Uananchi na utaifa wa mtu ni hali mbili ambazo zinamjenga kutokana na mapenzi mazito, ridhaa na ari moyoni ya kufanya jambo jema na kumsukuma kuwa tayari afe kwa ajili ya kuitetea nchi yake. Mtu wa aina hii ndiye hasa aletaye maendeleo ya taifa au nchi yake. Huyu ndiye mzalendo.
Narudia kukumbusha: “Mzalendo ni mtu anayeipenda nchi yake kwa moyo wake wote kiasi cha kuwa tayari kuipigania.” Hapa ninasema wazi wapo baadhi ya watu wanapenda kuwabughudhi wananchi kwa kisingizio cha uzalendo. Wananchi tuwe makini na fasili ya uzalendo.
Uzalendo haufundishwi kama ualimu, udereva au uashi kwa mtu kuwa na taaluma yake. Wala haushurutishwi kwa mtu kama adhabu.
Uzalendo ni ridhaa ndani ya moyo wa mtu. Na utekelezaji wake una mikondo mingi mbalimbali ya kuleta maendeleo kwa nchi au taifa.
Katika lugha yetu ya taifa – Kiswahili, mzalendo ina maana ifuatayo: Mtu anayeipenda nchi yake kwa moyo wake wote kiasi cha kuwa tayari kuipigania.
Mtu mwenye asili ya mahali fulani kwa kuzaliwa kuwa raia, mzawa, mwananchi, mzaliwa, mzalia. ( Angalia Kamusi Kuu ya Kiswahili, UK. 796 ).
Nchi au taifa linapata maendeleo makubwa ya kiuchumi, kisiasa na kijamii kutokana na wananchi wake wenye mioyo ya kujenga taifa lao huku wakiweka masilahi ya taifa kwanza, kwa sababu “hiari ya moyo yashinda utumwa.”
Watu hufanya kazi kwa kuridhia, bila kushurutishwa. Nidhamu hii huleta ufanisi mkubwa na kutoa fasili halisi ya demokrasia ya kweli na kuwaweka wananchi katika amani na utulivu.
Si hivyo tu, mihimili ya dola; Serikali, Bunge na Mahakama inapata ahueni katika kusimamia na kutekeleza wajibu wao.
Ni imani basi, kuona Bunge linafanya kazi zake kwa kuangalia masilahi ya jamii (wananchi), matumizi ya fedha na utekelezaji kazi wa serikali, ili wananchi wazidi kujenga imani kwa serikali yao. Kwenda kinyume cha haya ni kuitia serikali na wananchi katika mtafaruku. Hili si jambo jema.
Katika nchi inayohitaji maendeleo ya kiuchumi na kijamii, viongozi wake huwa makini katika kuzungumza, kupanga mipango ya maendeleo na kuhudumia raia wake.
Sera na itikadi za chama au vyama vinavyoendesha serikali husifika na kupewa hongera. Na hii ndiyo raha ya uongozi.
Viongozi wanaojaribu kutumia uzalendo kuweka vizingiti vya masilahi baina ya serikali na wananchi, hawa hawatufai katika safari yetu ya kuendea maendeleo. Njia ya maendeleo haitakiwi kuwa na mazonge mazonge. Hali hii imejitokeza hivi majuzi katika kuingilia masilahi ya wananchi.
Uzalendo una maana na umuhimu wake katika ujenzi wa taifa. Kuumiza watu katika tozo kali kwa kigezo cha uzalendo haikubaliki. Uzalendo hauletwi na mtu kwa mtu. Ni mtu mwenyewe ndiye anayejenga uzalendo ndani ya moyo wake.
Binafsi, nimefarijika kusikia serikali imechukua hatua ya awali ya kusikia na kufuatilia tozo hizo na kuzipatia ufumbuzi mzuri kwa mtoa na mpokeaji tozo. Hapa cha msingi ni kuwa na subira. Wakati tukiwa ndani ya subira, uzalendo wetu usiyumbishwe na wale wanaopandikiza uzalendo.
Naamini kushauri ni jambo jema. Mara kadhaa nimepata kusikia ‘uzalendo’ unavyotumika katika masuala ya michezo, ushirika, kazi za kujenga taifa n.k.
Watu wanaambiwa kufanya kazi kwa kujitolea; wakifanya hivyo ndio uzalendo, huku masilahi yakiminywa na pengine kutumiwa na hao washawishi.
Si vema baadhi ya viongozi wetu kutumia mwanya wa kukandamiza wananchi kwa kisingizio cha uzalendo. Tusipoteze maana na umuhimu wa uzalendo na mzalendo. Uzalendo umo ndani ya moyo wa mtu.