๐ Wateja wapya 109,918 waunganishiwa na huduma ya umeme nchini
๐ Kamati ya Bunge yaipongeza TANESCO kwa kuimarisha Miundombinu ya umeme
Na Mwandishi Wetu, JamhuriMedia, Dodoma
Serikali kupitia Shirika la Umeme Tanzania (TANESCO) limesema kuwa uwezo wa mitambo ya kufua umeme iliyounganishwa katika mfumo wa Gridi ya Taifa hadi kufikia mwezi Desemba, mwakajana ni jumla ya Megawati 3,091.71 ikilinganishwa na Megawati 2,842.96 zilizokuwepo mwezi septemba, 2024 ikiwa ni ongezeko la Megawati 248.75 sawa na asilimia 8.75.
Kauli hiyo ilitolewa na Naibu Waziri wa Nishati, Judith Kapinga Januari 16, 2024 jijini Dodoma, wakati wa kujadili taarifa ya Wizara ya Nishati kuhusu hali ya uzalishaji na usambazaji wa umeme nchini kwa kipindi cha kuanzia mwezi Septemba hadi desemba, 2024 kwa wajumbe wa kamati ya kudumu ya Bunge ya Nishati na Madini.
โOngezeko hilo lilitokana na kuingia kwa Megawati 235 kutoka katika Mradi wa JNHPP pamoja na mitambo ya Kigoma kuingia kwenye Gridi ya Taifa.โ Smesema Mhe. Judith Kapinga
Ameeleza kuwa, Shirika la Umeme Tanzania (TANESCO) katika hatua nyingine limeendelea na ukarabati mitambo mbalimbali ya kuzalisha umeme ikiwemo ile ya Kihansi, Kidatu pamoja na Ubungo ili kuwezesha Taifa kuwa na umeme wa uhakika muda wote.
Aidha, Kapinga amesema kuwa hali ya miundombinu ya kusafirisha na kusambaza umeme nchini inaendelea kuwa nzuri jambo ambalo limechangia upatikanaji wa umeme wa uhakika kwa wateja na miundombinu hiyo inayojumuisha njia za kusafirisha umeme zenye jumla ya urefu wa kilomita 8, 025.38 pamoja na njia za kusambaza umeme zenye urefu wa kilomita 197, 597.34.
Kupitia miundombinu hiyo, Shirika limeweza kuunganisha wateja wapya 109,918 ndani ya kipindi cha kuanzia mwezi Septemba, 2024 hadi mwezi Desemba, 2024. Ongezeko la wateja hao limewezesha jumla ya wateja waliounganishiwa umeme nchini kufikia 5, 225, 193.
Kwa upande wake, Mwenyekiti wa Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Nishati na Madini, Mhe. David Mathayo David ameipongeza Wizara kupitia Shirika la Umeme Tanzania (TANESCO) kwa kuendelea kuimarisha miumbombinu mbalimbali ya uzalishaji, usambazaji na usafirishaji wa umeme katika maeneo mbalimbali nchini.