalewa, sasa akaja akajiita Ngalewason, Mndengereko wa Rufiji akiitwa Bwana Mngumi sasa anajiita El Mugh’umi na Mchaga akiitwa Robati sasa anajiita “Roberts” ili mradi asikike kizungu.

Hapo ndipo Serikali ya TANU ikaona kuna ulazima au ipo haja ya kuwajengea Watanganyika weusi ari ya kujiamini na kujivunia utaifa wao. Wajengewe mazingira ya kujitambua kuwa utu wao unatokana na kuzaliwa kwao humu humu nchini. Wajijue, wajitambulishe kwa moyo wao wa utaifa. Hapo ndipo likaja neno hili la UZALENDO – “uenyeji” wa hapa hapa nchini wala siyo suala la uzawa tu. Maadamu umezaliwa katika nchi hii, basi wewe ni Mtanganyika. Lakini unaweza usiwe Mzalendo!

Mwaka huu Taifa linapotukumbusha uasilia wetu na kutuletea kampeni hii ya uzalendo naona ni wakati mwafaka sisi tujitambue tuko wazalendo wa nchi hii na tuoneshe matendo hayo ya kizalendo.

Inafaa hapa kuonesha asili ya hili neno UZALENDO. Sisi Watanzania tulitafsiri neno lile la kizungu – “PATRIOT” toka kwa Waingereza. Kumbe hao Waingereza walilitoa kwenye Taifa la Wagiriki. Hawa Wagiriki wana ustaarabu wa miaka mingi sana. Wao na Warumi wameleta maneno mengi katika mataifa mbalimbali.

Basi kule Ugiriki neno hili linaitwa “PATRIŌETĒS” likiwa na maana ya “wa nchi yangu” mwenzangu wa nchi moja nami. Kumbe enzi zile Wagiriki walikuwa wabaguzi. Wao kwa wao wakajiita “patriots”, lakini wakazi wageni (imigrants) kutoka mataifa mengine kama Wajerumani, Wataliano, Warusi, Waturuki na kadhalika wakawapa jina jingine – hawa wakawaita “ALIENS” neno hili asili yake ni kwa Warumi – maana neno la kilatini ni “ALIENUS” likiwa na maana “mgeni”.

Hapo tunaona Wagiriki ambao walikuwa ni wenyeji wazawa ndio wakiitwa “patriots” – “wazalendo” na wageni wote wakiitwa “Aliens”. Kuanzia hapo maneno hayo mawili yamekuwa yanatumika katika mataifa mbalimbali ulimwenguni. Sisi nasi tukalikwaa neno hilo la “patriot” kutoka watawala wetu Waingereza na tukalitafsiri kwa Kiswahili chetu tukapata hili neno “MZALENDO”.

“Mzalendo” basi ni mzawa wa nchi hii na anatofautiana na mtu wa kuja ambaye Baba wa Taifa alimwita “immigrant” siku zile za kudai Uhuru wetu.

Haishangazi katika Taifa lolote kuwa na makundi namna hiyo ya wakazi katika nchi. Sisi hapa Tangamyika hata miongoni mwa makabila yetu tuna ka-ubaguzi ka-utambulisho namna hiyo. Mathalani, kule Kagera yeyote asiyekuwa mzawa kule wenyeji wa Kagera wanamwita “NYAMAHANGA”. Ukienda Kilimanjaro nako usipokuwa mzawa kule utaitwa “CHASAKA”, kule Songea Wangoni watakuita “MHENJA” nenda Mtwara Wamakuwa watakuita “ALETO” wakati Wayao wataita “ACHALENDO”.

Itoshe hapa niseme tu hata mataifa yale ya Ulaya kuna lahaja (dielects) mbalimbali katika kila Taifa ingawa wenzetu hawakutumia neno makabila. Uingereza, mathalani, wapo Waingereza (the English) wapo Wawelsh (Wales) wapo Waskoti (Scotish) na wao wa Airishi (Irish) wote hao kwa utaifa wao ni BRITISH – Waingereza kwa ujumla wao. Ujerumani wapo wale wa kusini Wabavaria na wapo wale wa Kaskazini Waprasha (Prussians). Ubelgiji wapo wa Kusini asili ya Ufaransa na wapo wa Kaskazini asili ya Uholanzi (Flenish). Ikija kwenye utaifa, basi wote ni Wajerumani au ni Wafaransa kimila na kiutamaduni.

Ukienda Marekani ndipo utachoka. Kule kuna mseto wa mataifa yote ya ulimwenguni – Waingereza, Wafaransa, Waholanzi, Wagiriki, Wapolandi, Wajerumani, Wataliano, Wachina, Wakapani, Wahindi Wekundu mpaka Wabantu wa Afrika ambao kule wanaitwa Manigro. Lakini pamoja na mseto wote huo Marekani na Wazungu kwa ujumla wao wamejijengea utamaduni au hali ya UZALENDO mkubwa kabisa.